Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-01-14 17:14:47    
Kusikiliza muziki wa kale wa China kwenye jumba la makumbusho

cri

Mjini Zhengzhou ambao ni mji mkuu wa mkoa wa Henan ulioko sehemu ya kati ya China, kuna jumba moja maalumu la makumbusho, watu wanaotembelea jumba hilo la makumbusho wanaweza kupata nafasi ya kuona maonesho ya muziki uliopigwa kwa ala za muziki za miaka elfu kadhaa iliyopita..

Muziki mnaosikia hivi sasa ni muziki wa kupokea wageni uliopigwa miaka zaidi ya elfu tatu iliyopita. Jumba la makumbusho la mkoa wa Henan, ambalo lina eneo la mita za mraba zaidi ya laki moja, ni jumba la makumbusho linaloonesha mambo ya historia na sanaa. Jumba hilo la makumbusho lilianza kutembelewa na watu kuanzia mwaka 1998, kila mwaka linapokea wageni kiasi cha laki tatu wa nchini na kutoka nchi za nje. Vitu vya kiutamaduni vinavyohifadhiwa kwenye jumba la makumbusho la Henan vinafikia zaidi la laki 1.3 vikichukua sehemu ya moja kwa nane ya jumla ya idadi ya vitu vya kale vinavyohifadhiwa katika majumba mbalimbali ya makumbusho ya China. Baadhi ya ala za muziki za kale zilizofukuliwa kutoka ardhini zilitengenezwa kwa vifaa vya kipekee na zenye maumbo na sauti nzuri, ala hizo za muziki zinaonesha kiwango cha juu cha muziki wa zamani za kale za nchini China. Kwa mfano, filimbi iliyotengenezwa kwa mfupa wa ndege, ambayo ni ala ya muziki yenye umbo la bomba jembamba iliyogunduliwa zamani zaidi nchini China. Mwongozaji wa bendi ya ala za muziki za kale ya China Bibi Wang Xue alisema,

"Filimbi hiyo iliyotengenezwa kwa mfupa miaka 8,000 iliyopita, inaweza kutoa sauti za aina saba."

Seti ya kengele ni mfumo wenye Kengele nyingi zaidi katika bendi za muziki za kale, kengele zilizoko katika mfumo huo zilitengenezwa kwa kuiga kengele za kale zilizofukuliwa mkoani Henan. Kuna jumla ya kengele hizo za kale 26, ambazo zilitengenezwa miaka zaidi ya 2,500 iliyopita. Kengele hizo zikiwa ni ala za muziki zilizokuwa zinatumika kwa ajili ya wafalme wa zamani wa China, zilitengenezwa kwa ufundi mkubwa, na zina sauti za aina nyingi. Hebu tusikilize kidogo sauti za kengele hizo:

Baadhi ya ala za muziki zilizotumika katika bendi za kale za nchini China zilitengenezwa zaidi ya miaka 8,000 iliyopita, na zile za karibuni zilitengenezwa zaidi ya miaka 2,300 iliyopita. Muziki wa kale wa miaka zaidi ya elfu kadhaa iliyopita ni mzuri, lakini kupiga ala hizo za muziki si kazi rahisi. Bibi Chang Yi ni mpiga muziki katika bendi ya muziki wa kale ya Huaxia, ala ya muziki anayopiga inaitwa "Qing", ambayo ni seti moja ya vipande vyembamba vya aina ya mawe, alituambia kuwa kitu muhimu zaidi katika kupiga ala za muziki za kale ni kuwa na ustadi wa kupiga ala hizo. Alisema,

"Kiasi cha nguvu inayotumika katika kupiga vipande hivyo vya mawe kinahusiana na uzuri wa muziki, mpiga ala za muziki akipiga kwa nguvu kubwa au ndogo zaidi, sauti inayotoka haiwi nzuri. Kitu kingine muhimu ni sehemu inayopigwa kwenye kipande cha jiwe, kila kipande cha jiwe kina sehemu yake ya kupigwa, sio kila sehemu inayoweza kupigwa."

Hapo hapo muziki ulikuwa unapigwa. Mpigaji muziki huku alipiga ala ya muziki ya asili ya China inayofanana na kinanda huku akiimba:

Wakati wa kufanya maonesho, wanamuziki wote huvaa mavazi ya watu wa kale. Mpangilio wa muziki na maonesho ya ala za muziki vinalingana hali iliyosimuliwa katika data za uchunguzi kuhusu mambo na vitu vya kale.

Mazingira hayo yanafanya watalii waliopo pale kusahau enzi waliyoko sasa. Mtafiti wa jumba la makumbusho la mkoa wa Henan Bibi Li Hong alisema, bendi ya ala za muziki za kale ya Huaxia imefufua mabaki ya utamaduni wa muziki ya kale na kuongeza njia moja ya kuwaonesha watu ala za muziki za kale. Alisema,

"Tunataka wale vijana wavae nguo za kale na kupiga muziki wa kale ili kuwafanya watazamaji wetu wawe katika mazingira ya historia ya kale, na kufanya maingiliano kati ya hali ya kale na watu wa sasa!"

Ili kuonesha muziki wa kale wa miaka elfu kadhaa iliyopita, jumba la makumbusho la Henan limetengeneza aina zaidi ya 20 za ala za muziki za kale, na kuanzisha bendi ya muziki wa kale ya Huaxia mwaka 2000 kwa ajili ya kuonesha muziki wa kale wa China, hivi sasa bendi hiyo imeweza kupiga muziki wa nyimbo zaidi ya 200. Sauti za baadhi ya ala za muziki za kale zilizotengenezwa hivi sasa zinakaribia kufanana na sauti zinazotoka katika ala za muziki za hivi sasa.

Kuangalia mabaki ya kiutamaduni ya kale na kusikiliza muziki uliopigwa kwa ala za muziki za kale kwenye jumba la makumbusho la Henan siyo tu ni jambo linalopendwa na watalii wa kawaida, hata liliwavutia sana viongozi wa nchi mbalimbali waliotembelea huko wakiwemo wa nchi za Korea ya Kusini, Tanzania na Thailand. Bibi Wu Hong kutoka Taiwan, China alimwambia mwandishi wetu wa habari akisema,

"Leo nimeona vitu vingi sana na kusikiliza muziki uliopigwa kwa ala za muziki mbalimbali za kale, nimefurahi sana"

Kila baada ya maonesho ya muziki kumalizika, bendi ya ala za muziki ya Huaxia huwaomba watazamaji waende kwenye jukwaa kushiriki kupiga ala za muziki. Safari hiyo watalii kadhaa waliotoka Ufaransa walipiga muziki wa kwao. Muziki huo wa sasa uliopigwa na wachezaji wa China na watalii kwa ala za muziki za kale za China uliwafurahisha sana watazamaji.

Kama tunasema kuwa, mambo yanaoneshwa kwenye jumba la makumbusho la Henan kwa watalii wa nchini na kutoka nchi za nje ni historia ya China, basi muziki unaopigwa kwa ala za muziki za kale za China na bendi ya Huaxia unaonesha uzuri na kivutio cha ala za muziki za kale za China.

Idhaa ya kiswahili 2008-01-14