• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Wanafunzi wa lugha ya Kiswahili katika chuo kikuu cha mawasiliano ya habari cha China

    (GMT+08:00) 2009-07-10 15:36:12

    Hivi sasa barani Afrika waafrika wengi zaidi wanajifunza lugha ya Kichina, lakini je mnajua nchini China pia kuna watu wengi wanaojifunza lugha ya Kiswahili? Kwa nini wanajifunza lugha ya Kiswahili, na wanajifunza lugha hiyo kwa njia gani? Kuanzia kipindi hiki cha leo, tutawajulisha vyuo vikuu vitatu nchini China vinavyofundisha lugha ya Kiswahili, yaani Chuo kikuu cha mawasiliano ya habari cha China, Chuo kikuu cha lugha za kigeni cha Beijing, na Chuo kikuu cha lugha za kigeni cha Tianjin. Katika kipindi hicho cha leo, tutawajulisha Chuo kikuu cha mawasiliano ya habari cha China ambacho ni chuo cha kwanza kilichoanza kufundisha lugha ya Kiswahili nchini China.

    Wasikilizaji wapendwa, wimbo mliosikia uliimbwa na mvulana Yang Fan na msichana Jin Xiao ambao ni wanafunzi wa darasa la kozi ya lugha ya Kiswahili la chuo kikuu cha mawasiliano ya habari cha China. Yang Fan na Jin Xiao wamejifunza lugha ya Kiswahili kwa miaka mitatu, darasa lao lina wanafunzi 15. Miaka mitatu iliyopita wengi wao walikuwa hawajui Kiswahili, lakini hivi sasa kila mwanafunzi anajua kuimba nyimbo zaidi ya 10 za Kiswahili.

    Chuo kikuu cha mawasiliano ya habari cha China zamani kiliitwa kuwa chuo kikuu cha Radio cha Beijing. Mwaka 1960 chuo kikuu cha Radio cha Beijing kilianzisha rasmi kozi ya lugha ya Kiswahili, na chuo hicho pia ni chuo kikuu cha kwanza kilichoanzisha kozi hiyo nchini China.

    Nchi nyingi za Afrika zilipata uhuru katika miaka ya 60 ya karne iliyopita. Baada ya mapambano ya muda mrefu, Tanganyika ilitangaza kujipatia uhuru tarehe 9 Desemba mwaka 1961, na Zanzibar ilitangaza kujipatia uhuru tarehe 10 Desemba mwaka 1963. Tarehe 26 Aprili mwaka 1964 Jamhuri ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar ilianzishwa, na tarehe 29 Juni mwaka 1964 jina la Jamhuri hiyo lilibadilika kuwa Jamhuri ya muungano wa Tanzania. Tanzania ilianzisha uhusiano wa kibalozi na China tarehe 26 Aprili mwaka 1964.

    Profesa Chen Yuanmeng mwenye umri wa miaka zaidi ya 60 sasa amestaafu kutoka chuo kikuu cha mawasiliano ya habari cha China, yeye aliwahi kuwa mtafsiri wa lugha ya Kiswahili katika kikundi cha madaktari wa China waliofanya kazi Zanzibar katika miaka ya 60 ya karne iliyopita. Baadaye alishughulikia mafunzo ya lugha ya Kiswahili katika chuo kikuu cha radio cha Beijing yaani chuo kikuu cha mawasiliano ya habari cha China. Profesa Chen alisema urafiki kati ya China na Afrika ulitoa fursa kwa lugha ya Kiswahili kuletwa nchini China. Profesa Chen

    Miaka ya 60 ya karne iliyopita, chuo kikuu cha radio cha Beijing kiliandikisha kwa nyakati tofauti wanafunzi wa kozi ya lugha ya Kiswahili katika mwaka 1960, mwaka1964 na mwaka 1965. Baada ya kuhimitu masomo yao, wengi wa wanafunzi hao walifanya kazi katika wizara ya mambo ya nje ya China, wizara ya biashara ya China, Radio China Kimataifa, idara ya uchapishaji wa vitabu vya lugha za kigeni, na kwenye vyuo vikuu. Miaka ya 90 ya karne iliyopita, chuo kikuu hicho kilirudisha masomo ya lugha ya Kiswahili, na kuwaandikisha wanafunzi wapya. Katika miaka 50 iliyopita, wanafunzi wapatao 141 wa lugha ya Kiswahili wa China wamehitimu masomo kwenye chuo kikuu hicho.

    Tangu mwanzo wa karne hii, uhusiano wa kirafiki na ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika umekuwa ukiendelezwa kwa kasi, hasa mkutano wa wakuu wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika hapa Beijing ulitia nguvu mpya ya uhai kwenye urafiki wa jadi kati ya pande hizo mbili. Katika hali mpya uhusiano wa kirafiki kati ya China na Afrika unakabiliwa na fursa mpya. Bi. Ao Manyun ni mwalimu wa lugha ya Kiswahili wa chuo kikuu cha mawasiliano ya habari cha China, alisema mustakabali mzuri wa ushirikiano kati ya China na Afrika unatoa fursa nyingi kwa watu wanaojua lugha ya Kiswahili.

    Chuo kikuu cha mawasiliano ya habari cha China kimeajiri mwalimu kutoka Kenya ambaye anawafundisha wanafunzi pamoja na walimu wa China kama Profesa Chen na Bi. Ao. Ili kuweka mazingira yanayowasaidia wanafunzi kujifunza lugha ya Kiswahili, chuo kikuu cha mawasiliano ya habari cha China kiliwasaidia wanafunzi hao kwenda Tanzania, ambapo walipata mafunzo ya miezi mitatu katika chuo kikuu cha Dar es Salaam. Masomo nchini Tanzania si kama tu yaliwasaidia wanafunzi hao kuinua kiwango chao cha lugha ya Kiswahili, bali pia yaliwahimiza kuelewa zaidi utamaduni wa Tanzania na watu wa huko.

    Yang Fan alisema wenzake na yeye walijifunza kuimba nyimbo nyingi za Kiswahili katika kipindi cha masomo nchini Tanzania, na wanapenda sana sanaa za Kiswahili.

    Baada ya mwaka mmoja, wanafunzi wa chuo kikuu cha mawasiliano ya habari cha China watahitimu masomo. Wanafunzi hao wana imani ya kupata ajira katika za siku za baadaye. Kutokana na maendeleo ya kampuni za China kama Huawei na Zhongxing barani Afrika, wachina wanaojua lugha ya Kiswahili barani Afrika wanahitajiwa sana. Wanafunzi wengi wanataka kwenda tena barani Afrika baada ya kuhitimu masomo yao. Walisema watafurahi sana kama wataweza kutumia lugha ya Kiswahili kutoa mchango kwa ushirikiano na mawasiliano kati ya China na Afrika.

    Wasikilizaji wapendwa, kipindi hiki cha daraja la urafiki kati ya China na Afrika kinaishia hapa kwa leo. Katika kipindi chetu cha wiki ijayo, tutaendelea kuwajulisha kuhusu vyuo vikuu vinavyofundisha lugha ya Kiswahili nchini China, msikose kutusikiliza. Kwa herini.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako