Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-07-07 20:20:12    
Jumuiya ya mitaa ya China yatoa huduma bora kwa wakazi

cri

Kutokana na maendeleo ya haraka ya kimji nchini China, ujenzi wa mitaa mijini umepata maendeleo makubwa, ambayo yameonekana dhahiri katika huduma za mitaa kama vile matibabu, kuwahudumia wazee nyumbani na kushughulikia watu waliofanya makosa ya kukiuka sheria waliohukumiwa kurekebishwa mienendo yao mitaani.

Katika mtaa wa Zhenwushan wa mji wa Chongqing, kusini magharibi mwa China, mwandishi wetu wa habari aliona kuwa, kituo cha matibabu cha mtaani kimewarahisishia sana wakazi kuonana na daktari. Mkazi wa mtaa huo Bi. Cao Yingfang alisema kuwa, licha ya kuwahudumia wagonjwa, kituo hicho cha tiba pia kimeweka kadi ya afya kwa kila mkazi na kuwafanyia upimaji wa afya kila baada ya muda Fulani. Anasema:

"Kituo cha tiba cha mtaa wetu kinatuhudumia vizuri sana, pia kinatoza gharama ndogo zaidi kuliko hospitali kubwa. Kila mwaka kituo hicho kinafanya upimaji wa afya mara mbili kwa wakazi wote wa mtaani bila gharama yoyote."

Huduma za tiba ni moja ya huduma za mitaani zinazohimizwa katika miji ya China. Zamani kamati ya wakazi kwenye mitaa ilitoa huduma za kupokea barua au kukusanya ada ya usafi ya kila familia. Katika miaka ya karibuni, kutokana na kuharakisha mchakato wa uendelezaji wa kimji, mambo yaliyomo kwenye huduma za mitaani yanaongezeka siku hadi siku. Mitaa mingi ya mijini imeweka vituo vya tiba ili kutosheleza mahitaji ya wakazi. Beijing imekuwa na vituo zaidi ya 700 vya tiba vya mitaa, na kuunda kimsingi mtandao wa utoaji huduma za tiba mjini kote.

Kuhusu shughuli za kuwahudumia wazee nyumbani. Zamani wazee wa China walikuwa wanawategemea watoto wao au kwenda kwenye nyumba maalum za kuwatunza wazee. Hivi sasa shughuli za kuwahudumia wazee nyumbani zimekuwa huduma ya aina mpya inayokaribishwa sana na wazee, ambapo wazee wanaweza kupata uangalizi mzuri kutoka kwa watumishi wa nyumbani na kuishi maisha yao ya uzeeni kwa furaha katika mazingira waliyoyazoea. Mtaa wa Qinan wa Beijing mwaka jana ulianzisha "nyumba ya kuwatunza wazee bila ukuta", yaani wazee wa mtaa huo wanaweza kupata huduma kama zile za nyumba maalum ya kuwatunza wazee wakiishi nyumbani kwao, watumishi wanatoa huduma husika kutokana na mahitaji halisi ya kila familia yenye mzee au wazee. Mzee Wang Shiliang wa mtaa huo anasema:

"Mimi naishi nyumbani pamoja na watoto wangu, nafurahia huduma zilizotolewa na jumuiya ya mtaa huu, zinazofanana na zile za nyumba maalum ya kuwatunza wazee bila kuondoka kwenye mazingira niliyoyazoea."

Licha ya kutoa huduma kwa wakazi wa kawaida, jumuiya kadhaa za mitaa nchini China pia zinatoa msaada kwa ajili ya watu waliofanya makosa ya kukiuka sheria kujikosoa na kujirekebisha mtaani. Kuanzia mwezi Julai mwaka 2003, watu waliofanya makosa madogo ya kukiuka sheria, au wale watakaopunguziwa kifungo kutokana na mwenendo mzuri wataruhusiwa kusimamiwa na jumuiya ya mitaa wanayoishi badala ya kufungwa gerezani. Hivi sasa mji wa Beijing na mikoa ya Shangdong, Jiangsu na mingineyo imeanzisha huduma ya kuwasaidia watu wa aina hiyo. Mjini Beijing, watu zaidi ya 4000 wanapokea huduma hiyo. Wafanyakazi wa jumuiya ya mitaa wanawasiliana nao mara kwa mara ili kuwasaidia wajikosoe na kujirekebisha chini ya usimamizi wa mitaa. Mtaalam wa elimu ya jamii wa Beijing Bwana Zhou Zhengji alipongeza sana kazi hiyo ya mitaani. Anasema:

"Kwa upande wa kiutu, watu watasikia shinikizo la kiroho wakifungwa gerezani. Baada ya kumaliza kifungo gerezani na kurejea kwenye jamii, huenda watashindwa kuwasiliana na watu wengine kwa njia ya kawaida. Kuwawekea chini ya usimamizi wa mitaani na kuwahimiza wajikosoe na kujirekebisha kunaweza kuwasaidia warejee kwenye maisha ya kawaida ya jamii kwa urahisi."

Ili kuboresha huduma za mitaani, baadhi ya miji pia imeanzisha kituo cha huduma za mitaani cha mji mzima. Kwa mfano kituo cha huduma za mitaani cha Beijing kimeweka mfumo wa simu kutoa huduma za mitaani, ambapo unakusanya pamoja namba za simu maalum za mitaa mbalimbali. Kituo hicho kikipokea simu za wateja wanaohitaji huduma huwaarifu watumishi walio karibu na wateja kutoa huduma zilizohitajika, kama vile kufanya kazi za nyumbani, kufanya utengenezaji na kuondoa matatizo nyumbani, kutoa huduma za kiutamaduni, matibabu na kutoa ushauri wa kisheria.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara ya mambo ya raia ya China, muda si mrefu baadaye serikali ya China itatoa waraka kuhusu kuimarisha huduma za mitaani ili kutoa huduma nzuri zaidi kwa wakazi.