Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-12-12 15:11:11    
Barua1212

cri
 Makala 2-Kijiji cha Sanxingdui chenye mambo yasiyofahamika

Kabla ya kusoma makala hiyo, tunatoa maswali mawili. La kwanza, Sehemu ya Sanxingdui iliwahi kung'ara kwa miaka mingapi? La pili, miongoni mwa mabaki ya kale yaliyofukuliwa katika Sehemu ya Sanxingdui, vyombo vya aina gani vinaweza kuonesha ustadi murua wa usanii wa wakati ule? Je ni vyombo vya jade au vyombo vya shaba nyeusi?

Wakati Sehemu ya Sanxingdui ilipoitwa kuwa ni "Kijiji cha Nyota tatu", hakuna mtu aliyeweza kufikiri kuwa, mkulima Yan alipokuwa akilima mashamba angegundua mabaki ya Sehemu ya Sanxingdui, ugunduzi huo uliwashangaza watu, baadaye watafiti walifanya kazi za kufukua na kufanya utafiti kwa miongo kadhaa, wakathibitisha kuwa sehemu ya Mabaki ya Kijiji cha Sanxingdui ilikuwa sehemu ulipokuwa mji mkuu wa Dola la Shu la kale, ustaarabu wa dola hilo uliwahi kung'ara kwa miaka 2000, tunaweza kusema kuwa, Sehemu ya Sanxingdui iliwahi kung'ara kwa miaka 2000. Ugunduzi huo ulikamilisha historia ya utamaduni wa taifa la China, na kuonesha kuwa ustaarabu wa Sanxingdui ni sehemu moja ya utamaduni mama wa taifa la China kama ulivyo ustaarabu wa Mito Changjiang na Huanghe.

Kijiji cha Sanxing kiko mkoani Sichuan, kusini magharibi ya China, watalii wakitaka kwenda kwenye kijiji hicho wanatakiwa kupanda gari na kusafiri kwa saa moja hivi kutoka Chengdu, mji mkuu wa mkoa wa Sichuan. Hivi leo kijiji hicho kidogo kinavutia watu zaidi kutokana na ugunduzi wa mabaki ya kale miaka 75 iliyopita. Na miaka 10 iliyopita Jumba la makumbusho lilijengwa kwenye sehemu yaliyofukuliwa mabaki ya kale, jengo hilo limepewa jina la Sanxingdui.

Mwelezaji wa Jumba la makumbusho Bibi Qiu Xueqing alisema, kugunduliwa kwa mabaki ya kale kwenye latitudo 30 ya kaskazini kuna umuhimu mkubwa. Alisema:

Kwenye latitudo 30 ya kaskazini ya dunia pia kuna Mlima Jo Mo Lan Ma, mabaki ya ustarabu wa Maya, Bermuda Triangle, vyote hivyo vinaonekana kuwa bado havijafahamika kabisa kwa binadamu. Na Sehemu ya Sanxingdui ni mji wa kale pia ni dola la kale lililogunduliwa katika eneo la kusini magharibi ya China ambapo mabaki ya kale yaliyofukuliwa huko yanahusu mambo mengi mbalimbali yanayoonesha utamaduni unaong'ara kabisa katika zama za kale.

Katika utafiti wa mabaki ya kale watu wamegundua kuwa, miaka 3000 iliyopita mji huo wa kale uliojengwa kikamilifu uliachwa kwa ghafla, ambapo ustaarabu wa Sanxingdui uliokuwa unasitawi kwenye kiwango cha juu ulitokomezwa mara moja. Miaka mitano iliyopita, ugunduzi wa mabaki ya kale ya Sehemu ya Jinsha iliyoko kwenye kitongoji cha Mji wa Chengdu uliwapa watafiti mwangaza wa kuona kuwa, mabaki ya kale yaliyofukuliwa katika sehemu hizo mbili yana mitindo inayolingana kabisa. Hivyo wataalamu wengi wanaona kuwa mabaki ya Sehemu ya Jinsha iliyochelewa kujengwa kwa miaka 500 hadi 1000 kuliko Sehemu ya Sanxingdui ni sehemu inayoendeleza ustaarabu wa Sehemu ya Sanxingdui. Na wengine walisema, Sehemu ya Sanxingdui ilihamia kwenye Sehemu ya Jinsha. Kuhusu sababu za kuachwa kwa Mji wa Sanxingdui uliong'ara kwa miaka 2000, baadhi ya watafiti walisema ni kutokana na mafuriko, wengine walisema ni kutokana na vita, na wengine walisema ni kutokana na maambukizi ya magonjwa yaliyotokea wakati ule, lakini kumbukumbu za historia hazijagunduliwa, hivyo mpaka sasa hali halisi halijafahamika.

Kutokana na mabaki ya kale yaliyofukuliwa kwenye Sehemu ya Sanxingdui, watu wanaweza kutoa maswali mengi zaidi. Mwelekezaji wa watalii Bibi Qiu Xueqing alipojibu maswali ya watu alisema, vyombo vya shaba nyeusi vilivyofukuliwa kwenye Sehemu ya Sanxingdui vinawavuta watazamaji zaidi, kwani baadhi ya sanamu za watu zilizochongwa kwa shaba nyeusi zinaonekana kuwa ni tofauti kabisa na binadamu wa hivi leo, kwani sanamu hizo za watu ni zenye macho makubwa, pua inayochongoka, ambazo zinatofautiana kabisa na sura ya watu wa Bara la Asia. Bibi Qiu alijulisha hasa kinyago cha shaba nyeusi kilichooneshwa kwenye jumba hilo la makumbusho, inasemekana kuwa kinyago hicho ni sura halisi ya mfalme wa kwanza wa Dola la Shu. Bibi Qiu alisema:

Hiki ni kinyago cha shaba nyeusi kikubwa kabisa duniani, pia ni hazina ya taifa letu, kinyago hiki chenye maumbo ya ajabu, macho yake ya mche duara yanakodolewa nje, sehemu iliyo mbele ya mboni ni ya umbo la pembe nne, na masikio ni makubwa na yenye ncha, watalii wakiyatazama wote wanasema macho hayo ya kinyago yanayoweza kuona mbali na masikio yake yanaweza kusikia vilio na sauti kwa kufuata upepo.

Chombo cha shaba nyeusi cha mti mrefu kilichoneshwa kwenye jumba hilo kilimvutia sana Bwana Humbert Droz, hata mtalii huyo kutoka Ufaransa alitia shaka juu ya uchambuzi wake mwenyewe. Alisema:

Mabaki hayo ya kale ya China yaliwahi kuoneshwa nchini Ufaransa miaka kadhaa iliyopita. Ingawa anajua kuwa China ni nchi yenye historia ndefu tangu enzi na dahari, lakini alipotazama mabaki hayo ya kale bado anashangaa, hivyo akang'ang'ania mbele ya chombo hicho cha shaba nyeusi cha mti mrefu. Chombo hicho cha mti kinasifiwa kuwa ni maajabu duniani, ambacho urefu wake ni mita 3.6. Watu wa zama za kale wa China waliona kuwa miti ni mithili ya ulimwengu mzima, na jua, mwezi na nyota ni mithili ya matunda ya miti. Baada ya kufahamishwa na Bibi Qiu Xueqing huenda utapata uelewa fulani maalum. Bibi Qiu alisema:

Sanaa hiyo ya shaba nyeusi ni chombo cha shaba nyeusi kilichotengenezwa kwa shida kubwa kabisa na kuonesha ustadi mkubwa kabisa. Kwani umbo lake halionekani katika sehemu yoyote duniani, na ufundi wa kusubu chombo hicho pia haukuonekana katika sehemu nyingine duniani. Kazi ya kusubu chombo hicho kikubwa cha shaba nyeusi haiwezi kukamilishwa kwa mara moja, lazima kukalibu sehemu moja baada ya nyingine. Na miti minane ya shaba nyeusi iliyofukuliwa kwenye Sehemu ya Sanxingdui, ni miwili tu kati yao ilifufuliwa kikamilifu, na kufufuliwa kwa mti huo mrefu wafanyakazi walitumia miaka mitatu.

Hali halisi ni kwamba, mbali na ustadi wa kusubu miti hiyo ya shaba nyeusi, miti hiyo imeonesha zaidi ufahamu wa wachina wa zama za kale juu ya mbingu na ardhi. Kutokana na hayo mshauri wa Jumba la makumbusho la Sanxingdui Bwana Ao Tianzhao mwenye umri zaidi ya miaka 70, ambaye amefanya utafiti kuhusu utamaduni wa Sanxingdui kwa zaidi ya miaka 50 alitoa uchambuzi wake kutokana na vyombo vya shaba nyeusi vilivyofukuliwa katika Sehemu ya Sanxingdui alisema, madaraka ya kidini na madaraka ya kifalme yaliunganishwa pamoja, huu ni umaalum wa utawala wa zama za kale za wakati ule, na Sehemu ya Sanxingdui ilikuwa kiini cha kuhiji.

Vinyago vingi vya watu vya shaba nyeusi na vyombo vya shaba nyeusi vilivyotumiwa katika kutambika, dola la kale la Sanxingdui lilipitia dini asili, shughuli za kuabudu dunia ya maumbile, miungu na mababu, likaunganisha nchi na kuidhibiti kifikra na kijumuiya. Huenda katika dola la Shu la zama za kale, mara kwa mara zilifanyika shughuli nyingi kubwa za kutambika ili kuvuta watu wa madhehebu tofauti ya kidini walioko mbali na karibu kuhiji sehemu hiyo.

Tunaweza kusema kuwa, vyombo vya shaba nyeusi ni vyombo vyenye uwakilishi kabisa ndani ya mabaki ya kale yaliyofukuliwa katika Sehemu ya Sanxingdui, ambavyo vimeonesha vilivyo ustadi wa usanii wa zama za kale. Lakini mabaki mengine mengi ya kale yaliyofukuliwa kwenye Sehemu ya Sanxingdui kama vile pembe za ndovu pamoja na simba na makombe baharini mpaka sasa ni kama vitandawili kwa watafiti. Kwani kijografia, mkoani Sichuan kabisa siyo sehemu iliyowafaa ndovu kuishi. Na kutokana na maelezo ya Bibi Qiu Xueqing huenda watalii wanaweza kupata ufahamu fulani.

Wasomi fulani walisema, pembe za ndovu zilifika kwenye sehemu ya Sanxingdui kwa kupitia "Njia ya hariri ya kusini". Mbali na pembe za ndovu, vitu vya shaba na makombe karibu 5000 vilivyofukuliwa kwenye Sehemu ya Sanxingdui pia ni mabaki ya kale yaliyo muhimu ambayo yameonesha kuwa, katika zama za kale, Dola la Shu lilifanya biashara na nchi za nje hata hadi sehemu za Asia ya magharibi na Asia ya kusini, ustawi wa biashara ulionekana dhahiri kutokana mabaki ya kale yaliyofukuliwa kwenye sehemu hiyo.

Kwa kuwa utamaduni wa Sanxingdui umewafanya watu watie mashaka na kuwa na maswali mbalimbali, hivyo ingawa imekuwa miaka 10 tu tangu kuanzishwa kwa Jumba la makumbusho ya Sanxingdui, lakini jumba hilo limewavuta watalii wengi wasiohesabika, na mabaki ya kale yaliyofukuliwa kwenye Sehemu ya Sanxingdui pia yaliwahi kuoneshwa katika mabara manne duniani isipokuwa Bara la Afrika. Naibu mkurugenzi wa Jumba la makumbusho la Sanxingdui Bwana Zhang Jizhong alisema, mabaki ya kale yenye maumbo ya ajabu na murua yaliyofukuliwa kwenye Sehemu ya Sanxingdui pamoja na ustaarabu wa zama za kale usiofahamika una mvuto mkubwa sana kwa watalii kutoka nchi za nje. Bwana Zhang alisema:

Watalii wana hamu kubwa zaidi juu ya utamaduni wa kale usiofahamika wa Sanxingdui, utamaduni huo umesifiwa na nchi za nje kuwa ni kofia ya ufalme ya ustaarabu wa Mto Changjiang, na mabaki ya kale ya Sanxingdui ni vitu pekee ambavyo havijapatikana katika sehemu nyingine duniani, ambavyo vina mtindo maalum wa mashariki na utamaduni wa Dola la Shu la mkoa wa Sichuan, pia vina mvuto mkubwa sana kwa watalii wa nchi za nje.

Bibi Sirkka Korela kutoka Finland ni mmoja kati ya watalii kutoka nchi za nje, naye alishangazwa na maajabu ya Sanxingdui alisema:

Maonesho kwenye Jumba la makumbusho ya Sanxingdui yamepangiliwa vizuri na kuonesha umaalum wake kipekee, mabaki ya kale yaliyooneshwa kwenye jumba hilo hasa vinyago vinaonekana ni vitu vyenye hali ya miujiza, na miti ya shaba nyeusi pamoja na vinyago vya ndege wa ajabu, vinawafurahisha sana watu.

Hivi leo watu wengi wanatembelea jumba hilo la makumbusho lenye eneo la hekta 20 ambalo kuna mabaki mengi murua ya kale, hakika kila mmoja wao anaweza kupata ufahamu wake juu ya mabaki ya kale ya Sanxingdui.

Sasa tunarudia tena maswali yetu mawili: La kwanza, Sehemu ya Sanxingdui iliwahi kung'ara kwa miaka mingapi? La pili, miongoni mwa mabaki ya kale yaliyofukuliwa katika Sehemu ya Sanxingdui, ni vyombo vya aina gani vinavyoweza kuonesha ustadi murua wa usanii wa wakati ule? Je, ni vyombo vya jade au vyombo vya shaba nyeusi?

Idhaa ya kiswahili 2006-12-12