Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-04-04 15:14:00    
Sanduku la barua 0404

cri
Msikilizaji wetu Kennedy Nyongesa Barasa wa sanduku la posta 1172 Bungoma Kenya ametuletea barua akisema, mwaka wa 2006 uliwadia kwa furaha kubwa, kwani klabu yake ya CRI salamu Club ilipokea barua na kalenda kutoka kwa Radio China kimataifa. Mwaka 2005 idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa imefanya juhudi kubwa katika kuendeleza kuchapa kazi kwa ajili ya kuboresha vipindi, kuchapisha jarida dogo la daraja la urafiki, kwenda nchi za Kenya na Tanzania kutafuta ushrikiano wa kuboresha usikivu wa matangazo kwa wasikilizaji.

Anasema ameambiwa kuwa Kituo cha FM 91.9 cha Radio China kimataifa kimeanzishwa huko Nairobi Kenya, kwa niaba ya wasikilizaji wa klabu yake anatoa pongezi kwetu. Anasema mapendekezo yake ni kuwa, idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa ishughulikie vitu vifuatavyo: ifahamishe, iburudishe na ielimishe. Klabu yake ikishirikiana na Mutanda Ayubu Shariff imetoa kanda za Radio wakizingatia hivyo vitu vitatu, kufahamisha kuhusu ugonjwa wa Ukimwi, afya na yale majanga ya kitaifa. Katika kuburdisha yeye amerekodi vipindi vyetu vilivyopeperushwa hewani vikiwemo vipindi vya salamu zenu, muziki na vingine vingi. Ilimbidi kuvirekodi kwani wengi wa klabu yake huwa kazini vipindi vinapoendelea ili wakirudi wavisikilize. Katika kuelimisha yeye na Mutanda Ayubu Sheriff hutembelea tovuti yetu na kwenye mtandao wa internet iliwapatia habari ya kuelimisha watu wasio na habari kuhusu kituo hiki.

Maoni yake ni kuwa hapo Kenya wasikilizaji huamini kuwa mcheza kwao hutunzwa, barua yetu ilimwarifu kuwa nguvu na uwezo wa idhaa yetu bado si mkubwa sana, lakini wanaamini kwamba hatutawasahau kikazi, kimawasiliano na kadhalika. Licha ya kukosa mashine ya kunasa vipindi vyetu kwa njia nzuri, mashabiki wetu humtaka arekodi vipindi vyetu akitumia radio yake ndogo, sasa imembidi atuombe tumsaidie apate mashine ili avinase vipindi vyetu na maoni, ili watu waone kuwa Radio China kimataifa ni idhaa ya kipekee na ya kimataifa kweli. Ana matumaini kuwa mwaka huu 2006 tutaendelea kumtumia kadi za salamu, barua mbalimbali, picha za viumbe mbalimbali.

Tunamshukuru kwa dhati msikilizaji wetu Kennedy Nyongesa Barasa kwa barua yake na mapendekezo yake, kweli juhudi zake na wenzake wa klabu yake za kusikiliza matangazo yetu zinatia moyo kweli, tutatoa ripoti kwa idara husika, kama ikiwezekana, tutawasaidia, lakini kwa kweli hatujui tutaweza kutimiza ahadi yetu lini. Ni matumaini yetu kuwa, wataendelea kusikiliza matangazo yetu na kutembelea tovuti yetu, na sisi tutaendelea kuchapa kazi ili kuwaridhisha wasikilizaji wetu.

Msikilizaji Vioellyne Aliviza pamoja na Fesbeth Nelima wa sanduku la posta 172 Bongoma Kenya wameanza barua zao kwa kututaka tupokee salamu zao kutoka huko Kenya, wana matumaini kuwa tunaendelea na kazi vizuri sana, na wanatushukuru kwa kazi zetu zote mwaka huu.

Wanasema hata hivyo wana swali ya kutuuliza ambayo wamemwuliza baba yao Ayub lakini hakuwapa jibu sahihi, wanataka tuwaeleze kama hapa China kuna watoto kama wao? Na kama wako kwa nini hawatumii salamu kwa idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa? Kwani mara kwa mara wao hapo Kenya wanajiuliza bila kupata jibu. Hawa wenzao wa China wanaishije? Au hawaelewi Kiswahili?

Kweli swali hili ni la kwanza kuulizwa na wasikilizaji wetu, kwenye kipindi chetu cha salamu zenu kwa kawaida ni wasikilizaji wanatuletea kadi za kusalimiana na sisi tunasoma, wasikilizaji wetu wanapenda kipindi hiki kinachoweza kuongeza mawasiliano kati yao. Nchini China bila shaka kuna watoto kama hao wawili Vioellyne Aliviza pamoja na Fesbeth Nelima, wengi wao hawaelewi Kiswahili, na wanasoma kwenye shule mbalimbali, labda hata wengi wao hawajapata habari kuhusu idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa, hii siyo ya ajabu, kwani China ni nchi kubwa, idadi ya watu wake ni wengi, siyo watu wengi ambao wanaweza kutujua, sisi watangazaji na watayarishaji wa idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa tunaweza kujulikana miongoni mwa wasikilizaji wetu, lakini wenzetu wengi wachina hawatujui, tunafanya kazi kwa ajili ya rafiki zetu walioko Afrika na sehemu nyingine duniani, wanaofahamu lugha ya Kiswahili. Hiyo ndio hali halisi.

Na wasikilizaji wetu hao wawili wanasema, kwa minajili hii ombi lao ni kuwahusu hao watoto kwa vipindi ambavyo vitawawezesha kuwafahamu zaidi. Isitoshe wanaambiwa na baba Ayub kuwa mtu akijaribu na ajibu maswali vilivyo ya chemsha bongo anaweza kufanikiwa tuzo ya kutembelea China kwa siku kadhaa, je, hii nafasi ni ya watu wazima pekee au pia wao watoto wanaweza kuwa washiriki kwenye chemsha bongo na kupewa tuzo kama hiyo?

Kuhusu swali hili, kweli ni vigumu kuwajibu, tunafurahia juhudi za watoto hao wawili, ingawa wanasema wao ni watoto, lakini maswali waliotoa na walivyoandika yameonesha kuwa wao ni watoto wenye bidii katika masomo yao. Tunaona kila msikilizaji anayefahamu Kiswahili anakaribishwa kushiriki mashindano ya chemsha bongo, lakini kwa kweli anatakiwa kusikiliza kwa makini na kujibu maswali kwa usahihi, na kutoa maoni yake kwa ufasaha, hivyo labda bado kuna pengo kati ya watoto na watu wazima, ambapo wasikilizaji wetu wanashiriki na kutoa majibu vizuri, lakini mshindi wa kwanza huwa ni mmoja, baadhi ya wakati, hata wasikilizaji wetu hawataweza kupata bahati, kwani Radio China kimataifa kila siku inatangaza kwa lugha 43, wasikilizaji wake ni wengi, na kila mwaka washindi wanaopewa tuzo ya kutembelea China ni wachache, lakini wakishikilia kusikiliza vipindi vyetu, siku hadi siku watapata bahati

Msikilizaji wetu Okongo Okeya wa sanduku la posta 381 Iganga Uganda ametuletea barua akisema, ana furaha nyingi kuwapongeza wafanyakazi wa Radio China kimataifa na wananchi wa Jamhuri ya watu wa China kwa umoja wao wa kitaifa na kimataifa. Katika kujenga jamii ya kimataifa katika hali ya undugu, umoja, ushirikiano, mshikamano, usawa, upendo, urafiki na kadhalika.

Anasema idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa ipokee heshima kubwa sana kutokana na sifa zake mbalimbali kutoka kwangu, kwani haina umbali wala ukabila, ni ya uaminifu, kujenga moyo wa wasikilizaji kuwa na ushujaa, wasikilizaji kutambulika kimataifa, na kila siku inatoa habari motomoto zenye kuaminika na kwa kusimulia hadithi za China ya kale.

Anasema Radio China kimataifa ni mwanga na tumaini la wasikilizaji katika sifa nyingi zaidi, yeye mwenyewe tangu alipoanza kusikiliza Radio China kimataifa alinufaika kwa usikilizaji mzuri na anasema ataisikiliza kwa maisha yake yote. Anaamini kuwa busara, umoja, hekima na akili, uadilifu, roho nzuri mbele ya walimwengu waliyo nayo wachina tangu zamani, ilitoka kwa mababu zao, hivi sasa walimwengu wanajifunza kutoka kwa wachina

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu Okongo Okeya kwa barua zake alizoandika, ni matumaini yetu kuwa ataendelea kusikiliza matangazo yetu na kutoa maoni na mapendekezo juu ya vipindi vyetu ili tuweze kukidhi vizuri mahitaji ya wasikilizaji wetu.

Idhaa ya kiswahili 2006-04-04