Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-01-01 18:54:39    
Maendeleo ya uchumi wa China yasifiwa na dunia

cri

Katika mwaka 2007 uchumi wa China umepata mafanikio ya kufurahisha. Kuanzia mwezi Januari hadi mwezi Septemba mwaka 2007 uchumi wa China ulipata maendeleo ya haraka na yenye utulivu, mapato ya wakazi wa mijini na vijijini yaliongezeka kwa kiasi kikubwa, kazi ya kubana matumizi ya nishati na kupunguza utoaji na maji taka na hewa chafu ilipata maendeleo mapya. Mafanikio hayo yote yanafuatiliwa na jumuiya ya kimataifa.

Kuanzia mwezi Januari hadi mwezi Septemba mwaka 2007 thamani ya uzalishaji nchini China ilizidi yuan trilioni 16, ambayo iliongezeka kwa asilimia 11.5 kuliko mwaka 2006 wakati kama huu. Wataalamu walikadiria kuwa, mwaka 2007 ongezeko la uchumi wa China litafikia zaidi ya asilimia 11. Naibu kiongozi wa ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini China Bw. Franz Jessen alilisifu sana ongezeko kubwa la uchumi wa China, alisema,

"Mwaka 2000 serikali ya China iliweka lengo la kuongezeka kwa pato la taifa kwa mara moja katika miaka 10 ijayo. Naamini kuwa serikali ya China itatimiza malengo mbalimbali yaliyowekwa kwenye mpango wa 11 wa miaka mitano."

Mwaka 2007 matumizi ya wananchi wa China yaliongezeka kwa haraka, na yalitoa mchango mkubwa kwa asilimia 37 ya ongezeko la uchumi katika miezi tisa ya mwanzo. Mauzo ya bidhaa katika nchi za nje na uwekezaji ambazo ni nguvu nyingine mbili za kusukuma mbele ongezeko la uchumi wa China zinafanya kazi ndogo kuliko matumizi ya wakazi wa China. Katika miezi tisa ya mwanzo, mauzo ya bidhaa katika nchi za nje yaliongezeka kwa asilimia 0.6 kuliko mwaka 2006 wakati kama huu, na uwekezaji ulipungua kidogo.

Bw. Michael Jett ni meneja mkuu wa kampuni ya BBA ya Uingereza, ambayo ni kampuni kubwa zaidi ya vitambaa visivyo vya kufumwa duniani. Anaona kuwa ongezeko la mapato ya wakazi na maendeleo ya huduma za jamii ni sababu muhimu ya kuhimiza manunuzi nchini China, alisema,

"Ongezeko la ununuzi nchini China linamaanisha kuwa kiwango cha maisha na mapato ya wananchi wa China yanainuliwa."

Kwa mujibu wa takwimu, katika miezi tisa ya mwanzo ya mwaka 2007, wastani wa mapato ya wakazi wa mijini na vijijini kwa mtu uliongezeka kwa asilimia 13.2 na asilimia 14.8.

Aidha, watu wengi zaidi wameshiriki kwenye mfumo wa huduma za jamii, na idadi ya watu wanaoshiriki kwenye bima za uzeeni, matibabu na ajira pia imeongezeka. Hali hiyo inatokana na serikali kuu ya China kutenga fedha nyingi zaidi kwa huduma za jamii. Mwakilishi mkuu wa ofisi ya shirika la fedha duniani nchini China Bw. Vivek Arora aliisifu hali hiyo, alisema,

"Nafikiri mwaka huu jambo moja la kufurahisha ni kuwa serikali ya China imetenga fedha nyingi zaidi kwa shughuli kadhaa za jamii, zikiwemo elimu na matibabu. Hatua hizo zinasaidia kuinua kiwango cha maisha ya wananchi, pia zinasaidia maendeleo ya uchumi yenye uwiano."

Maendeleo ya uchumi wa China hayakupatikana kwa urahisi. Mwaka 2006 matatizo kadhaa yalitokea, yakiwemo ongezeko kubwa kupita kiasi la uwekezaji, utoaji mkubwa kupita kiasi wa mikopo na urari mkubwa kupita kiasi wa biashara ya nje, na mwaka 2007 masuala kadhaa mapya yametokea tena, kama vile kupanda kwa bei za bidhaa. Ili kuhakikisha maendeleo ya uchumi kwa utulivu, serikali ya China ilichukua hatua mbalimbali za usimamizi kwa ujumla, na kutumia zaidi sera za fedha. Hadi hivi sasa benki kuu ya China imeongeza riba kwa mara tano, kupandisha kiwango cha akiba zinazotakiwa kutoka kwa mabenki kwa mara kumi. Hatua hizo za kifedha ambazo zilitumiwa kwa mara chache zamani, zimekuwa hatua za kawaida za marekebisho na udhibiti wa uchumi kwa ujumla nchini China. Kutokana na udhibiti wa uchumi kwa sera za fedha, ongezeko la uchumi wa China lilipungua na kufikia asilimia 11.5 ya kipindi kuanzia mwezi Julai hadi mwezi Septemba kutoka asilimia 11.9 kuanzia mwezi Aprili hadi mwezi Juni.

Licha ya sera za fedha, kazi ya kubana matumizi ya nishati na kupunguza utoaji wa hewa chafu na maji taka pia imekuwa njia nyingine muhimu ya marekebisho na udhibiti wa uchumi. Mwaka huu China ilifuta marudisho ya ushuru wa bidhaa za aina zaidi ya 500 ambazo zinatumia nishati nyingi na kusababisha uchafuzi mkubwa, na benki zilianza kupunguza au kusimamisha mikopo kwa makampuni ambayo yanatumia nishati nyingi na kusababisha uchafuzi mkubwa.

Habari kutoka idara husika za China zinaonesha kuwa, katika miezi tisa ya mwanzo ya mwaka 2007, matumizi ya nishati kwa kupata kiasi fulani cha pato la taifa yalipungua kwa asilimia 3 kuliko mwaka 2006 wakati kama huu. Utoaji wa sulfur dioxide na mahitaji ya kikemikali ya Oxygen vilipungua kwa mara ya kwanza. Kwenye mkutano wa mabadiliko ya hali ya hewa ya Umoja wa Mataifa, mwenyekiti wa kamati inayoshughulikia mabadiliko ya hali ya hewa ya Umoja wa Mataifa Bw. Rajendra Pachauri aliyasifu mafanikio ya China, alisema,

"China inafanya juhudi katika matumizi ya nishati endelevu zikiwemo nishati za mwanga wa jua na nguvu za upepo. China pia inafanya juhudi kuongeza ufanisi wa matumizi ya nishati, na kudhibiti utoaji wa hewa zinazosababisha kuongezeka kwa joto duniani."

Wanauchumi wa nchi za nje wanaona kuwa, ongezeko kubwa la uchumi wa China limetoa mchango mkubwa kwa dunia. Ripoti ya mustakabali wa uchumi wa dunia iliyotolewa na shirika la fedha duniani linaonesha kuwa, China itakuwa nchi iliyotoa mchango mkubwa zaidi kwa ongezeko la uchumi duniani kuliko Marekani katika mwaka 2007, ambayo ilitoa robo ya mchango kwa ongezeko la uchumi duniani. Mkurugenzi wa idara ya utafiti ya shirika la fedha duniani Bw. Simon Johnson alisema,

"Mwaka huu tulihesabu kwa mujibu wa uwezo wa ununuzi, China itakuwa nchi iliyotoa mchango mkubwa zaidi kwa ongezeko la uchumi duniani. Hii ni mara ya kwanza kupata matokeo hayo kwenye takwimu za shirika letu."