Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-08-08 16:58:00    
Mwimbaji Mashuhuri wa Kabila la Watibet Dan Zeng

cri

Kabila la Watibet ni moja kati ya makabila 56 ya China, watu wa kabila hilo ni hodari katika kuimba na kucheza ngoma, watu husema, "Mtibet yeyote anayeweza kuongea anaweza kuimba, na anayeweza kutembea anaweza kucheza ngoma."

"Theluji imelundikana mlimani, maji ya theluji yanarutubisha majani, wafugaji wanafurahi moyoni......" Huu ni wimbo ambao mwimbaji Dan Zeng anaupenda na ameuimba kwa miaka mingi, hakutegemea kama wimbo huo ungempatia umaarufu duniani.

Dan Zeng alizaliwa katika ukoo maskini, wazazi wake hawakusoma sana, lakini walijitahidi kumsomesha yeye. Baada ya kuhitimu elimu ya sekondari ya juu Dan Zeng alijiunga na idara ya usanii ya Chuo cha Ualimu cha Tibet na kusomea muziki wa jadi wa Tibet.

Mwaka 1981 Den Zeng alipohitimu alichaguliwa na Kikundi cha Nyimbo na Dansi cha Tibet na kuwa mwimbaji. Baada ya nusu mwaka alijiunga na Chuo Kikuu cha Muziki cha Shanghai, ambacho ni chuo maarufu cha muziki nchini China.

Bw. Dan Zeng alipokumbuka alipokuwa katika chuo kikuu hicho alisema, alikuwa mwanafunzi pekee wa kabila la Watibet katika darasa lake, na mwanzoni alikuwa akishika mkia kati ya wanafunzi wenzake katika uimbaji. Alisema, "Nilipokuwa nasoma katika Chuo Kikuu cha Muziki cha Shanghai nilitunzwa sana. Kutokana na kuwa msingi wangu wa uimbaji ulikuwa hafifu, walimu walinifundisha zaidi nje ya darasa."

Baada ya miaka minne, Dan Zeng alihitimu kwa matokeo ya nafasi ya pili katika mtihani wa darasa lake. Mwaka 1985 Dan Zeng alipata tuzo ya kwanza katika mashindano ya taifa ya waimbaji wa kikabila. Na tokea hapo katika muda wa miaka 15 alipata tuzo mara kumi kadhaa katika mashindano mbalimbali ya waimbaji.

Kuanzia miaka ya 90 ya karne iliyopita Dan Zeng akiwa pamoja na wasanii wengine, alionesha nyimbo zake katika nchi zaidi 20 za Asia, Ulaya, Amerika ya Kaskazini na Kusini, kwa nyimbo zake aliwafahamisha utamaduni wa Tibet ulivyo. Dan Zeng alisema, "Tibet inasifiwa kuwa ni bahari ya nyimbo na dansi, watu wa Tibet kizazi kwa kizazi wanaishi katika sehemu ya "paa la dunia" na wamevumbua utamaduni mkubwa. Watu wa nchi za nje wengi hawakuwahi kutembelea Tibet, hawajui utamaduni wake. Tulipopanda tu jukwaani mara makofi yakaanza kupigwa, na baada ya kumaliza kuimba, watu wote wakasimama na kutushangilia kwa muda mrefu."

Dan Zeng alisema, michezo yake pia iliwabadilisha mawazo watu wasiofahamu hali ya hivi sasa ya Tibet kutokana na kukaa katika nchi za nje kwa muda mrefu. "Tokea mwaka 1951 Tibet ilipokombolewa kwa amani hadi sasa, mabadiliko makubwa yametokea, lakini Watibet walioishi katika nchi za nje kwa muda mrefu waliathiriwa na propaganda nyingi, na hawafahamu ukweli ulivyo mkoani Tibet. Mwanzoni nilipokutana nao, watu hao walikuwa hawana urafiki nami. Baada ya kutizama michezo wakaamini kuwa utamaduni wa Tibet kweli bado upo, na wanataka kutembelea kwetu kuona hali ilivyo."

Kutokana na shughuli nyingi, kila mwaka Dan Zeng hawezi kukaa na jamaa zake kwa nusu mwaka. Lakini mkewe alipomzungumzia mumewe aliona fahari, akisema, "Yeye ni mume mzuri, na wenzake wote wanaona kuwa yeye ni mume mzuri wa kuigwa. Anapokuwa nyumbani anafanya kazi zote za nyumbani. Mimi naunga mkono kazi yake."

Mwaka jana katika likizo ya sikukuu ya taifa Dan Zeng kwa mara ya kwanza alionesha michezo pamoja na binti yake anayesoma katika shule ya dansi iliyo chini ya Chuo Kikuu cha Muziki cha Shenyang. Dan Zeng alisema, ameridhika sana na uhodari wa binti yake katika michezo. Dan Zeng alisema, akiwa mwimbaji wa kabila la Watibet ataendelea kutoa mchango wake kwa ajili ya watazamaji wa nchini na nchi za nje, akiwa profesa mwalikwa wa Chuo Kikuu cha Tibet atajinyima muda mwingi ili awafundishe zaidi vijana kwa elimu yake, uzoefu wake na ufahamu wake kuhusu uimbaji.

Idhaa ya kiswahili 2005-08-08