Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-01-01 19:18:38    
Mtu mashuhuri katika historia ya China, Lin Zexu

cri

Katika historia ya karibu ya China, Lin Zexu ni shujaa wa taifa la China anayefahamika kwa Wachina wengi, na hadithi yake ya kuteketeza kasumba ni moja ya makala zake zilizoko katika kitabu cha historia ya China katika shule za msingi na sekondari. Kwenye msingi wa mnara uliopo katika uwanja wa Tia An Men mjini Beijing zimechongwa sanamu za historia ya tukio hilo.

Bw. Lin Zexu alizaliwa mwaka 1785 katika mji wa Fuzhou mkoani Fujian. Maisha yake ya kiofisa yalikuwa ni kama kwa wasomi wengi katika jamii ya kimwinyi. Alipokuwa na umri wa miaka 20 alichaguliwa kuwa ofisa baada ya kufaulu mtihani wa kifalme, na tokea hapo alianza kushika nyadhifa za kazi mbalimbali katika maisha yake, aliwahi kuwa ofisa wa miradi ya hifadhi ya maji, kilimo, mahakama na kupambana na ufisadi kwa maofisa. Kutokana na juhudi zake alisifiwa sana na raia, na kupendwa na mfalme. Mwaka 1838, Lin Zexu aliagizwa na mfalme kwenda mkoani Guangdong, kusini mwa China, kufanya mapambano dhidi ya matumizi ya kasumba. Kutokana na mapambano hayo ameigawa historia ya kale na ya karibu ya China bila kukusudia.

Kabla ya kumwelezea Lin Zexu, kuna haja ya kueleza kwa ufupi hali ya China ilivyokuwa wakati huo. Baada ya China kuingia katika karne ya 19, jamii ya kimwinyi ilikuwa imefikia mwisho wake, utawala wa Enzi ya Qing ulikuwa ukiporomoka siku hadi siku, lakini kutokana na kujitenga na dunia, Enzi ya Qing iliendelea kujigamba kama ni nchi kubwa duniani bila kufahamu kwamba nchi za Ulaya zilikuwa zimepata maendeleo makubwa na kuanza kuinyemelea China ambayo ilikuwa na eneo kubwa, watu wengi na mali nyingi. Ili kupata faida kubwa na ya haraka, wafanyabiashara wa Ulaya waliingiza kasumba nyingi katika sehemu ya kusini ya China. Katika muda wa miaka 20 hivi, zaidi ya masanduku elfu 40 yaliingizwa nchini China kutoka elfu nne ya hapo mwanzo. Uvutaji bangi ulienea haraka miongoni mwa Wachina na uliathiri vibaya afya zao na ulisababisha ufisadi kwa maofisa. Fedha nyingi za China zilimimina mfukoni mwa wafanyabiashara wa nje, mapato ya serikali ya Enzi ya Qing yakapungua haraka. Bw. Lin Zexu alimwandikia barua mfalme akimtahadharisha kuwa kushamiri kwa biashara ya kasumba kunahusiana moja kwa moja na uhai wa taifa. Kwa hiyo mfalme alimwagiza aende kupambana na biashara ya kasumba.

Lin Zexu alianzisha mapambano mara baada ya kufika kwenye mji wa Guangzhou, mji mkuu wa mkoa wa Guangdong. Sambamba na kuimarisha ulinzi wa baharini na kuwakamata walanguzi wa kasumba, pia aliwaamuru wafanyabiashara wa nje wasalimishe kasumba zao. Kwenye onyo alilotoa kwa wafanyabiashara wa nchi za nje alisema, "Sitaondoka mpaka nimalize kabisa kasumba." Kutokana na msimamo imara na hatua kali, wafanyabiashara walilazimika kusalimisha kasumba masanduku zaidi ya elfu 20 ya kasumba yenye jumla ya tani 1,188. Lin Zexu alichoma moto kasumba hizo kwenye ufukwe wa Humen mjini Guangzhou, na moto uliwaka siku 23, kila siku watu maelfu kwa maelfu walikwenda kuangalia kwa furaha. Hilo lilikuwa ni "tukio la la Humen la kuteketeza kasumba".

Mapambano dhidi ya kasumba yalikasirisha serikali ya Uingereza. Mwaka 1840, jeshi la Uingereza lilizingira bahari ya mji wa Guangzhou, "Vita vya Kasumba" vikazuka. Kutokana na kupangwa na Lin Zexu askari na wakazi walikuwa wamejizatiti kupambana, kutokana na ulinzi mkali jeshi la majini la Uingereza liliacha kuushambulia mji wa Guangzhou bali lilielekea kaskazini na kuushambulia mji wa Tianjin, matokeo yakawa serikali dhaifu ya Enzi ya Qing ililazimika kusaini mkataba usio wa haki na Uingereza na kuigawia Uingereza ardhi ya China Kong Kong. Kutokana na askari wa Uingereza kuingia nchini China mfalme alimlaumu Lin Zexu na kumwondoa madarakani na kumwadhibu kuwa askari wa kawaida na kwenda mbali kwenye mpaka wa kaskazini magharibi. Lakini baadaye mfalme alikumbuka tena uaminifu wake, alimrudisha kutoka mpakani na kumpa tena wadhifa mkubwa. Lin Zexu hakuwa na neno, bali aliendelea na juhudi zake kama alivyokuwa zamani, na alipata mafanikio makubwa katika kazi zake. Lin Zexu alifariki mwaka 1850, mfalme alimpa sifa ya "mwaminifu wa taifa".

Tukio la kuteketeza kasumba lilionesha nia thabiti ya watu wa China kupambana na uvamizi wa nchi za nje, ni tukio la kung'ara katika historia ya mapambano dhidi ya mabeberu. Kutokana na mapambano yake, Lin Zexu amekuwa mfano wa uzalendo kwa taifa la China. Mchango wa Lin Zexu ni mkubwa lakini mkubwa zaidi ulikuwa ni moyo wake wa kufuatilia elimu iliyotangulia.

Katika zama hizo serikali ya Enzi ya Qing ilikataa mambo yote kutoka nje na kuwapumbaza wananchi. Kutokana na sababu hiyo taifa zima halikufahamu hali ya nchi za magharibi, hata mawaziri walikuwa hawajui nchi za Uingereza na Marekani zilikuwa ni nchi gani na ziko wapi. Lin Zexu alikuwa hivyo, lakini baada ya kufika mji wa Guangzhou kushughulika na mapambano dhidi ya kasumba mara akatambua tatizo hilo. Kwa haraka alijishughulisha na elimu kuhusu nchi za magharibi, aliwashirikisha watu kukusanya vitabu na magazeti ya nchi za nje na kuwaagiza Wachina waliorudi nchini kutoka nchi za nje na wanafunzi wa shule za misheni kutafsiri. Magazeti na vitabu vilivyotafsiriwa vilikuwa vya aina nyingi vikiwa ni pamoja na mambo ya uchumi, mambo ya kijeshi, historia, sheria na jiografia. Kitabu kilichokuwa na thamani kubwa zaidi kilikuwa ni kitabu kilichoandikwa na Mwingereza Bw. Hugh Murray kiitwacho "Kitabu Kamili cha Jiografia ya Dunia". Hiki ni kitabu cha kwanza kabisa cha jiografia na historia duniani.

Lin Zexu alikuwa na nia ya kuimarisha taifa la China na kukinga uvamizi wa nje kwa kujiendeleza kwa elimu iliyotangulia ya nchi za magharibi, fikra zake za kutaka kufungua mlango zilikuwa na athari kubwa kwa vizazi vya baadaye. Kutokana na athari yake kulikuwa na maofisa na wasomi wengi walioingiza sayansi na tenkolojia ya nchi za magharibi. Enzi ya Qing iliyokuwa nyuma ilianza kufungua pole pole mlango uliofungwa kabisa.