Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-12-12 16:11:14    
mji mdogo Mudu

cri
Katika sehemu ya magharibi ya Suzhou ambao ni mji maarufu wenye vivutio vya utalii, kuna mji mdogo unaoitwa Mudu. Mji mdogo wa Mudu unaegemea kwenye Mlima Lingyan, ambapo mito miwili midogo Xiangxi na Xujiang inapita?ambapo mabustani ya kale yaliyotapakaa kwenye sehemu mbalimbali mjini humo, yameuongezea mji huo mdogo hali ya utulivu na ya kupendeza.

Jina la mji huo Mudu, maana yake ya kichina ilitokana na hadithi iliyosimuliwa zaidi ya miaka 2000 iliyopita, ambapo kulikuwa na Dola Wu na Dola Yue. Siku moja madola hayo mawili yalipambana kivita, Dola Wu lililishinda Dola Yue. Mfalme wa Dola Yue alitaka kulipiza kisasi, akimtuma msichana mrembo aitwaye Xishi kwenda kwenye Dola Wu kumtumikia mfalme wa Dola Wu.

Mfalme huyo alimpenda sana Xishi, akamjengea Jumba kubwa kwenye Mlima Lingyan, ili kumfurahisha, hata mfalme wa Dola Wu aliwataka wajenzi watumie miti kutoka Dola Yue kumjengea Xishi Jumba hilo. Ndiyo maana miti mingi iliyosafirishwa kutoka kwenye Dola Yue hadi kwenye Dola Wu ambayo iling'ang'ania kwenye mto Gangdu na kuuziba mto huo kwa miaka mitatu. Neno miti, kichina ni Shu, mu au mutou, Mutou iliziba Mto Gandu, hivyo sehemu hiyo ikaitwa Mudu.

Baada ya kuishi kwenye Jumba la Guanwa, Xishi na wasichana wahudumu wake kila siku walitumia maji ya mto kunawa uso, ilisemekana kuwa Xishi na wasichana hao kila siku walitumia manukato, maji ya mto waliyotumia kila siku pia yakawa na harufu nzuri ya manukato, hivyo siku za baadaye mto huo ulioelekea chini ya Mlima Lingyan ukaitwa na watu kuwa Xiangxi, maana yake ya kichina ni mto wenye harufu nzuri ya manukato, siku baada ya siku, Xiangxi pia ikapewa jina lingine la Mudu. Mbali ya Xiangxi, huko Mudu pia kuna mfereji mmoja Xujiang. Mkuu wa mji wa wilaya Mudu Bwana Wang Weimin alisema, huko Mudu kuna hadithi nyingi zinazosimulia kila mto na kila daraja. Akisema:

Mto Xu mjini Mudu ulikuwa mfereji uliojengwa na Jemadari Wu Zixu akiongoza askari. Mfereji huo ulipita kwenye Mlango wa Xu wa Suzhou na Ziwa Taihu, halafu kuingia kwenye Mto Changjiang. Mfereji huo ulikuwa njia muhimu ya kimkakati wakati wa zama za kale, pia ulikuwa mfereji wa kwanza wa China kujengwa kwa nguvu za binadamu. Mito Xiangxi na Mto Xujiang yenye tofauti ilikutana mjini Mudu.

Mudu ni mji mdogo wenye mtindo dhahiri wa sehemu ya kusini iliyoko kando ya Mto Changjiang, makazi mengi ya mji huo mdogo yalijengwa kando ya mto, "Milango ya nyuma ya nyumba inakaribia milima, na milango ya mbele ya nyumba inaegemea mto, wakazi wa mji wanalala karibu na mto", hii ni mandhari pekee ya mji wa Mudu. Mjini humo kuna madaraja mbalimbali yenye maumbo tofauti, ambayo yanawavutia sana watalii.

Mtaa wa Shantang wenye urefu wa zaidi ya mita 800 ni njia muhimu zaidi mjini Mudu, ambapo kuna bustani binafsi na maduka mengi, hayo yote yanaonesha kuwa mtaa huo ulikuwa na shughuli nyingi za kibiashara tangu enzi na dahari. Naibu meneja mkuu wa kampuni ya utalii ya Mudu Bwana Zhou Jukun alisema:

Mji wa kale wa Mudu uko sehemu muhimu ya Ziwa Taihu na Mji maarufu Suzhou, hadhi yake ya kijiografia ni muhimu sana. Katika zama za mwishoni mwa Enzi ya Ming na mwanzoni mwa Enzi ya Qing, sehemu hiyo ilikuwa kituo kikubwa cha biashara cha magharibi ya Suzhou.

Bwana Zhou alifahamisha kuwa, ili kuonesha mandhari ya zama za kale za Mtaa Shantang, mwaka huu na mwaka kesho serikali ya huko itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi ili kuonesha sura ya kihistoria ya Mtaa Shantang. Baada ya kukamilisha ujenzi, milima na mito, mabustani na mji wa kale vitapatana na kuwavutia watalii wengi zaidi.

Zaidi ya miaka 600 iliyopita, mjini Mudu kulikuwa na mabustani 30 binafsi, na mabustani zaidi ya 10 kati ya hayo bado yapo. Ujenzi wa mabustani hayo binafsi si kama tu ulifuata mtindo wa ujenzi wa mabustani maarufu ya Suzhou, bali pia ulionesha mitindo tofauti ya wamiliki wa mabustani hayo, na mabustani hayo yaliyoko sehemu ya milima pia yana vivutio vya kipekee.

Miongoni mwa mabustani hayo, bustani ya Familia ya Yan ni maarufu zaidi. Bustani hiyo iligawanywa kuwa mabustani madogo manne kutokana na tofauti ya majira ya mchipuko, majira ya joto, majira ya mpukutiko na majira ya baridi, miundo ya mabustani hayo ilisanifiwa vizuri sana na kuonesha ustadi murua wa wajenzi ambao ulisifiwa sana na watalii. Bwana Mei Bing aliyewahi kuitembelea Bustani ya Familia ya Yan mara kwa mara alisema:

Naona Bustani ya Familia ya Yan ni tofauti na mabustani mengine ya Suzhou, bustani hiyo kabisa ni kama makazi. Katikati kuna nyumba, mabustani madogo yameizunguka nyumba hiyo, na mabustani hayo yalijengwa kutokana na umaalum tofauti ya majira manne, hivyo yanapendeza zaidi.

Mbali na Bustani ya Familia ya Yan, Bustani nyingine ya Hongyin Shanfang. Bustani hiyo ni kubwa sana, kwenye sehemu ya nyuma ya bustani hiyo kuna msonobari mmoja wenye urefu wa mita 10 na umri wa miaka zaidi ya 500, ambao unawavutia sana watalii. Bwana Mei Bing alisema, ukitembelea mabustani binafsi ya mji wa Mudu si kama tu unaweza kujionea ujenzi wa kifahari wa China, bali pia unaweza kupata raha katika mabustani yenye mandhari nzuri. Bwana Mei alisema:

Mabustani ya mji wa Mudu ni mahali pa kupumzika na kujistarehesha kwa watu, pia ni mahali pa marafiki kukutana na kufanya shughuli za utamaduni.

Kutembelea katika mji mdogo wa Mudu kunaweza kukaribia historia ya China, maendeleo ya mji huo ya hivi sasa yameonesha kuwa mji huo mdogo unafungua ukurasa mpya wa historia.

Idhaa ya kiswahili 2005-12-12