Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-10-08 14:52:51    
Moja ya mbinu 36: Kunufaika kutokana na vurugu

cri

Mbinu ya "Kunufaika kutokana na vurugu" inatokana na uzoefu wa maisha ya kila siku, kwamba watu wanapokamata samaki ndani ya mto wenye maji machache huwa wanakoroga maji na kuyachafua, hivyo inakuwa ni rahisi kuwakamata samaki. Mbinu ya "Kunufaika kutokana na vurugu" inayotumika katika vita, ina maana ya kwamba wakati maadui wanapokuwa katika hali ya vurugu, utumie mbinu hiyo na kupata ushindi. Ufuatao ni mfano wa matumizi ya mbinu hiyo katika vita vya zamani nchini China.

Mwanzoni mwa karne ya nane kilikuwa ni kipindi cha ustawi mkubwa katika Enzi ya Tang, mji mkuu wa enzi hiyo, Chang An (mji wa Xi'an wa leo) ulikuwa ni mji uliostawi sana duniani, lakini wakati huo kabila la Waqidan lililopo kaskazini mashariki mwa China lilifanya uasi na mara kwa mara kufanya mashambulizi dhidi ya jeshi la Enzi ya Tang. Mfalme wa enzi hiyo alimtuma jemadari Zhang Shougui kwenda kwenye mji uliokuwa muhimu kwa vita Youzhou kutuliza uasi. Mji wa Youzhou ndio mji wa Beijing wa sasa, kutokana na mahali uliopo kijiografia, mabwana wa vita walikuwa wakitamani sana mji huo, na wakati huo mji huo ulikuwa ni kama ngao ya kuzuia mashambulizi ya jeshi la kabila la Waqidan.

Jemadari wa jeshi la kabila la Waqidan aliyeitwa Ke Tugan aliongoza askari wake kuushambulia mji wa Youzhou mara kadhaa, lakini hakufanikiwa, baadaye alituma mjumbe wake kwenda kwenye mji huo ili kupeleleza hali ya jeshi linalolinda mji huo kwa kisingizio cha kukubali kutawaliwa na mfalme wa Enzi ya Tang. Jemadari wa Enzi ya Tang aliyeitwa Zhang Shougui alijidai kama hafahamu hila ya mjumbe huyo, alimkaribisha kwa heshima. Siku ya pili pia alituma mjumbe wake kwenda kwenye kambi za askari wa Qidan na kuwatuliza moyo, lakini kwa kweli alikuwa na lengo la kufahamu hali ya undani ya jeshi la Qidan.

Mjumbe wa Enzi ya Tang alikaribishwa vizuri katika kambi za askari wa Qidan, kwenye tafrija mjumbe huyo aligundua kwamba makamanda wa askari wa Qidan walikuwa na maoni tofauti kuhusu utawala wa mfalme wa Enzi ya Tang. Jemadari Ke Tugan alishikilia kufanya uasi na jemadari mwingine Li Guozhe alimpinga na hata alimwambia mjumbe wa Enzi ya Tang kwamba watu wa kabila la Waqidan pia wanapinga vita. Kutokana na hali hiyo mjumbe wa Enzi ya Tang alimshawishi Li Guozhe aachane na jemadari mwenzake Ke Tugan na kumhakikishia kwamba atapewa wadhifa muhimu na mfalme wake wa Enzi ya Tang. Li Guozhe alishawishika na kukubali kumwua Ke Tugan akipata nafasi. Mjumbe huyo alirudi mjini Youzhou na kutoa ripoti kwa jemadari Zhang Shougui hali ilivyokuwa ndani ya jeshi la Qidan.

Baadaye, kweli jemadari Li Guozhe aliongoza askari wake kufanya mashambulizi ya ghafla dhidi ya kambi ya askari wa jemadari mwenzake Ke Tugan. Kutokana na kutokuwa na maandalizi jemadari Li Guozhe aliuawa, hali ya kambi ya askari wa Qidan ikawa imevurugika vibaya. Jemadari aliyelinda mji wa Youzhou alikuwa amejiandaa, kwa haraka aliwaongoza askari wake kuingia kwenye kambi za maadui, wakati huo askari wa majemadari wawili walikuwa wakipigana na kuuana, hali ilikuwa ya vurugu kubwa. Jemadari Zhang Shougui alipata ushindi katika hali ya vurugu na aliwakamata makamanda wengi wakiwa hai. Tokea hapo uasi ulitulizwa kabisa.

Mfano wa matumizi ya mbinu hiyo unadhihirisha kuwa, Jeshi la Enzi ya Tang lilipata ushindi kutokana na hali ya maoni tofauti kati ya makamanda, raia wa kawaida kupinga vita, na nguvu za aina tofauti zilipambana.

Kwa mujibu wa maneno, mbinu hiyo ya "kunufaika kutokana na vurugu" ina maana mbaya na inafanana na mbinu ya "Kupora mali wakati wa ajali ya moto". Katika jamii ya hivi leo mbinu hiyo ya "kunufaika kutokana na vurugu" pia inatumika sana katika ushindani wa biashara, baadhi ya wafanyabiashara wananufaika kwa kutumia tabia ya wateja kufuata watu walio wengi au ambao hawana uhakika kuhusu hali ya soko itakavyokuwa baadaye, Kwa upande mwingine, ili kujikinga na mbinu hiyo na kujiletea hasara, lazima uwe na busara na kuwa na uwezo wa kutafakari hali ya mambo bila ya kushawishiwa na kubabaishwa na wengine ili "samaki" wako wasikamatwe katika hali ya maji yaliyovurugika.

Idhaa ya kiswahili 2007-10-08