Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-04-04 16:02:17    
Shanghai yafanya juhudi kubwa kuandaa maonesho ya bidhaa duniani mwaka 2010

cri

Maonesho ya bidhaa duniani yanatarajiwa kufanyika mwaka 2010 huko Shanghai, mji wa mashariki mwa China. Hivi sasa ni miaka mitatu imebaki kabla ya kufunguliwa kwa maonesho hayo, shughuli mbalimbali za maandalizi ya maonesho hayo zinaendelea vizuri mjini Shanghai.

Mwishoni mwa mwaka 2002 Shanghai, mji mkubwa kabisa wa viwanda na biashara nchini China ulipata nafasi ya kuwa mwenyeji wa maonesho ya dunia ya mwaka 2010. Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa maonesho ya bidhaa duniani kufanyika katika nchi zinazoendelea.

Kwa mujibu wa mpango uliotangazwa na Shanghai, mwaka huu maandalizi ya maonesho ya dunia yameingia katika mwaka wa pili. Naibu mkuu wa idara ya uratibu ya maonesho ya bidhaa duniani ya Shanghai Bw. Zhou Hanmin alieleza kuwa, shughuli mbalimbali za maandalizi zinaendelea vizuri.

Mji wa Shanghai umejiwekea lengo la kushirikisha nchi na mashirika ya kimataifa 200 kwenye maonesho hayo ya bidhaa duniani. Kama lengo hilo litatimizwa, idadi hiyo itaweka rekodi mpya kwenye historia ya maonesho ya budhaa duniani. Hadi kufikia tarehe 27 Machi mwaka huu, nchi na mashirika ya kimataifa 125 zimeeleza kuwa zitashiriki kwenye maonesho ya bidhaa duniani ya Shanghai. Kuhusu vivutio vya Shanghai, naibu mkuu wa idara ya uratibu ya maonesho ya dunia ya Shanghai Bw. Zhou Hanmin alisema, China inawavutia wageni wengi siku hadi siku, pamoja na hayo maonesho ya bidhaa duniani ya Shanghai yana kauli mbiu inayowavutia watu wengi, nayo ni "miji inaleta maisha mazuri". Aidha, ofisa huyo alitaja sababu nyingine muhimu kuwa, maonesho ya dunia ya Shanghai yanafuatilia ipasavyo nchi zinazoendelea. Alisema "China imeanzisha mfuko wa dola za kimarekani milioni 100 wa kusaidia nchi zinazoendelea kushiriki kwenye maonesho ya bidhaa duniani ya Shanghai, nchi zinazoendelea zitakazonufaika na mfuko huo ni zile zilizo nyuma kimaendeleo na zile zenye mapato ya chini na ya wastani. Hivi sasa kuna nchi 114 duniani ambazo zimetimiza masharti hayo, na China itaziandalia maeneo ya kufanyia maonesho bila malipo."

Inakadiriwa kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu, idadi ya nchi na mashirika ya kimataifa yatakayoshiriki kwenye maonesho ya bidhaa duniani ya Shanghai itaongezeka na kufikia 170. Kwa upande wa idadi ya watalii, makadirio yanaonesha kuwa watu milioni 70 hivi watatembelea maonesho hayo ya bidhaa duniani yatakayofanyika mwaka 2010.

Hivi sasa pilikapilika nyingi za ujenzi zinaendelea kwenye bustani itakayofanyika maonesho hayo. Ujenzi wa zana mbalimbali za miundombinu, majumba na zana nyingine zinazohusika ulianza mwaka jana, na unatazamiwa kukamilika katika nusu ya pili ya mwaka 2009.

Kutokana na mpangilio, bustani hiyo yenye eneo la kilomita 5.28 za mraba ipo kwenye kando mbili za Mto Huangpu, kwa hiyo daraja moja lenye urefu wa mita 450 litajengwa.

Pamoja na hayo, wakazi wa familia zaidi ya elfu 18 pamoja na viwanda na kampuni zipatazo 300 zilizoko kwenye bustani hiyo zinapaswa kupangwa upya. Na shughuli za kuwahamisha wakazi hao ni muhimu sana katika maandalizi ya maonesho ya bidhaa duniani ya Shanghai. Kutokana na majadiliano, hivi sasa wakazi hao wamehamia kwenye nyumba mpya kubwa zaidi. Awali eneo la makazi kwa wastani wa kila familia ya huko lilikuwa zaidi ya mita 30 za mraba tu, lakini sasa eneo hilo limeongezeka kwa maradufu. Zaidi ya hayo serikali inawapa wakazi hao ruzuku za kununua nyumba mpya.

Mama Zhang Jinliu mwenye umri wa miaka 50 na familia yake yenye watu 7 walikuwa wanaishi kwenye nyumba yenye eneo la mita 78 za mraba. Safari hii walipata nyumba mbili zenye jumla ya eneo la mita 170 za mraba. Mama huyo alisema  "Kama tungenunua nyumba kwa kutumia akiba zetu bila msaada wa serikali, ingetuchukua miungo kadhaa. Lakini sasa kutokana na msaada wa serikali, nimeanza kuishi kwenye mtaa wa makazi ya kisasa."

Mbali na wakazi wa huko, viwanda mbalimbali pia vilihamishwa kwa ajili ya ujenzi wa bustani ya maonesho ya bidhaa duniani. Kiwanda cha chuma na chuma cha pua cha Pudong kilichoanzishwa mwaka 1913 ni kiwanda kikubwa kabisa miongoni mwa viwanda vilivyohamishwa, kilikuwa na eneo la zaidi ya hekta 200. Kutokana na kutakiwa kuhama, kiwanda hicho kilipaswa kusimamisha uzalishaji na hivyo kupata hasara. Hata hivyo meneja wa kiwanda hicho anayeshughulikia uhamiaji Bw. Chen Xiangting alisema wafanyakazi wengi wa kiwanda hicho wanaona kuwa kuhama huko kutaleta fursa nyingi za maendeleo. Katika kiwanda kipya kinachojengwa kwenye sehemu ya kaskazini ya mji wa Shanghai, wafanyakazi watatumia teknolojia na zana mpya, ambazo zitarahisisha uzalishaji, kupunguza matumizi na uchafuzi.

Bw. Chen Xiangting alisema  "Kwa mtizamo wa upeo wa mbali, kuhama huko kutaleta nafasi za maendeleo kwa kiwanda na wafanyakazi. Ukubwa wa eneo la kiwanda kipya ni mara moja zaidi kuliko ule wa zamani, na kitatumia teknolojia mpya za kisasa, ambazo zitaleta ufanisi wa uzalishaji na kupunguza uchafuzi. Aidha ubora wa bidhaa zetu utainuka na hivyo kuongeza thamani zake."

Hivi sasa asilimia 95 ya viwanda vimehamishwa kutoka kwenye eneo la bustani ya maonsho ya bidhaa duniani. Meya mdogo wa mji wa Shanghai Bw. Yang Xiong alieleza kuridhika na maandalizi ya maonesho hayo, alisema "Maandalizi ya maonsho ya bidhaa duniani yanaendelea bila matatizo, hii inatokana na ufuatiliaji wa serikali kuu ya China na jumuiya ya kimataifa pamoja na uungaji mkono wa wananchi wakiwemo wakazi wa mji wa Shanghai."

Hivi sasa ni miaka mitatu imebaki kabla ya kufanyika kwa maonsho ya bidhaa duniani ya Shanghai. Karibuni Shanghai na kutembelea maonesho hayo makubwa mwaka 2010.

Idhaa ya kiswahili 2007-04-04