Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-03-03 20:31:14    
Maisha ya Bi. Shi Juan katika sehemu ya magharibi mwa China akiwa mwalimu wa kujitolea

cri

    Mwaka 2004, Bibi Shi Juan aliamua kuacha kazi yake katika idara ya sheria mjini Shenzhen, kusini mwa China na kwenda kuishi katika sehemu ya mlimani ya magharibi mwa China akiwa mwalimu wa kujitolea. Watu wengi hawawezi kufahamu ni kwa nini yeye aliacha maisha mazuri ya mjini na kuanza kufanya kazi katika kijiji cha mlimani mkoani Guizhou, magharibi mwa China? Jibu lake ni rahisi, akisema:

    "Mimi napenda kuishi pamoja na wanafunzi hao, na kuwafundisha ili kubadilishana nao mawazo yao ya kimaisha. Natumai kuwa juhudi zangu zitawafahamisha umuhimu wa ujuzi."

    Katika China ya leo, watu wengi zaidi wameanza kuwa na wazo kama Bibi Shi Juan alivyokuwa, wakitumai kujishirikisha katika kazi za kutoa huduma za kijamii kwa vitendo vya kujitolea. Katika miaka ya hivi karibuni, idara za serikali au zisizo za serikali kila mwaka huwashirikisha watu wanaotaka kujitolea na kuwatuma katika sehemu za magharibi ambazo ziko nyuma kiuchumi kufanya kazi za huduma za elimu, matibabu, uzalishaji wa kilimo, utoaji huduma za kisheria na usimamizi wa utawala. Ilipofika mwishoni mwa mwaka jana, idadi ya watu wanaojitolea katika sehemu za magharibi ilifikia elfu 20.

    Akiwa mmoja wa watu wanaojitolea, Bibi Shi Juan alisema kuwa, uamuzi wake ulitokana na kuathiriwa na watu waliotangulia. Japokuwa alikuwa anaishi maisha mazuri mjini, lakini moyoni mwake yeye hufikiria jinsi ya kufanya shughuli zinazoweza kuwasaidia watu wanaohitaji misaada, na uelewa na uungaji mkono wa mume wake pia umemtia moyo zaidi.

    Mume wa Bibi Shi Juan anaitwa Zhang Weisong, yeye pia anafanya kazi katika idara ya sheria mjini Shenzhen. Akiwa mtu aliyezaliwa kijijini, yeye anaelewa vizuri matatizo wanayopata watoto wa vijijini kwenda shule kutokana na matatizo ya kiuchumi ya sehemu iliyoko pembezoni. Hivyo anamwunga mkono mke wake kushughulikia elimu katika sehemu ya magharibi. Alisema :

    "Mimi namuunga mkono mke wangu afanye kazi anavyopenda. Uamuzi wake wa kwenda katika sehemu ya magharibi kuwa mwalimu wa kujitolea ni muhimu. Anaweza kutumia ujuzi wake, uzoefu wa maisha yake na athari yake kubadilisha maisha ya watoto wa sehemu ya mlimani."

    Shule ya msingi anayofundishia Bibi Shi Juan iko katika sehemu ya milimani mkoani Guizhou, kwenye mita zaidi ya 2000 juu ya usawa wa bahari. Shule hiyo ina majengo matano yasiyo na ghorofa, ina wanafunzi 170, na kipande cha chuma kinatumika kama kengele ya shule hiyo.

    Kila siku Bibi Shi Juan ndiyo anaingia darasani kutokana na kengele hiyo. Alipokuwa chuo kikuu alisomea sheria, hivyo si vigumu kwake kuwafundisha somo la kichina wanafunzi wa darasa la nne. Licha ya kuwafundisha wanafunzi mambo yaliyoandikwa kwenye kitabu, pia anajaribu awezavyo kuwafahamisha mambo ya dunia.

    Kuwafundisha watoto wa mlimani ndiyo maisha ya Bibi Shi Juan, aliagana na maisha ya mjini. Kwenda kuishi katika mazingira asiyofahamu kumempa maisha mapya na yenye furaha kubwa. Anapenda ukimya maalum wa mlimani, anapenda mto unaotiririka chini ya mlima, na kuwapenda wanakijiji wa huko.

    Wanakijiji pia wanampenda sana Bibi Shi Juan kutoka mjini, mwanakijiji Bwana Yang Chongkuan alisema:

    "Yeye ni mwanamke, amekuja kwetu hapa kutoka mji mkubwa wa Shenzhen, anajaribu kupambana na maisha magumu ya kwetu, tunamheshimu sana."

    Wanafunzi wake ndiyo wana furaha kubwa zaidi, wanampenda sana mwalimu wao Shi, na kueleza upendo wao kwa njia maalum ya watoto wa mlimani, wanafunzi hao humletea mwalimu wao chakula cha kienyeji na maua. Bibi Shi Juan alisema kuwa, yeye hujisikia vizuri sana anapokuwa pamoja na wanafunzi wake wapendwa.

    Lakini mara kwa mara yeye humfikiria mtoto wake wa kiume ambaye mwaka huu ana umri wa miaka 6 tu, yeye hana njia nyingine ila tu kumpigia simu mtoto wake. Lakini mawasiliano ya simu kwenye sehemu za milimani si nzuri, kila anapotaka kupiga simu, anapaswa kusimama juu ya paa la nyumba. Kwenye simu, mtoto wake mwenye hamu ya kufahamishwa hali ya watoto wa milimani humwuliza masuali mengi kuhusu jinsi watoto wa milimani wanavyosoma na kuishi.

     Maisha ya muda mfupi ya kujitolea yamemfahamisha zaidi sehemu ya magharibi mwa China. Matakwa ya watoto wa milimani ya kujifunza yamemsisimua sana Bibi Shi Juan, hivyo yeye hajuti hata kidogo uamuzi wake wa kuacha maisha ya mjini na familia yake na kuwa mwalimu wa kujitolea milimani.

Idhaa ya Kiswahili 2005-03-03