Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-04-08 16:07:41    
Kubadilisha maafa ya upepo kuwa chanzo cha nishati kwenye wilaya ya Tongyu mkoani Jilin B

cri

Baada ya mradi wa kipindi cha kwanza wa kituo cha kuzalisha umeme kwa nishati ya upepo cha Tongyu kuanza kujengwa, mradi huo bado ulikabiliwa na ukosefu mkubwa wa fedha. Ili kuhakikisha mradi huo unamalizika, kampuni ya umeme ya mkoa wa Jilin iliamua kukusanya fedha kwa kuwauzia hisa wafanyakazi wa makampuni ya umeme mkoani humo. Ujenzi wa mradi wa kipindi cha kwanza ulipoanza, wafanyakazi wa kampuni ya umeme wa wilaya ya Tongyu walikuwa na matumaini makubwa kuhusu mstakabali wa mradi huo, lakini walikuwa na mashaka kuhusu kununua hisa za mradi huo, kwa sababu hawajawahi kutumia fedha zao kuwekeza kwenye miradi, tena mradi huo ni mkubwa sana kwa wilaya ya Tongyu ambayo iko nyuma kiuchumi. Hivyo watu wote waliangalia msimamo wa mhandisi mkuu wa idara ya utoaji wa umeme kwa kilimo ya wilaya hiyo, ambayo imekuwa inaendelea kusukuma mbele mradi huo Bw. Gu TieZheng. Bw. Gu alisema,

"Nilinunua hisa elfu 10. Nikishughulikia kazi ya kuzalisha umeme kwa nishati ya upepo, ni lazima ninunue kwanza na ninunue hisa za kutosha. Kama sina imani kuhusu mradi huo, nitawezaje kuwashawishi wafanyakazi wengine kununua hisa?"

Bw. Gu ambaye anakaribia kustaafu, alimhimiza mke wake kutumia akiba yao kununua hisa elfu 10. Watu wengine walipoona Bw. Gu ana imani kubwa, hawakusitasita tena, na hata watu kadhaa waliazima pesa kutoka kwa jamaa na marafiki zao. Na tatizo la upungufu wa fedha lilitatuliwa haraka. Mwanzoni mwa mwaka 1999, kituo cha kwanza cha kuzalisha umeme kwa nishati ya upepo kilijengwa. Baada ya kituo hicho cha kuzalisha umeme kuanza kufanya kazi, kodi iliyotolewa na kituo hicho ilichukua asilimia 10 ya mapato ya serikali ya wilaya ya Tongyu. Kutokana na mfano huo mzuri, watu wa makampuni makubwa ya kuzalisha umeme walifika huko kukagua maliasili ya nishati ya upepo wilayani humo na kusaini makubaliano ya ujenzi na wilaya hiyo. Hivi sasa idadi ya vituo vya kuzalisha umeme kwa nishati ya upepo ambavyo vimejengwa au vinajengwa imefikia 17, na mji wa Baicheng umekuwa moja kati ya vituo vikubwa vya kuzalisha umeme kwa nishati ya upepo nchini China. Mwanzoni mwa mwaka 2008, kiwanja cha kuzalisha umeme kwa nishati ya upepo chenye uwezo wa kuzalisha kilowati laki 4 za umeme kilijengwa wilayani Tongyu. Lakini Bw. Gu Tiezheng alikabiliwa na tatizo jipya, alisema,

" wilaya ya Tongyu ina Maliasili nyingi ya nishati ya upepo, lakini matumizi ya maliasili hayo yanakabliwa na tatizo la usafirishaji wa umeme."

Wilaya ya Tongyu ikiwa ni wilaya iliyoko nyuma kiuchumi, zamani haikupeleka umeme mwingi katika gridi ya taifa, hivyo kituo kikubwa cha transfoma hakikujengwa wilayani humo. Lakini hivi sasa inazalisha umeme kwa wingi, kama haitapeleka umeme kwenye gridi ya taifa, itakuwa ni kazi bure. Kutokana na juhudi za serikali ya wilaya hiyo na serikali ya mkoa wa Liaoning, ujenzi wa kituo cha transfoma chenye uwezo wa kupeleka umeme kilowati laki 5, umewekwa kwenye mpango wa ujenzi wa majengo ya umeme wa mkoa huo, na utaanza mwaka huu. Kwa mujibu wa maendeleo ya hivi sasa, vituo vya pili na vya tatu vya transfoma huenda vitajengwa katika siku za usoni.

Kutokana na maendeleo ya vituo vya kuzalisha umeme kwa nishati ya upepo, utengenezaji wa mitambo unapata maendeleo hatua kwa hatua. Zamani watu walipeleka mitambo ya kuzalisha umeme wilayani humo kutoka miji mingine, lakini gharama za uchukuzi zinachukua nusu ya bei ya mitambo hiyo. Wanaviwanda walipoona kuwa sehemu hiyo inahitaji mitambo mingi ya kuzalisha umeme, walianza kujenga viwanda wilayani humo, ambavyo vimewapatia wakulima wa huko nafasi nyingi za ajira. Hivi sasa viwanda vya kutengeneza mitambo ya kuzalisha umeme kwa nishati ya upepo vinatoa kodi nyingi zaidi kuliko vituo vya kuzalisha umeme. Mwaka huu mapato ya serikali za wilaya hiyo itazidi Yuan milioni 100, ambayo nusu yanatokana na shughuli ya kuzalisha umeme kwa nishati ya upepo. Wilaya hiyo iliyoko nyuma kiuchumi ambayo ilihitaji msaada wa serikali inajipatia utajiri hatua kwa hatua.

Baada ya wilaya hiyo kufanya uzalishaji wa umeme kwa nishati ya upepo, wenyeji wa huko waligundua kuwa vitu vilivyowasumbua zamani vimekuwa vitu vyenye thamani kubwa. Mwangaza wa jua pia unaweza kutumiwa kuzalisha umeme. Hivi sasa kituo cha kwanza cha kuzalisha umeme kwa nishati ya mwangaza wa jua kinajengwa wilayani humo, na kitaanza kufanya kazi mwaka huu. Mwenyekiti wa bodi ya kampuni ya nishati ya upepo ya Korea Kusini ambayo iliwekeza kwenye shughuli za kuzalisha umeme kwa nishati ya upepo wilayani humo Bw. Ahn ,ameanza kufikiria mpango mpya wa uwekezaji, alisema,

"Katika sehemu hiyo maliasili ya nishati ya jua ni nyingi sana, kutokana na China kuongeza nguvu kutumia nishati hiyo, tunapanga kuwekeza kwenye shughuli za kuzalisha umeme kwa nishati ya jua katika siku za usoni."

Matumizi ya nishati ya upepo na nishati ya jua yamewafanya wenyeji wa Tongyu wafahamu nishati safi. Serikali kuu ya China iliipongeza wilaya hiyo kuwa wilaya ya kwanza ya vielelezo inayotumia nishati zisizochafua mazingira nchini China, na kutoa sera mbalimbali kuiunga mkono kuendeleza matumizi ya nishati hizo. Ili kuzuia mchanga unaopeperushwa na upepo usiharibu maskani ya wakazi wa huko, wilaya hiyo ilifanya harakati kubwa za kupanda miti katika majira ya spring kila mwaka. Eneo linalofunikwa na miti limepanuka kuwa asilimia 25 kutoka asilimia 15 mwaka 2000. Hivi sasa wakazi wa wilaya hiyo wana hamu kubwa ya kupanda miti, kwa sababu wamenufaika na upandaji wa miti. Bw. Jiang Weiguo alisema watu wote wametambua kuwa wanaweza kubadilisha mazingira mabaya kwa kupanda miti mingi, alisema,

"Tumepanda miti mashambani, hivi sasa mchanga unaopeperushwa na upepo umepungua kwa kiasi kikubwa. Kupanda miti ni jambo zuri sana. Hatuwezi kuzuia michanga inayopeperushwa na upepo bila ya miti, lakini zamani watu hawakuwa na wazo hilo."

Ingawa upepo bado unaendelea kuvuma, lakini wakazi wa Tongyu wana furaha kubwa. Wakulima wametajirika, na wanapanga kujenga nyumba mpya, wavulana hawana haja ya kufanya kazi za vibarua katika miji mingine, wasichana wamepata wachumba kwenye wilaya yao, na Bw. Gu Tiezheng ana tabasamu kila siku.

Idhaa ya kiswahili 2008-04-08