• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Wilaya ya Jixi, mkoani Anhui

    (GMT+08:00) 2013-07-15 11:14:51
    Wasikilizaji wapendwa, karibuni katika kipindi cha utamaduni wetu kinachowajia kutoka Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa, leo kayika kipindi hiki tutaangalia mambo ya utamaduni katika Jixi, mkoani Anhui.

    "unapoingia kwenye kijiji kimoja, ni kama umefungua ukurasa wa historia, na ukikanyaga jiwe, ni kama umegusa enzi moja ya kale." Hayo ni maneno yanayosemwa na wenyeji wa wilaya ya Jixi wanapojaribu kutufahamisha kuhusu maskani yao. Wanapozungumzia uzuri wa wilaya ya Jixi, huwa wanaielezea kwa fahari. Mwenyeji wa wilaya hiyo Bw Yang Shuangji ambaye alizaliwa na kukulia katika wilaya hiyo alipoeleza kuhusu mvuto wa wilaya ya Jixi alisema:

    "moja ya vivutio vya Jixi ni kitoweo cha kianhui, chakula cha mtindo wa kianhui kilianzishwa katika wilaya ya Jixi, mbali na hayo, watu wengi mashuhuri walitoka Jixi, na majengo ya kale ya wilaya hiyo pia yana uwakilishi wa mtindo wa kianhui, wilaya ya Jixi pia ni chanzo cha wino wa kianhui, ambao ni moja ya vivutio vya Jixi."

    Wilaya ya Jixi iko kusini mwa mkoa wa Anhui, umbali wa saa moja kwa gari kutoka mlima Huangshan. Wilaya hiyo ni moja ya wilaya sita za kale za Anhui, na moja ya vyanzo vya utamaduni wa Anhui, na inasifiwa kuwa ni "chimbuko la chakula cha kianhui, na chimbuko la wino wa kianhui". Utamaduni wa Anhui ni moja ya tamaduni tatu za kikanda, ambao unahusika maeneo mbalimbali yakiwemo uchumi, jamii, elimu, fasihi, sanaa, ujenzi na matibabu. Kwa upande wa kijiografia, Jixi ni sehemu ya kiini kwa utamaduni wa Anhui, na utamaduni wa Anhui unahusisha mambo mengi ya Jixi.

    Kijiji cha Longchuan ni kijiji cha kale cha ukoo wa Hu kilichoko wilayani Jixi, ukitembea kijiji hicho, utaona mnara na hekalu la kale, daraja la kale lenye paa, mitaa inayoenda sambamba na mifereji, na makazi yenye mapambo mbalimbali ya kuchongwa. Kijiji kizima ni kama jumba la makumbusho ya utamaduni wa Anhui.

    "kijiji tunachoingia sasa kinaitwa Long Chuan, kilijengwa katika enzi ya Jin ya mashariki, kijiji hiki kina historia ya zaidi ya miaka 1600. Sasa zaidi ya familia 400 zinaishi katika kijiji hicho, kwa ujumla ni wakazi zaidi ya 1300. Zaidi ya asilimia 90 kati yao wana jina moja la ukoo yaani Hu, kuna familia moja tu ambayo jina lao la ukoo ni Ding."

    Hekalu la kale la ukoo wa Hu wilayani Jixi lina ukubwa wa mita mita 1564 za mraba

    Kijiji cha Longchuan kina mabaki mengi ya kihistoria, kwa sasa ina mabaki zaidi ya 300 yaliyohifadhiwa vizuri na kikamilifu. Hekalu la ukoo wa Hu linalosifiwa kuwa ni "hazina ya taifa" ni moja ya makabi hayo. Hekalu hilo lililojengwa katika enzi ya Song lilikuwa ni hekalu ya ukoo kwa waziri wa fedha wa enzi ya Ming Hu Fu, waziri wa ulinzi wa enzi hiyo Hu Zongxian n.k.

    Katika utamaduni wa Anhui, hekalu la ukoo ni sehemu ya kuwakumbuka mababu na kuenzi maadili ya kale. Kwenye mahekalu mengi ya ukoo, kuliandikwa "nidhamu za ukoo", lengo lake ni kuwafundisha watu wa vizazi vijavyo wazingatie maadili ya ukoo na ya jamii katika maisha yao.

    Katika wakati wa kale, watu wengi kutoka wilaya ya Jixi walikuwa maofisa wa serikali au wafanyabiashara. Hali hiyo pia inatokana na utamaduni wa hekalu la ukoo. Wakati huo, mbali na wazee, watu waliofanya vizuri katika masomo au kazi zao tu waliruhusiwa kuingia kwenye mahekalu ya ukoo, kwa njia hiyo utamaduni huo unawahamaisha watoto wafanye bidii katika masomo, ili waweze kuleta fahari kwa ukoo.

    Mbali na kazi ya kuabudu mababu, mahekalu mengi ya ukoo pia ni sehemu ya sanaa. Hekalu la ukoo wa Hu linaloelekea kaskazini lina eneo la mita za mraba 1564, jengo lake kuu lina mtindo wa enzi ya Mingi, lakini mapambo yake ya ndani yana mtindo wa enzi ya Qing. Hekalu hilo lilijengwa kwa mbao na matofali, ndani yake kuna mapambo mbalimbali ya kuchongwa, sanaa hizo zina mtindo wake maalumu na zinasifiwa kuwa ni lulu inayong'ara katika sanaa ya uchongaji.

    Mapambo ya kuchongwa yameenea kila mahali ndani ya hekalu hilo, na mengi yako kwenye milango na madirisha. Mapambo hayo yote yalichongwa sura za dragon na phoenix, milima, maua na ndege au mandhari nzuri za kimaumbile n.k. uchongaji wote unaonekana kuwa na uhai. Jumba kuu la hekalu hilo ni mahali ambapo viongozi wa ukoo walifanya sherehe ya kuabudu mababu. Mapambo ya kuchongwa yaliyoko kila upande wa jumba hilo ni tofauti na mahali pengine, na pia yana maana tofauti.

    "mapambo ya upande huo yote ni maua ya lotus, mchoro wa kwanza ni maua ya yungiyungi na kaka, kwa kichina yungiyungi na kaka zikiweka pamoja matamshi yake yana maana ya "masikilizano", jamii yenye masikilizano, jamii ni kama ukoo mkubwa, ukoo mdogo ni kama bata wanaocheza kwenye maji, hii ndiyo maana ya mchoro wa pili. Mchoro wa tatu ni dagaa kamba wawili, wakati wa kale, dagaa kamba walikuwa wanamaanisha kila la heri, mchoro wa nne ni chura wawili wakilia chini ya maua ya yungiyungi, maana yake pia ni kusikilizana. Michoro hiyo minne tukiiweka pamoja, maana yake ni jamii na familia zinapaswa kusikilizana, na watu wanapaswa kupatana."

    Ukitembelea hekalu la ukoo wa Hu, utajiona kama unatazama jumba la maonesho ya sanaa za enzi za Ming na Qing.

    Huizhou, kwa jina lingine inaitwa "maskani kwa wafanyabiashara wa Anhui". Mwenyeji wa Jixi Bw. Wang Jingsong anaeleza:

    "katika enzi ya Ming na Qing, wafanyabiashara wengi wa Anhui walitoka hapa Jixi, walifanya biashara huko Hangzhou au Dunxi, popote kulipokuwa na wafanyabiashara kutoka hapa Jixi, polepole lilianza kuwepo soko halafu baada ya muda kukawa na mtaa.

    Wilaya ya Jixi inahusiana kwa karibu na kwa kina na utamaduni wa Anhui. Upande mmoja wa utamaduni huo ni utamaduni wa wafanyabiashara. Katika enzi ya Song, wafanyabiashara wa Jixi tayari walikuwa wanafanya biashara kubwa za wino wa Anhui, chai, migahawa ya chakula na vitu vingine vingi, walienea kote nchini China, hata walienda nje hadi Asia ya kusini mashariki, Ulaya na Marekani. Hadi kufikia mwanzoni mwa karne ya 20, asilimia 25 ya wakazi wa Jixi walikuwa wanafanya biashara nje.

    Mbali na wafanyabiashara, kitu kingine kinachojulikana duniani ni wino wa Anhui. Katika enzi ya Qing, kulikuwa na watu wanne waliojulikana kwa ustadi wao wa kutengeneza wino, na wawili kati yao walitoka Jixi, waliitwa Bw. Wang Jinsheng na Bw. Hu Kaiwen. Siku hizi watu wa vizazi vya Bw. Hu Kaiwen wameenea katika sehemu mbalimbali nchini China, na wamestawisha na kukuza zaidi ustadi wa kutengeneza wino, na wilaya ya Jixi ambayo ni "chimbuko la wino wa Anhui" pia imechukua hatua za kuhifadhi ustadi huo maalumu.

    Kivutio kingine cha utamaduni wa Anhui ni chakula chake. Chakula cha Anhui ni moja ya mitindo 8 ya chakula cha kichina. Wafanyabiashara wa Anhui wanapenda sana vitoweo vya nyumbani, kwa hiyo mahali popote walipofika, walikwenda na chakula cha kianhui. Moja ya chakula cha Jixi kinachojulikana ni aina ya mkate maalumu unaoitwa Ta guo, ambao inapatikana katika kila mgahawa huko Jixi. Mzee mmoja aliyekuwa anatengeneza Taguo anasema:

    "kwanza nakanda donge hadi liwe na umbo la duara, halafu naweka na kulifunika, na kukanda tena, sasa tayari imekuwa Taguo, onja ladha yake, wote walioonja wanasema ni tamu sana."

    Mkate wa Taguo una vijazo vya aina nyingi tofauti, kama vile kabichi, boga, achali na seda, na zinachanganywa na nyama za vipande vidogovidogo. Taguo ina ngozi nyembamba sana, baada ya kukaangwa inakuwa na rangi ya dhahabu. Mkate wa Taguo pia una historia ndefu, wakati wa kale wenyeji wa Anhui walipofanya kazi mashambani, kama vile kukata kuni au kuchota chai, hawakuweza kurudi nyumbani kula chakula cha mchana, kwa hiyo iliwabidi wabebe chakula, na mkate wa Taguo ni chakula walichobeba. Wafanyabiashara wa Anhui walipotoka nje kufanya biashara, iliwabidi watembee siku kwa kadhaa kuvuka milima, mikate hiyo pia ilikuwa ni chakula chao kwa sababu ujazo una achali yenye chumvi nyingi, na kwa hiyo inaweza kuhifadhiwa kwa siku kadhaa bila kuharibika.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako