Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-01-01 17:47:37    
Kipindi maalum cha chemsha bongo kuhusu vivutio vya utalii vya "Mkoa wa Sichuan, maskani ya Panda" (4)

cri

Wasikilizaji wapendwa, katika makala ya tatu ya chemsha bongo kuhusu vivutio vya "Mkoa wa Sichuan, Maskani ya Panda" tuliwaelezea Mlima E mei na Mlima Leshan iliyojaa harufu nzito ya utamaduni wa dini ya Kibuddha, leo katika makala ya nne tutawaelezea sehemu za Mlima Qingcheng na Mfereji Dujiangyan ambazo ni mali ya urithi wa utamaduni duniani.

Kwanza tunatoa maswali mawili. Swali la kwanza, Je, ni Mlima gani unaweza kuchukuliwa kuwa ni sehemu moja ya chanzo cha dini ya Kidao, yaani dini ya kienyeji ya China? Swali la pili, Mfereji Dujiangyan ni mradi wa kuhifadhi maji mashambani uliojengwa zamani sana kuliko miradi mingine kama hiyo duniani, mifereji huo umekuwa na historia ya miaka mingapi? Tuna imani kuwa, baada ya kusikiliza makala ya nne mtapata majibu sahihi.

Watalii wakifunga safari kutoka Chengdu, mji mkuu wa Mkoa wa Sichuan kuelekea sehemu ya kaskazini magharibi ya mji huo, baada ya saa moja tu watafika Mlima Qingcheng. Wakiingia kwenye mlango wa mlima, na kupanda ngazi mara watahisi hali ya utulivu kabisa ya Mlima Qingcheng. Kando mbili za mlima huo kuna miti mingi inayositawi tangu enzi na dahari; maji ya kijito yanatiririka kwa kufuata bonde la mlima lenye vipengele vinavyopindapinda, wakati fulani maji yanatiririka kwa kasi, na wakati mwingine yanatiririka polepole, matone ya maji yakianguka kwenye majani yanametameta; na mlimani kuna ukungu unaoenea kila mahali, na katika sehemu ya juu zaidi mlimani ukungu ni mwingi zaidi.

Mlima Qingcheng ni sehemu moja muhimu ya chanzo cha Dini ya Kidao, yaani dini ya kienyeji ya China. Dini ya Kidao inazingatia zaidi "binadamu waishi katika hali ya kupatana na dunia ya kimaumbile". Tunadhani zaidi ya miaka 1800 iliyopita, mwanzilishi wa Dini ya Kidao Zhang Ling hakika alikuwa amevutiwa na mandhari nzuri ya Mlima Qingcheng na hali ya utulivu ya huko, ndipo alipoamua kuishi katika sehemu hiyo na akaanzisha dini ya kienyeji ya huko.

Baada ya kuanzishwa kwa Dini ya Kidao, dini hiyo ilikuwa dini yenye ushawishi mkubwa kabisa nchini China na hata sehemu ya Asia ya mashariki katika muda mrefu. Mwongozaji wa watalii Kang Yu alieleza kuwa, hivi sasa katika Mlima Qingcheng kuna watawa zaidi ya 100 ambao wanaishi maisha ya kufuata kwa makini sana nidhamu yao ya kidini. Lakini mwanzoni mwa kuanzishwa kwa Dini ya Kidao, hali haikuwa hivyo.

Hapo awali waumini wa dini ya Kidao waliweza kusoma somo lao la dini nyumbani kwao, hata waliruhusiwa kuoa na kupata watoto, pia waliruhusiwa kunywa pombe na kula chakula cha nyama, Dini ya Kidao ilizingatia zaidi kufuata maadili ya kidini kwa hiari. Lakini hivi sasa watawa wa dini hiyo wanapaswa kuishi katika mahekalu na kusoma somo la dini chini ya mafunzo ya walimu, ambapo hawaruhusiwi kunywa pombe na kula nyama, na hawaruhusiwi kuoa au kupata watoto.

Baada ya kusikiliza hadithi kuhusu Dini ya Kidao, watalii wanaweza kuangalia kwa makini majengo ya mahekalu ya Dini ya Kidao ili kuelewa vizuri zaidi nia halisi ya dini hiyo. Kwenye Mlima Qingcheng kuna mahekalu kumi kadhaa ya Dini ya Kidao yaliyohifadhiwa kikamilifu pamoja na mabaki mengi ya kale. Kwa kuwa Dini ya Kidao inatetea kuishi maisha ya kawaida katika dunia ya maumbile, hivyo majengo mengi ya mahekalu hayo yalijengwa ndani ya milima na kufunikwa na majani ya miti yanayositawi, majengo hayo yanaonekana kuungana na kupatana kabisa na milima na miti ya sehemu hiyo.

Miongoni mwa mahekalu mengi ya Dini ya Kidao, Hekalu la Shangqing liko kwenye sehemu iliyo karibu na kilele cha mlima. Katika Hekalu la Shangqing inaabudiwa sanamu ya Buddha Taishanglaojun, yaani Buddha mkuu Laozi wa Dini ya Kidao. Wakazi wa huko wanasema, waumini wa dini ya Kidao wanaofika kwenye Hekalu la Shangqing wakiabudu kwa dhati Buddha wao, huwa wanaweza kutimiza matumaini yao baada ya kuondoka, hivyo waumini wa dini wengi wanafika huko kuabudu Buddha.

Lakini kwa kweli watalii wengi hawajui kwamba wanaweza kupita njia nyingine fupi kupanda Mlima Qingcheng kutalii. Hapo kabla tuliwaelezea kuhusu sehemu ya mbele ya mlima huo, lakini sehemu ya nyuma ya Mlima Qingcheng kuna hali ya utulivu zaidi na mandhari ya asili zaidi, ingawa hakuna waumini wengi wa dini wanaofika huko kuabudu Buddha. Mji mdogo wa kale wa Taian ulioko huko ni sehemu inayowafaa watalii kupumzika njiani.

Watalii wakitembea kwenye njia nyembamba iliyo safi mjini Taian, wanaweza kuona maji ya kijito kando ya njia yanatiririka na kupita kila njia na kila familia mjini humo. Katika mji huo mdogo wa kale, watu wanaweza kutembea peku. Kando mbili za njia ya mawe, kuna nyumba za wakazi pia kuna maduka mbalimbali, na kila jengo lina kuta za rangi nyeupe na paa za vigae vya rangi nyeusi pamoja na milango yenye mapambo ya michongo. Katika kila duka, huning'inizwa nyama zilizokaushwa, na ndani ya makabati huwekwa mboga za zaidi ya aina kumi kadhaa ambazo watalii wengi hakika wanashindwa kujua majina yake, na katika kila duka kuna vyombo vikubwa vya vioo, ndani hujazwa pombe zilizotengenezwa na waendeshaji wa maduka hayo.

Watalii wanaweza kutafuta mkahawa mmoja wa chai na kukaa kwenye viti wakinywa chai ya majani, huku wanaangalia mawingu yanayoelea mlimani, ambapo wanaweza kujisikia raha mustarehe. Bwana Huang Weiqi ambaye anajifunza kuchora michoro ya milima na mito ya kichina tangu alipokuwa mtoto, safari hii alifika Mji wa kale wa Taian kutoka Mji mkubwa Guangzhou, ili kuishi maisha ya siku chache yaliyo ya utulivu katika mazingira ya asili. Alisema:

Mimi napenda kuchora picha za milima na mito, Mlima wa Qingcheng ni mahali pazuri pa kuwawezesha watu wahisi hali ya kuishi kwa kupatana na dunia ya maumbile wanayoitafuta waumini wa dini ya Kidao. Kama nikipata nafasi natarajia kuishi kwa mwezi mmoja kila mwaka katika mji huo mdogo wa kale.

Baada ya kutembelea Mlima Qingcheng, kwenye njia hiyo ya utalii pia kuna kivutio cha utalii yaani Mfereji wa Dujiangyan ulioko karibu na Mlima Qingcheng, ambao ni mradi wa kuhifadhi maji mashambani uliojengwa zamani kabisa kuliko mingine duniani. Mfereji wa Dujiangyan uko katikati ya sehemu ya mtiririko wa Mto Minjiang, ambao ulijengwa na ofisa wa serikali ya huko Bwana Li Bing akiwaongoza wakazi wa huko zaidi ya miaka 2000 iliyopita. Katika dunia nzima, miradi kadha wa kadha maarufu ya kuhifadhi maji mashambani, na mifereji iliyojengwa katika dola la kale la Babylon na Rome ya kale yote yaliachwa, ni mfereji wa Dujiangyan tu ambao mpaka sasa unatumika.

Inasemekana kuwa kabla ya kukamilishwa kwa ujenzi wa Mfereji wa Dujiangyan, kila ifikapo majira ya mchipuko na majira ya joto, mafuriko yalipotokea, mkondo kwenye mto ulikuwa na kasi sana, na ulisababisha mafuriko makubwa mara kwa mara. Usanifu kuhusu ujenzi wa Mfereji wa Dujiangyan ni kwamba Mto Mingjiang uligawanywa kuwa mito miwili, ili kupunguza mafuriko na pia kumwagia maji mashambani. Na Boma la Mdomo wa Samaki wa kugawanya mtiririko wa maji ni mradi muhimu kabisa ambao ulionesha ustadi murua kabisa wa usanifu wa ujenzi wa mfereji huo.

Akielekezwa na mwongozaji wa utalii, mwandishi wetu wa habari aliona kuwa, Boma la kugawanya mtiririko wa maji katikati ya Mto Mingjiag mithili ya samaki mkubwa anayelala katikati ya mto, akagawanya Mto Mingjiang kuwa mto wa ndani na mto wa nje, mto wa ndani unaweza kumwaga maji mashambani, na mto wa nje unatumiwa kuondoa mafuriko. Mwongozaji Zhou Tingjun akifahamisha alisema:

Zamani ofisa Li Bing alipowaongoza watu kuchimba mto, kwa makusudi walichimba kwa kina kirefu sana, na uso wa mto ni mwembamba, lakini kimo cha kitanda cha mto wa nje ni kifupi kuliko kile cha mto wa ndani, na uso wa mto ni mpana. Ndiyo maana katika majira ya ukame, maji yalipotiririka polepole mpaka kwenye mdomo wa samaki, mtiririko mkuu wa maji ulioelekea chini uliweza kufika kwenye mto wa ndani, ambapo kina cha mto ni kirefu, ambapo asilimia 60 ya maji yakaingia ndani ya mto wa ndani, na asilimia 40 ya maji yanaondolewa kutoka mto wa nje. Asilimia 60 ya maji yaliyoingia ndani ya mto wa ndani yaliweza kutumiwa kwa kumwagilia mashamba, hivyo katika majira ya ukame, sehemu ya chini ya mtiririko wa maji ya mto, haikuweza kuathiriwa na maafa ya ukame.

Lakini wakati mtiririko wa maji ulipokuwa mkubwa sana, mtiririko huo wa maji uliweza kuelekea kwenye mto wenye uso mpana, ambapo asilimia 60 ya maji yakaingia kwenye mto wa nje, na sehemu ya chini ya mtiririko wa maji ya mto haikuweza kutishiwa na mafuriko. Mtalii aliyetoka Marekani Bwana Ken Boyd alipotembelea Mfereji wa Dujiangyan alishangaa na kusifu sana usanifu murua wa ujenzi wa mfereji huo pamoja na uhodari walio nao watu wa China katika zama za kale. Alisema:

"Nashangaa mfereji huo ulijengwa zaidi ya miaka 2000 iliyopita, usanifu wake kweli ni murua sana, ulifika hadi kuweka kumwaga maji mashambani katika majira ya ukame, na kuwasaidia wakulima kulima mashamba; na katika majira ya masika, mfereji huo uliweza kuondoa mafuriko ili kuepusha maafa."

Watu wengine walisema, ni kuwepo kwa mfereji wa Dujiangyan Mkoani Sichuan, ndipo kumeufanya mkoa huo uwe na vivutio vingi vya watalii.

Wasikilizaji wapendwa, sasa tunarudia kutoa maswali mawili. Swali la kwanza, Je, ni Mlima gani unaweza kuchukuliwa kuwa ni sehemu moja ya chanzo cha dini ya Kidao, yaani dini ya kienyeji ya China? Swali la pili, Mfereji Dujiang ni mradi wa kuhifadhi maji mashambani uliojengwa zamani sana kuliko miradi mingine kama hiyo duniani, mifereji huo umekuwa na historia ya miaka mingapi? Matangazo ya makala hiyo ya nne yatarudiwa katika kipindi cha sanduku la barua cha wiki hii, na wiki ijayo tutawaletea makala ya 5 ya chemsha bongo kuhusu vivutio vya "Mkoa wa Sichuan, Maskani ya Panda", msikose kutusikiliza.