|
|
|||
Tarehe 19 rais Hamid Karzai wa Afghanistan aliapishwa huko Kabul kuwa rais wa Afghanistan, na kuanza kipindi cha pili cha urais cha miaka nitano.
Siku hiyo maofisa wa kisiasa karibu 800 kutoka Afghanistan na nchi nyingine zaidi ya 40 walihudhuria sherehe ya kuapishwa kwa rais Karzai, wakiwemo rais Asif Ali Zardari wa Pakistan, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bibi Hillary Clinton na waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Bw. David Miliband. Kwenye sherehe hiyo, rais Karzai aliahidi kuwa atachukua hatua ili kutatua masuala yafuatayo:
Kwanza ni suala la ufisadi. Kutokana na ripoti iliyotolewa tarehe 17 na jumuiya ya kimataifa ya kupambana na ufisadi, kati ya idara za kiserikali za nchi 180, hali ya ufisadi nchini Afghanistan ni mbaya zaidi ikifuatiwa na Somalia. Nchi mbalimbali za magharibi pia zilimshinikiza rais Karzai, na kumtaka atatue suala hilo. Kabla ya hapo, wizara ya mambo ya ndani ya Afghanistan tarehe 16 ilitangaza kuwa, Afghanistan itaunda idara mpya ya ngazi ya juu ya kupambana na ufisadi, ili kupambana na vitendo vya ufisadi. Rais Karzai siku hiyo aliahidi tena kuwa maofisa waliohusika na ufisadi wataadhibiwa kwa mujibu wa sheria. Alisema ufisadi ni "adui hatari" anayemkabili Afghanistan, mafisa wanaotuhumiwa kuhusika na ufisadi ni lazima wahukumiwe. Pia alisema atapambana na magendo ya dawa za kulevya.
Pili ni kuongeza imani ya umma kwa watumishi wa serikali. Kwa kuwa uchaguzi mkuu huo ulikuwa na udanganyifu katika sehemu nyingi, hivyo sura ya serikali ya Karzai imeharibiwa. Pamoja na kuwa kabla ya duru la pili la uchaguzi wa rais, Bw. Abdullah Abdullah alitangaza kujitoa kwenye uchaguzi, kwa hiyo Bw. Karzai alishinda uchaguzi huo katika hali ya kutokuwa na mpinzani. Katika hali hiyo, kama rais Karzai atawaalika wapinzani wake kujiunga na serikali mpya, itasaidia kuongeza imani na uungaji mkono wa watu kwa serikali yake. Kwenye sherehe ya kuapishwa, rais Karzai pia alisisitiza kuwa, anapenda kuwaalika wagombea wote wa rais, akiwemo Bw. Abdullah kujiunga na serikali mpya, ili kutoa mchango kwa ajili ya umoja wa kitaifa.
Tatu ni suala la usalama. Kuanzia mwaka huu, nguvu ya kundi la Taliban nchini Afghanistan imekuwa ikiimarika, na hali ya usalama inazidi kuwa mbaya siku hadi siku. Kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu, askari 472 wa jeshi la pamoja la NATO wameuawa nchini Afghanistan. Hivyo suala la usalama bado ni changamoto kubwa itakayomkabili rais Karzai katika kipindi chake cha madaraka. Kuhusu suala hilo, rais Karzai alisema jeshi la usalama la Afghanistan ni lazima lifanye kazi muhimu katika kupambana na makundi ya upinzani. Pia alisema ni lazima jeshi la usalama la Afghanistan lidhibiti hali ya usalama wa nchini Afghanistan katika miaka mitano ijayo. Lakini kundi la Taliban lilisema, halitapokea mwito wa rais Karzai kuhusu umoja wa kitaifa. Msemaji wa kundi hilo Bw. Zabiullah Mujahid alisema, serikali ya Karzai ni serikali isiyo na msingi wowote, kwa sababu jeshi la nchi za nje bado liko nchini Afghanistan.
Nne ni suala la maisha ya watu. Hivi sasa, Afghanistan bado ni moja kati ya nchi ambazo ziko nyuma kimaendeleo duniani. Kiwango cha ukosefu wa ajira nchini humo kimefikia asilimia 40, zaidi ya asilimia 50 ya watu wanaishi katika hali ya taabu sana. Kwa hiyo baadhi ya watu wanamtaka rais Karzai atatue masuala ya ufisadi na kuongeza nafasi za ajira katika kipindi chake kipya cha madaraka, na kuwasaidia kihalisi watu wa nchini kuinua kiwango cha maisha yao.
Maoni ya raia yanaonesha kuwa, hotuba ya rais Karzai imeonesha nia yake ya kisiasa ya kuanzisha mageuzi, lakini kuhimiza mageuzi sio tu kunahitaji nia, bali kunahitaji vitendo halisi. Na serikali ya Afghanistan bado inahitaji uungaji mkono wa jumuiya ya kimataifa ili kutatua masuala hayo magumu.
| © China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |