Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-12-12 16:21:22    
Mchonga picha za paka kwenye tunguri

cri

Tunguri ni kibuyu kidogo ambacho licha ya kuweza kutumiwa na waganga wa kienyeji kuwekea dawa zao, pia kinaweza kuwa kitu cha sanaa baada ya kuchorwa au kuchongwa na wasanii. Katika mji wa Lanzhou, kaskazini magharibi mwa China, kuchonga picha kwenye tunguri ni sanaa maarufu ya kienyeji, na tunguri maarufu ni zile zilizochongwa picha za paka na mzee Zhou Yisheng.

Soko la Huangmiao ni soko kubwa ambalo vitu vya sanaa na vya kale katika mji wa Lanzhou vinauzwa, wachongaji wengi wenyeji wako huko, wanachonga tunguri huku wakiziuza, watalii wanaotembelea mji wa Lanzhou huenda huko kununua vitu kwa ajili ya kumbukumbu zao. Mzee Zhou Yisheng ana duka dogo, lakini bei ya tunguri zake ni ghali kutokana na kazi yake ya sanaa kuwa nzuri.

Mzee Zhou Yisheng ana umri wa miaka 80, ni mrefu na mwenye afya, nguo yake nyeupe inamfanya aonekane mkakamvu. Alipoulizwa kwa nini bei ya tunguri yake ni ghali sana ikilinganishwa na tunguri nyingine, alijibu kwa kujivunia kwamba tunguri zake ni nzuri na hazipatikani mahali pengine kama zake, bei inalingana na ubora wa bidha yenyewe. Alisema,

"Sio najisifu, hapana! Michongo yangu haina dosari. Baada ya kuchonga huwa naichunguza kwa makini?zilizo nzuri naziuza na zile ambazo siridhiki nazo naziharibu, siziuzi na wala siwapi watu wengine."

Mzee huyo amekuwa akifanya kazi ya kuchonga picha za paka kwenye tunguri kwa miaka 60. Katika miaka ya 40 ya karne iliyopita mzee huyo alipokuwa na umri wa miaka 17 akiwa mtoto wa bosi wa duka moja, aliona wauza duka wakichora na kuchonga picha kwenye tunguri, alianza kujifunza kutoka kwao. Alichorachora na kuchongachonga hadi wauza duka wakaona ufundi wake umekuwa mzuri, wakampeleka kwa mwalimu wao ambaye alikuwa fundi wa kwanza wa kuchonga picha kwenye tunguri Bw. Li Wenzhai, kwa bahati nzuri Zhou Yisheng alikuwa mwanafunzi wake.

Zhou Yisheng alifundishwa na mwalimu wake kwa miaka kadhaa, kiwango chake cha ufundi kiliinuka sana. Picha zilizochongwa na mwalimu wake zilikuwa ni sanaa ya maandishi ambayo ilikuwa ikipambwa kwa picha, na Zhou Yisheng alipokuwa mwanafunzi alichonga zaidi picha za wasichana wa China ya kale, picha za wasichana kwenye tunguri zilitofautiana kwa sura na hisia. Baadaye mwalimu wa Zhou Yisheng alifariki, tokea hapo Zhou Yisheng alihuzunika kwa muda mrefu bila kutaka kufanya lolote hadi siku moja ambapo aliona paka mmoja aliyejikunyata kwenye kiti, alivutiwa sana jinsi paka huyo alivyokuwa amekaa kwa starehe, Zhou Yisheng mara alichukua karatasi na penseli akaanza kumchora paka alivyo, baadaye alichonga picha hiyo kwenye tunguri. Vivyo hivyo, Zhou Yisheng alishikwa na furaha ya kuchonga picha za paka na ilikuwa ni nadra kwake kuchonga picha nyingine. Mzee Zhou Yisheng alisema, si rahisi kuchonga picha za paka, kwani watu wote wanafahamu jinsi paka alivyo. Kwa hiyo ni lazima umchunguze kwa makini. Alisema,

"Baba yangu alipenda kufuga paka, na mimi vile vile. Baada ya mimi kuanza kuchonga picha za paka nilizidi kuchunguza. Nilikamata mjusi na panya mdogo nikamwachia paka acheze. Nilipiga picha jinsi paka alivyokuwa anawachezea. Kutokana na uchunguzi wangu wa kina na wa muda mrefu, picha zangu zimekuwa kama ni paka hai."

Ili kuchora picha ya paka aliyerukia windo lake, Zhou Yishen licha ya kuchunguza paka mchana, pia alimchunguza usiku na mara nyingi alichelewa kulala mpaka alfajiri. Kutokana na juhudi zake sasa tunguri za Zhou Yisheng zenye picha za paka zimekuwa maarufu. Tunguri zake zilizo kubwa ni kama pea na ndogo ni kama yai, kila tunguri ina michongo ya picha ya paka kama hai ambao baadhi wanarukia kipepeo, baadhi wanamchezea panya mdogo, baadhi wamelala chini ya maua na baadhi wanazunguka wakijaribu kukamata mikia yao wenyewe.

Mzee Zhou Yisheng ni makini kwenye kazi yake tokea anapochagua tunguri hadi anapofikiria picha. Alisema,

"Tunguri lazima iwe laini na isiwe na madoa, na umbo lake liwe zuri, kisha nitaipiga msasa na kuipiga polishi na kuisugulia kwa pua yangu."

Baada ya kazi zote hizo, tunguri inakuwa nyororo na kung'ara, yeye anaanza kufikiria picha yake na kuanza kuchonga. Picha za paka kwenye tunguri zinachongwa kwa mistari michache tu na kila mstari ni wa lazima. Tunguri zake zinanunuliwa sana hata zinahitaji kuagizwa mapema, na baadhi zinauzwa nchini Japan na kwenye nchi za Ulaya.

Kazi ya kuchonga picha za paka inamsaidia kiafya, ingawa amekuwa na miaka zaidi ya 80 lakini masikio yake yanasikia vizuri na macho yake makali, kwani kazi yake inamfurahisha kila siku. Lakini vilevile ana masikitiko, masikitiko yake ni kuwa mpaka sasa hajapata mtu anayefaa kuwa mrithi wa sanaa yake. Siku hizi vijana hawatulii na kukaa chini kuchonga tunguri kila siku. Anatumai serikali imfanyie matangazo ili vijana wathamini na kupenda sanaa hiyo, wajifunze sanaa hiyo kwa ari bila kulegalega.

Idhaa ya kiswahili 2005-12-12