Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-08 10:11:39    
Barua 0808

cri
Msikilizaji wetu Stepheny M. Gekora wa S.L.P 71, Tarime, Mara, Tanzania ametuandikia barua akiuliza maswali matatu, akiomba kujua historia ya Radio China kimataifa kwa ufupi. Maswali hayo ni kama yafuatayo:

(1) Je, Radio China Kimataifa ilirusha matangazo yake ya kwanza hewani kwa lugha ya Kiswahili mwaka gani?

Radio China kimataifa ilirusha hewani matangazo yake ya Kiswahili tarehe 1 Septemba mwaka 1961, mpaka mwaka huu karibu miaka 45 itapita.

(2) Je, idhaa ya Kiswahili ilikuwa na watangazaji wangapi wakati huo?

Mwanzoni mwa kuanzishwa kwa matangazo ya Kiswahili ya Radio China kimataifa, idhaa ya Kiswahili iliwategemea zaidi watangazaji kutoka Zanzibar, Tanzania, ambapo watangazaji wapatao wanne hadi watano kutoka Zanzibar Tanzania walitusaidia kutangaza, baada ya miaka miwili watangazaji wengine wa China walianza kushiriki kwenye kazi ya kutangaza.

Msikilizaji wetu Bi. Celestine Mayogi wa S.L.P 2995, Kisii, Kenya katika barua yake kwanza anatoa pongezi kwa vipindi na matangazo ya idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa anayopokea kupitia Radio KBC Nairobi. Anasema Radio China Kimataifa ni ya kipekee nchini kote. Bi. Mayogi anasema yeye ni shabiki mpya wa Radio China Kimataifa, na anaitegea sikio radio hiyo kwa sababu inaelimisha, inaburudisha na inafundisha.

Alisema akimaliza masomo yake atajiunga na Radio China Kimataifa kila wakati kwa kutegea sikio matangazo ya Radio CRI kwa asilimia 100 lakini sasa anapokea asilimia 95 tu, vile vile anataka kutufamisha kuwa akimaliza masomo yake atajiunga na mafunzo ya utangazaji, ili wakati ujao kama ataweza awe mfanyakazi wa Radio China kimataifa, kwa hivyo anawashukuru wafanyakazi wa CRI kwa vipindi na matangazo yanayovutia na yanawafundisha wasikilizaji kila wakati wanapoyapokea.

Bi. Mayogi ni mwanafunzi katika shule ya upili ya Mokwerero huko Kisii, na yuko kidato cha tatu. Kazi yake ni kusoma na kutegea sikio matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa, anaona kuwa radio hii inatangaza ukweli na anatumai itaendelea kufanya hivyo hivyo. Mwishoni anatoa shukrani kwa wafanyakazi na watangazaji wote wa Radio China kimataifa, vile vile na kwa mashabiki wote wanaoitegea sikio radio hiyo.

Tunamshukuru sana Bi. Mayogi kwa barua yake, ni matumaini yetu kuwa, atafanya bidii kujifunza Kiswahili na utangazaji ili apate fursa ya kugombea nafasi ya mtangazaji kwenye radio yetu.

Msikilizaji wetu Ahobokile Mwaibabu wa S.L.P. 362, Tukuyu, Mbeya, Tanzania alimetuletea barua akitoa shukrani kwa uongozi mzima wa idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa kwa makini katika kuchapa kazi za kila siku, hali ambayo inafanya vipindi pamoja na radio kwa ujumla kuboreka zaidi kila kunapokucha. Hali hiyo nzuri ya uboreshaji wa vipindi imewafanya watu wengi wavutiwe na Radio China Kimataifa kuliko radio nyingine.

Anasema hata hivyo baadhi ya watu katika sehemu anayoishi wamekuwa wakimlalalmikia, kwani kwa kiwango kikubwa yeye ndiye aliyewashawishi watu wengi wasikilize Radio China Kimataifa na kuwafahamisha masafa ambapo radio hiyo inashika. Wanamlalamikia kwamba wanataka awaunganishe ili waweze kutoa maoni yao, kwani watu hao hawawezi kutumia kompyuta, ila wanaweza kutumia bahasha hizo zinazotumwa na Radio China Kimataifa. Lakini tatizo lake ni kwamba hajui namna ya kuwaunganisha.

Kwa hiyo Bw. Mwaibabu anaiomba Radio China Kimataifa itoe elimu kwa wasikilizaji kwa kusikiliza vipindi vya radio, au kutuma barua kwa baadhi ya wasikilizaji wanaotaka kujiunga na idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa, ili iweze kupata maoni kutoka kwa wasikilizaji wote.

Tunamshukuru sana Bwana Ahobokile Daimon kwa barua yake na juhudi zake za kuwasaidia wenzake kusikiliza matangazo yetu . Tunajua kutokana na kuwa matangazo yetu nchini Tanzania bado yanarushwa hewani kwenye masafa mafupi, si rahisi kuyapata kwa wasikilizaji wote walioko popote pale, tunafanya juhudi kubadilisha hali hiyo, tunaomba wasikilizaji wetu waweze kuvumilia kwa siku chache, tuna imani kuwa, kutokana na juhudi zetu na za idara husika za Tanzania bara na Zanzibar, muda si mrefu ujao usikivu wa matangazo yetu nchini Tanzania utaboreshwa.

Msikilizaji wetu Mutanda Ayub Shariff wa P. O. Box 172, Bungoma, Kenya katika barua yake anasema tangu idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa kwenye wimbi la FM izinduliwe, uchunguzi ambao amefanya kwa sasa katika sehemu kadhaa za Kenya zikiwemo Bungoma, Kakamega, Botere Mumias, Busia, Kitale, Webuye, Tongareni, Eldoret, Mt Elgou, Lugan na sehemu nyinginezo unaonesha kuwa wasikilizaji wanaitegea Radio China Kimataifa kwa hamu.

Anasema hata hivyo wengi wao wanasema au wanaomba Radio China Kimataifa ifanye juhudi, ili matangazo ya Kiswahili yaweze kuongezwa muda. Wakizingatia kuwa hii ndio lugha ya kitaifa na inaeleweka kwa watu mbalimbali nchini Kenya. Na kwa kuwa inasemwa, "mcheza kwao hutuzwa", ingawa wengine bado wana hamu ya kusoma habari kutoka kwenye tovuti za "Internet", lakini shida ni kuwa baadhi ya sehemu nchini Kenya hazina nguvu ya umeme, na kwa hiyo ni vigumu au ni ndoto kupata vifaa vya kuwawezesha kupata habari.

Bw. Shariff anaomba Radio China Kimataifa katika siku zijazo izingatie kuwa, kama kuna idara ya maktaba, habari zinaweza kutunzwa huko ili wasikilizaji waweze kuzisoma angalau kwenye maktaba moja au mbili nchini Kenya. Anasema kwa sasa Radio China Kimataifa imeingia kwenye roho za watu nchini Kenya, anatumai kuwa hayo yote yatatiliwa maanani, hata kutunzwa katika maktaba ya kuzunguka ambapo makala zinazochapishwa na ni ya muhimu sana, na maktaba ya kitaifa hapa Kenya, kwani karibu kila wilaya ina maktaba karibu. Isitoshe idhaa ya CRI pia ina nafasi bora ya kuanzisha jarida maalum la kuelimisha nchini Kenya, hii itasaidia kuinua uchumi na kutoa nafasi za kazi..

Katika barua yake Bw. Shariff pia ametoa maoni na mapendekezo mengi kuhusu vipindi vya afya, elimu, ushirikiano, uchumi na mengineyo kama vile mazingira. Kuhusu Afya anasema, kulingana na habari ambazo anazipata kutoka Radio China Kimataifa amejifunza mengi kuhusu afya, hasa jinsi vyakula aina mbalimbali vinavyoweza kujenga mwili, na hata vile vinavyoweza kupandwa, kupikwa na kuhifadhiwa. Kwa hivyo anatoa shukurani kwa watayarishaji wa vipindi hivyo, na sasa yeye na jamaa zake hawali ovyo bali wanazingatia mafunzo ya afya.

Na kuhusu elimu, kipindi hiki kwa ujumla kimeunganishwa na mambo ya afya, yaani kipindi cha elimu na afya. Wasikilizaji wengi wameweza kujifunza mengi, baadhi ya wachache wakiwemo, Bw. Xavier Telly Wambwa, Kenneta Nyongesa, Jendeka Goldah, Rispah Ombayo, Caroh Nyongesa, Christine Khaoyana wengineo wanasema elimu ambayo wanapata kutokana na kipindi cha elimu na afya ni ya kuwanjenga kimawazo na hata kupata ujuzi mwingi ambao utaendelea mpaka kwa vizazi vyao.

Na kuhusu ushirikiano, anasema idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa bila shaka imeleta maelewano mazuri kati ya China na Kenya. Vile vile kuna ushirikiano kati ya wahariri wa China na wahariri nchini Kenya. Kama vile siku chache zilizopita wahariri au waandishi wa Kenya Times na Standard walikutana na wale wa China, na hata wakapata fursa ya kujadiliana kuhusu mambo kadha wa kadha ya kimataifa, bila kusahau ushirikiano kati ya wasikilizaji na wahariri, wa idhaa yenyewe, na hata wenyewe kwa wenyewe. Na hii yote ni jambo la busara sana. Wakenya wanasema "Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu." Anaamini kuwa ushirikiano kati ya Kenya na China ukiendelea, basi uchumi wa nchi hizo mbili utaimarishwa.

Na kuhusu uchumi, anasema Radio China Kimataifa inaendelea kufanya juhudi ya kuleta mitambo yenye nguvu, kuendelea kuzuru Kenya na kutuma wahusika mara kwa mara, bila shaka kuna kuimarisha uchumi, hasa kwa usafiri na ujenzi. Kupitia matangazo ya Radio China Kimataifa kipindi hasa kipindi cha Afrika leo, kutakuwa na Wachina wengi ambao wataweza kwenda Kenya kutalii na vile vile kupitia kipindi cha Tazama China wakenya wengi wanaweza kufahamu kuhusu kutalii China, ambalo lingekuwa ni jambo gumu kama idhaa ya Kiswahili ya Radio China isingekuwepo.

Pia anasema Radio China kimataifa inahimiza utunzaji wa mazingira ya maisha, mara kwa mara baada ya habari vipindi vyote vinahusika sana na mambo ya kimaisha, kama vile mazingira yanayoweza kutunzwa, kuwalinda wanyama pori ambao wako hatarini kutoweka na upandaji wa miti. Yeye na wasikilizaji wengine wameamua kutunza mazingira kwa kupanda miti siku baada ya siku. Hata kwa siku chache tu wanaendelea kuunda chama cha kulinda au kutunza mazingira. Kazi imeshaanza na sasa unaoendelea ni upandaji wa matunda na mboga yakiwa ni pamoja na mapapai, maembe, maparachichi, pamoja na maua. Mpango ambao bado hawajabuni ni ufugaji wa nyuki na samaki.

Mwisho katika barua yake Bw. Shariff anatoa shukurani zake za dhati kwa watayarishaji wote wa vipindi, wahariri na watangazaji. Bila kumsahau Rais wa China Hu Jintao, mkuu wa Radio China kimataifa Wang Gengnian, na hata Rais wa Kenya na waziri Bw. Mutahi Kagwe, mkurugenzi Bw. John N. Waweni, meneja Bw. Wachira na hata Balozi wa China hapa Kenya Bw. Guo Chongli. Na pia anawasalimu Mama Chen pamoja na Bi. Du Shunfang, na kuwapa pongezi kutokana na kazi wanazofanya kwenye idhaa ya Kiswahili.

Tunamshukuru kwa dhati Bwana Mutanda Ayub Shariff kwa barua yake na mapendekezo yake mbalimbali ambayo yanatutia moyo, kutufurahisha na yote aliyosema tunaweza kuyazingatia kwa makini, ili kuboresha zaidi vipindi vyetu, ni matumaini yetu kuwa wasikilizaji wetu wengi wanaweza kutuletea barua na kutoa maoni na mapendekezo, tunatazamiwa kupanga upya vipindi vyetu vya FM huko Nairobi Kenya kuanzia mwezi Septemba, sasa bado tunafanya maandalizi.

Idhaa ya kiswahili 08-08