Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-10-10 16:59:51    
Barua 1008

cri

Msikilizaji wetu Ali Hamis Kimani wa shule ya Msingi Alaro, Othoro nchini Kenya ametuletea barua akitoa salamu kwa Radio China kimataifa, anasema yeye ni mzima wa afya na anaendelea kuchapa kazi huku akiitegea sikio idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa kila siku.

Dhumuni la barua yake ni kutujulisha kuwa amekuwa akipokea kadi za salamu, bahasha zilizolipiwa na picha mbalimbali za wanyama wa kichina pamoja na ukuta mkuu wa China. Anatoa shukrani sana kwa huduma hii ambayo ni adimu na nadra sana kuipata kutoka kwa radio nyingine za kimataifa.

Baada ya hapo Bw Kimani anapenda kutoa maoni na malalamiko yake juu ya shindano la chemsha bongo la mwaka jana 2005. Anasema alisikia washindi saba wakitangaza ambao wangepewa zawadi, lakini anauliza je ni zawadi gani hizo? au ni siri? Anauliza tena ni kwa nini washindi wamekuwa ni wachache huku Radio China Kimataifa inajua kuwa ina wasikilizaji wengi sana, na je kwa wasikilizaji waliopata majibu machache kama yeye hawatapata zawadi hata kidogo? Na kwa nini asitumiwe nakala ya majibu sahihi ya maswali ili aweze kujisahihisha?

Baada ya maswali na malalamiko yake, mwisho Bw Kimani anapendekeza kuwa zawadi zitolewe kwa wale wote waliopata angalau nusu ya maswali hayo ya chemsha bongo kama shukrani.

Tunamshukuru sana barua ya msikilizaji wetu Ali Hamis Kimani kwa barua yake yenye malalamiko kuhusu matokeo ya mashindano ya chemsha bongo. Kuhusu mashindano ya chemsha bongo, Radio China kimataifa inafuata kanuni zilizowekwa na uongozi wa Radio China. Radio China kimataifa kila siku inatangaza kwa lugha 43, miongoni mwake 38 ni lugha za kigeni, katika miaka ya hivi karibuni, kila mwaka inapokea barua milioni 200 hivi, ndiyo maana kila mwaka wasikilizaji wengi wanashiriki mashindano ya chemsha bongo, lakini wanaoweza kuchaguliwa kuwa washindi ni wachache tu, kwani Radio China kimataifa ni radio ya serikali kuu ya China, ambayo matumizi yake ya fedha yanatengwa na serikali kwenye bajeti ya taifa, kazi yake kuu ni kuandaa matangazo ya lugha za nchi mbalimbali kwenye mawimbi ya FM, masafa mafupi na masafa ya kati kwa kupitia radio za nchi mbalimbali, pamoja na kuandaa vipindi mbalimbali kwenye tovuti za lugha mbalimbali katika mtandao wa internet.

Kuandaa mashindano ya chemsha bongo ni moja ya kazi zake nyingi. Kila mwaka washindi 10 hivi wanaweza kuchaguliwa kuwa washindi maalum wa kupata fursa ya kutembelea China kwa wiki moja, washindi wengine waliopata nafasi za kwanza, pili na tatu wa mashindano ya chemsha bongo wanaweza kupata zawadi mbalimbali, zawadi hizo ndogo ndogo kama vile radio, vitambaa, fulana, mikoba na kadhalika ambazo tunawatumia wasikilizaji wetu washindi kuwafurahisha, na kila mara tunasoma barua za wasikilizaji wetu zinazoeleza kufurahia na kushukuru kwa zawadi hizo, wengi wao wanasema kupata ushindi siyo lengo, lengo ni kushiriki kwenye mashindano ya chemsha bongo, na kuzidi kuelewa hali mbalimbali ya China, na kuongeza urafiki kati ya Radio China Kimataifa na wasikilizaji wake.

Na mwaka 1997, msikilizaji wetu Kilulu Kulwa wa Shinyanga Tanzania aliwahi kupata ushindi maalum na kualikwa kuja China kwa matembezi, kuhusu habari hiyo tuliwahi kuwaelezea wasikilizaji wetu habari nyingi na kusoma barua alizotuletea Bwana Kilulu Kulwa mara kwa mara, baada ya kutembelea Beijing na sehemu nyingine nchini China kwa wiki moja, Bwana Kulwa ameongeza uelewa kuhusu China, mpaka sasa tunadumisha mawasiliano na urafiki kati yetu na Bwana Kulwa. Na kama tujuavyo kwamba, mwaka jana msikilizaji wetu Telly Wambwa wa Bongoma Kenya alipata ushindi na kualikwa kutembelea China, ambapo alifurahi sana na kueleza mengi juu ya matembezi yake kwa wasikilizaji wetu, yeye na wenzake wa klabu yao wanatutumia barua kila mara, hivi karibuni wamepata habari kuhusu Bwana Franz Manko Ngogo wa Tarime Tanzania na Bwana Mutanda Ayub Shariff wa Bongoma Kenya kupata ushindi tena wamefurahishwa sana, hivi sasa wana pilikapilika za kumsaidia Bwana Shariff kufanya shughuli husika. Tunawaelezea wasikilizaji wetu hayo yote ni kuwataka wasikilizaji wetu waongeze uelewa juu ya matangazo yetu na kazi zetu mbalimbali, ili tuzidishe maelewano na urafiki kati yetu.

Msikilizaji wetu Ramadhani Y. Kayungilo wa shule ya sekondari kahama, Shinyanga nchini Tanzania ametuletea barua akitumai kuwa wafanyakazi wote wa radio kimataifa ni wazima na tunaendelea vyema na kazi. Kwanza kabisa Bwana Kayungilo anaomba kama inawezekana barua hii imfikie pia mkuu wa Radio China Kimataifa Bwana Wang Gengnian, lengo la barua yake ni kuomba msaada kwani rafiki wa kweli ni yule akufaaye kwa dhiki.

Msikilizaji wetu huyu anasema msaada anaoomba sio wa gari, nyumba wala kazi bali anaomba kulipiwa karo ya shule ili aweze kuendelea na masomo yake. Hivi karibuni anatarajia kufanya mtihani wa taifa wa kidato cha pili, asipofanya mtihani huo basi hataweza kuendelea na kidato cha tatu. Anaendelea kusema kuwa anahitaji sana msaada huo kwa kuwa hivi sasa hana mtu wa kumlipia ada kwani akishindwa kuendelea na masomo atakuwa amepoteza malengo yake yote ya maisha. Mwisho anawatakia kazi njema wafanyakazi wote wa Radio China kimataifa.

Tunasoma barua hii ni kuwataka wasikilizaji wetu waelewe kuwa, tunaelewa wasikilizaji wetu fulanifulani wanakabiliwa na taabu mbalimbali na kuhitaji misaada, kweli tunataka kuwapa faraja. Lakini lazima waelewe kuwa Radio China kimataifa inafanya kazi ya kutangaza, gharama za matangazo ya radio zilitengwa na serikali kutokana na bajeti, haina utaratibu wa kuwa mfadhili wa marafiki zetu wenye taabu, tunaomba watuelewe. Asante sana.

Na Bw Mutanda Ayub Shariff wa S.L.B 172 Bungoma nchini Kenya katika barua yake aliyotutumia hivi karibuni anapenda kutuma salamu zake kwetu kwa wakati mwingine, anasema ingawa amekuwa mgonjwa kwa siku kadhaa lakini hajakosa kuisikiliza idhaa Kiswahili ya Radio China kimataifa.

Kwanza matangazo yanaendelea kutufikia kwa wakati mzuri, na kwa sasa wasikilizaji wameshaizoea. Hata hivyo wiki iliyopita kipindi cha salamu zenu, analalamika tulirudia matangazo yetu. Siku hizi tunajitahidi kukidhi mahitaji ya wasikilizaji wetu, lakini kwa kweli wakati fulani hatujui tufanye namna gani, kwani baadhi ya wasikilizaji wanapenda turudie matangazao ya salamu zenu na wanafurahishwa na utaratibu uliopo sasa, lakini wengine wanalalamika, kutokana na halisi halisi, labda bado hatujaweza kuwafurahisha kabisa wasikilizaji wote, lakini tutaweza kurekebisha. Ni matumaini yetu kuwa, wasikilizaji wengi zaidi watatuletea kadi za salamu zenu, ili tuweze kusoma zaidi.

Mbali na hayo Bwana Shariff pia anapenda kutoa shukrani kwa idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa na kwa wafanyakazi na viongozi wote kwa mipango mizuri waliyonayo. Hii ni mara ya kwanza kutuletea kipindi cha chemsha bongo na kutuhakikishia majibu mwaka huu. Hii imewatia washindani moyo na kama kawaida yupo mbioni kusubiri kwa mara ya tatu na ana hakika mola atamsaidia kuwa mshindi.

Mwisho anaomba wafuatao watumiwe maswali ili waweze kushiriki katika shindano la chemsha bongo mwakani. Nao ni kama wafuatao Elijah Bogonko Omariba, Janet Chebet, Dr Pius K.Masinde, Mary Mulongo, Knight Mutanda, Andrew Nyukuri, Josephine Mulongo, Jackline Zore, Emmah Mulongo na Einstain Vuyiya, wote hawa wanatunziwa barua na Bw Mutanda Ayub, S.L.B 172 Bungoma nchini Kenya.

Tunamshukuru sana kwa juhudi zake za kuwashirikisha watu kusikiliza matangazo ya Radio China kimataifa.

Na msikilizaji wetu Stephen Magoye Kumalija wa S.L.B 1067 Kahama, Shinyanga nchini Tanzania ametuletea barua akisema, Tarehe 26/04/2006 ilikuwa siku ya wananchi wa Tanzania na Zanzibar na Afrika kwa ujumla kuadhimisha siku ya Muungano wa kihistoria kati ya Tanganyika na Zanzibar, hasa baada ya muungano huo kutimiza miaka 42. Anasema bado kuna haja ya wazalendo hasa viongozi katika ngazi zote watumie busara na kurekebisha pale penye makosa ili kuimarisha muungano huo.

Pia anasema Rais wa Kwanza wa Tanzania hayati mwalimu Julius Kambarage Nyerere wakati wa uhai wake alipokuwa akihutubia mkutano maalum wa CCM mjini Dodoma miaka 15 iliyopita, alitoa maneno ya hekima sana, alisema Muungano ukifa kwa sababu za ukabila na udini basi hata Tanganyika itakufa kwa sababu hizo hizo..

Hivyo Bw Kumalija anautakia Muungano huu wa Tanganyika na Zanzibar uendelee vizazi hadi vizazi ili kudumisha amani, umoja, haki na upendo katika bara nzima la Afrika. Pia anaiombea jumuiya ya Afrika mashariki nayo iendelee kuwa na mshikamano wa pamoja katika kuleta maelewano na ushirikiano katika nyanja zote.

Mwisho, Bwana Kumalija anawatakia wafanyakazi wote wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa kila la kheri na mafanikio mema katika kazi hapo mjini Beijing.

Tunamshukuru sana Bwana Kumalija kwa barua yake ya kutuelezea hali ya nchini Tanzania asante sana. Ingawa tumechelewa, hapa tunafurahia kupongeza kwa dhati siku hiyo ya muungano wa Tanzania.

Idhaa ya kiswahili 2006-10-10