Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-11-11 21:52:32    
Vivutio vya Sichuan-wanyama Panda ambao ni alama ya Mkoa wa Sichuan

cri
Wasikilizaji wapendwa, karibuni katika kipindi hiki maalum cha chemsha bongo kuhusu "Vivutio vya Sichuan". Leo tunawaletea makala ya 4 ambapo tutazungumzia wanyama Panda ambao ni alama ya Mkoa wa Sichuan, ambao wanaishi katika hifadhi ya maumbile ya Wolong ililioko umbali wa zaidi ya kilomita 100 kutoka Chengdu, mji mkuu wa Mkoa wa Sichuan.

Kama tulivyofanya katika wiki zilizopita, kwanza tunatoa maswali mawili. Swali la kwanza, Je, Maskani ya Panda wakubwa nchini China yako Mkoani Sichuan? Swali la pili, katika eneo la hifadhi ya maumbile ya Wolong, kuna Panda wakubwa wangapi?

Wasikilizaji wapendwa, mlikuwa mkisikiliza wimbo uitwao Panda Mimi, wimbo huu ulitungwa na wanamuziki wa China zaidi ya miaka 20 iliyopita, wakati ambapo aina moja ya mianzi wanayopenda kula Panda wakubwa, ilikauka na ikafa kwenye eneo kubwa, hivyo panda wakubwa walikuwa hawawezi kupata chakula chao, wanamuziki wa China walitunga wimbo huo ili kuchangisha fedha kwa ajili ya maisha ya baadaye ya panda wakubwa. Hivi sasa katika eneo la hifadhi ya maumbile ya Wolong, mianzi ya aina hiyo inasitawi vizuri, panda wakubwa ambao ni wanyama wenye thamani kubwa kabisa wa kale duniani wanaishi vizuri katika eneo hilo la hifadhi ya kimaumbile.

Eneo la hifadhi ya maumbile ya panda wakubwa la Wolong liko kaskazini magharibi ya Mkoa wa Sichuan, ambapo panda wakubwa wengi wanaishi katika eneo hilo. Hivyo Mkoa wa Sichuan unachukuliwa kuwa ni maskani ya Panda wakubwa ambao ni hazina ya taifa la China. Kwa kuwa binadamu wanaweza kuwagundua panda wakubwa wa pori katika sehemu kadhaa za milimani katika mikoa ya Sichuan, Shanxi na Gansu, hivyo watalii wanaotaka kutazama panda wakubwa wanaweza tu kufika Bustani ya Panda wakubwa ya China kwenye eneo la hifadhi ya maumbile la Wolong. Ofisa wa eneo hilo Bwana Zhang Liming alisema:

Lengo letu ni kuwawezesha Panda wakubwa waishi maisha kwa muda mrefu, pia kuwapatia watu wanaopenda panda kote duniani fursa ya kukutana na Panda, kutokana na hayo, watalii wataelewa ni kwanini lazima kulinda mazingira ya viumbe, watafahamishwa historia ya Panda, na watafahamu umuhimu wa panda wakiwa wanyama wa kale mithili ya visukuku vyenye uhai.

Panda wakubwa ambao miili yao ni ya mviringo na minene, ambao wanatembea polepole, rangi ya manyoya yao nyeusi na nyeupe zinawavutia sana watu. Kwenye bustani ya Panda wakubwa ya China wamefugwa Panda wakubwa zaidi ya 100. Katika bustani hiyo, mwandishi wetu wa habari aliona panda wakubwa kadhaa waliochezacheza, kupanda ngazi, wengine wanaegemea mawe wakiota jua, na wengine wanapanda miti. Mfanyakazi wa bustani hiyo alimwambia mwandishi wa habari kuwa Panda ana tabia zaidi ya dubu, hivyo si rahisi kuanguka chini kutoka juu ya miti, kama wakianguka kutoka juu ya mti, panda hawawezi kujeruhiwa kutokana na unene wao na miili yao ya mviringo.

Kazi ngumu kabisa ni chakula cha Panda. Mwandishi wetu wa habari aliambiwa na mfugaji wa Panda kuwa, zamani Panda wakubwa walikula nyama, siku baada ya siku Panda hao wakaanza kula mianzi tu. Katika eneo la Wolong, mandhari nzuri na hali ya hewa yenye unyevunyevu inafaa sana ukuaji wa mianzi, hivyo eneo hilo linawavutia sana Panda wakubwa waishi na kuzaliana huko. Ingawa chakula chao kimekuwa mianzi, lakini uwezo wa Panda wa kuyeyusha chakula haukupata kuboreshwa, ili kudumisha uwezo wa miilini mwao, kwa kawaida Panda wakubwa hawafanyi shughuli kubwa, huwa wanatembea polepole. Bibi Rebecca Haase kutoka Marekani alipiga picha kuhusu Panda wakubwa walivyokula na kunywa, kucheza na kupigana, alifurahi sana kwani ni mara yake ya kwanza kukutana karibu na Panda wakubwa. Alisema:

Nimefurahi sana kuja eneo hilo kukutana karibu na Panda wakubwa, panda hao wanaonekana kuwa na afya nzuri na wanapendeza sana. Ni matumaini yangu kuwa eneo la Wolong litakuwa na Panda wakubwa wengi zaidi.

Katika Bustani ya Panda wakubwa ya China, kuna chumba kimoja cha kuwalea panda wachanga kwa njia ya binadamu. Watalii wanaweza kuona kwa kupitia kioo cha chumba hicho kuwa Panda wachanga walipozaliwa walikuwa wadogo sana mithili ya viganja vya mikono, na macho yao yalifumba, na juu ya ngozi zao kuna manyoya machache sana. Watu hawawezi kufikiri kuwa baada ya siku kadhaa watakua Panda wakubwa wanene na wenye manyoya mengi. Bwana Zhang Shichang kutoka Taiwan aliwaangalia Panda wachanga kwa muda mrefu, akashuhudia jinsi walezi walivyowanywesha maziwa ya ng'ombe Panda wachanga. Alisema:

Nimeelewa mengi kuhusu hazina ya taifa la China, mwongozaji wa utalii alinielezea hadithi ya historia ya panda, na mazingira ya kukua kwa Panda, nimejua kuwa si rahisi kwa Panda kuzaliana, na panda mama hawawezi kuwalea watoto wao wachanga.

Watalii wengi wanapenda sana panda wakubwa, hivyo wanapenda kutumia muda wao kufanya kazi ya kujitolea katika eneo la hifadhi ya maumbile ya Wolong. Mjapan Bibi Kodama Midori aliyevaa nguo ya mfugaji ni mmoja kati ya wanaojitolea. Alisema wenzake watatu walikuwa pamoja naye kufika eneo hilo, na wataishi kwa wiki moja pamoja na Panda wakubwa wa eneo hilo. Alisema:

Kila asubuhi ninawalisha Panda wakubwa, adhuhuri na jioni nilifagia vyumba vya Panda wakubwa. Kama nikija kutembea tu siwezi kupata fursa ya kukaa karibu na Panda wakubwa, hivyo nafurahi sana.

Wafugaji wa panda walifahamisha kuwa, vifo vya Panda wachanga huwa ni vingi sana, baadhi yao wanakufa kutokana na magonjwa, lakini wengi wanakufa baada ya kukandamizwa na Panda mama bila kuchukua tahadhari, na sababu kubwa ya vifo vya Panda wachanga ni kwamba, baada ya Panda kuzaa vichanga kadhaa, Panda mama anaweza kumlea mmoja tu kati yao, hivyo kama Panda wachanga wengine hawataweza kutunzwa watakufa. Watafiti wa bustani hiyo huwa wanachukua Panda wachanga walioachwa na Panda mama kuwalea kwa njia ya binadamu, ili Panda hao wachanga waweze kukua.

Hali halisi ni kwamba, watalii wakifika eneo la Wolong katika majira tofuati, wanaweza kushuhudia mchakato wa ukuaji wa Panda wakubwa katika vipindi tofauti. Mtaalamu wa utafiti wa Panda wakubwa Bwana Li Desheng alidokeza kuwa, katika majira ya siku za joto, hali ya hali ya hewa ya eneo la Wolong si joto, hiki ni kipindi cha kuchezacheza zaidi kwa panda wakubwa; na katika majira ya mpukutiko, watalii wanaweza kupata fursa ya kuona jinsi Panda wakubwa wanavyozaa Panda wachanga; na katika majira ya mchipuko ni kipindi cha Panda kuwa kwenye joto, ambapo mambo mengi ya kufurahisha yanaweza kutokea. Bwana Li alisema:

Panda wakubwa dume wa pori wanapenda kupigana kwanza, halafu washindi watapata kwanza fursa ya kuwapanda Panda jike. Lakini katika hali ya kuwafuga Panda wakubwa kwa njia ya kibinadamu haiwezekani kutokea mapigano makali kati ya Panda wakubwa dume, wakati wa kipindi cha joto kwa panda wakubwa jike, tunaweza kuwaweka Panda wakubwa dume kwenye vyumba vilivyoko karibu nao, ili waweze kuonana. Kwa kawaida, panda wakubwa hawatoi sauti yoyote, lakini wakati wa kipindi cha joto, Panda wakubwa huweza kutoa sauti za aina mbalimbali, mwanzoni wanalia mithili ya ndege, wakati wa kipindi cha mwisho wanalia kama mbwa wanavyobweka, na wakati wa kilele cha joto panda wakubwa hulia kama kondoo.

Hivi sasa katika msitu ulioko mbali na eneo la hifadhi ya maumbile la Wolong pia wanaishi Panda pori wakubwa zaidi ya 100, ambao wanachukua asilimia 10 ya Panda pori wakubwa kote duniani. Zamani watalii wa kawaida hawakuruhusiwa kuingia katika eneo la shughuli za Panda hao, lakini katika siku chache zilizopita, eneo la hifadhi ya maumbile limeanzisha mradi wa kwanza duniani wa kufanya utalii na utafiti wa kisayansi kuhusu Panda pori wakubwa, ili watalii wanaohusika wanaweza kuangalia na kuchunguza hali ya Panda pori wakubwa kwa kupitia mfumo wenye akili wa usimamizi na udhibiti.

Wasikilizaji wapendwa sasa tunarudia maswali mawili ya makala ya 4. Swali la kwanza, Je, Maskani ya Panda wakubwa nchini China yako Mkoani Sichuan ? Swali la pili, katika eneo la hifadhi ya kimaumbile ya Wolong, kuna panda wakubwa wangapi ?

Wasikilizaji wapendwa, matangazo ya makala hiyo ya 4 ya chemsha bongo kuhusu "Vivutio vya Mkoa wa Sichuan" yatarudiwa katika kipindi cha sanduku la barua wiki hii.".

Idhaa ya kiswahili 20008-11-10