• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Utamaduni wa mkoa wa Guangdong

    (GMT+08:00) 2013-08-05 11:13:50

    Kwanza kabisa, mkoa wa Guangdong uko kusini mwa China. Kwa kuwa sehemu nyingi za mkoa huo ziko pwani, watu wengi walihamia nchi za nje kwa sababu mbalimbali. Takwimu zinaonesha kuwa idadi ya wenyeji wa Guangdong wanaoishi nchi za nje zaidi ya 160, ni zaidi ya milioni 30, ikiwa ni theluthi mbili ya wachina wanaoishi nchi za nje.

    Bw. Liang ni mkazi wa wilaya ya Kaiping mkoani Guangdong ambaye wazazi na dada zake wote wamehamia nchini Canada. Hapa anaelezea zaidi.

    "Zaidi ya miaka 100 iliyopita, watu wengi wa wilaya yetu walikwenda nchi za nje kutafuta maisha bora. Baadaye wengine walikwenda kupitia msaada wa wenyeji waliowatangulia. Leo pia kuna watu wanaojaribu kuhamia nchi za nje. Hapa kwetu, katika zama za kale, watu wengi walihamia Marekani ambapo wachimbaji madini na wajenzi wa reli walihitajika sana."

    Bw. Liang anasema wakati huo, wachina wanaoishi nchi za nje walichangia sana maendeleo ya uchumi wa nchi walizohamia, pia wengi wao walipata maisha bora kuliko nyumbani. Ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zikiwemo ubaguzi na tofauti ya utamaduni, watu hao walikusanyika na kuishi kwa pamoja.

    Mji wa Jiangmen umesifiwa kuwa mji wa kwanza wenye wachina wengi zaidi waliohamia nchi za nje hapa China

    Watu hao wenye asili ya kichina pia wametoa mchango mkubwa kwa ajili ya maendeleo ya jamii na uchumi wa China. Bw. Zhao Tailai ni mchina anayeishi nchini Uingereza. Ili kutafuta vitu vya kale vya China venye thamani kubwa ya utamaduni, ambavyo vilihifadhiwa na mababu zake kwenye bustani ya nyumba ya familia yake nchini Uingereza, aliomba uraia wa Uingereza, na alitunza vitu hivyo kwa miaka 10. Hatimaye, alivikabidhi vitu hivyo vyote kwa serikali ya China. Ili kupata fedha nyingi zilizohitajika kusafirisha vitu hivyo, alilazimika kuuza nyumba zake nne. Hivi sasa vitu hivyo vinahifadhiwa katika jumba moja la makumbusho mjini Guangzhou, mkoani Guangdong.

    Bw. Zhao ni mfano mmoja wa wachina wanaoishi nchi za nje ambao wametoa mchango mkubwa kwa ajili ya maendeleo ya China. Takwimu zinaonesha kuwa, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2011, mkoa wa Guangdong ulipata uwekezaji wa dola za kimarekani bilioni 270 kutoka nchi za nje, na kati ya fedha hizo, asilimia 70 zimetolewa na wachina wanaoishi nchi za nje.

    Nyumba ya ngoma wilaya ya Kaiping, mkoani Guangdong ni nyumba ya watu waliofanya kazi nchi za nje, pia ni ngoma yao ya kujilinda. Katika zama za kale, wachina wengi waliotajirika katika nchi za nje, waliamua kurudi nchini China baada ya kuzeeka. Ili kulinda mali zao, walijenga nyumba ya ngoma. Bw. Chen ambaye ni mkazi wa wilaya ya Kaiping anafafanua zaidi jinsi mambo yalivyokuwa.

    "Wakati huo kulikuwa na wizi na majambazi wengi, hali hiyo ilitulazimisha tujifiche katika nyumba ya ngoma wakati wa usiku."

    Nyumba za ngoma wilayani Kaiping zina mitindo tofauti, kwasababu wamiliki wa nyumba hizo walikuwa wanaishi nchi mbalimbali za nje. Hivi sasa wakazi wa wilaya ya Kaiping hawana wasiwasi kuhusu wizi au majambazi, na nyumba hizo zimekuwa mandhari ya kuvutia wilayani humo.

    Vyakula vya Guangdong ni moja kati ya aina nne muhimu ya vyakula nchini China, vingine ni vyakula vya Shandong, Sichuan na Jiangsu. Vyakula vya Guangdong vina historia ndefu, na vilianza kujulikana wakati wa enzi ya Qin zaidi ya miaka 2,200 iliyopita. Katika enzi ya Qing, mji wa Guangdong ulikuwa mlango wa China wa kufanya biashara na nchi za nje, hivyo vyakula vya Guagndong vilichanganywa na vyakula vya nchi za magharibi. Hivi sasa vyakula vya Guangdong vinajulikana nchini China na nchi za nje, na kupendwa na watu wengi.

    Licha ya vyakula rasmi, kifunguakinywa cha Guangdong pia ni maarufu sana. Mkahawa mmoja ulioko kando ya bustani ya Yuexiu mkoani Guangzhou, unawavutia wateja wengi kila asubuhi, akiwemo Bw. Wu. Hapa Bw Wu ambaye ni mteja anaelezea zaidi

    "Napenda sana kifunguakinywa hapa. Kila asubuhi, naamka mapema sana. Baada ya kufanya mazoezi ya kujenga afya, ninakuja hapa kula kifunguakinywa, na kuongea na watu wengine. Halafu ninaenda bustani kutazama magazeti."

    Mbali na kifunguakinywa, supu ni alama nyingine ya utamaduni wa vyakula vya Guangdong. Methali moja ya Guangdong inasema, heri nikose chakula kuliko supu. Watu wa Guangdong wamezoea kunywa supu kabla ya kuanza kula chakula. Inasemekana kuwa hali hii inatokana na hali ya hewa mkoani humo. Mkoani Guangdong, ni lazima wapishi wawe na uwezo wa kupika supu nzuri. Bw. Wang Shunbo ambaye anapenda sana kupika supu, anaelezea sababu zake.

    "Napenda kupika supu kwa kutumia chungu, kwa sababu chungu hicho kinafaa sana kuchemshia maji na vyakula. Supu iliyopikwa kwa kutumia chungu ni tamu zaidi."

    Basi kabla ya kukamilisha kipindi chetu cha leo, hebu kwanza sikiliza wimbo huu mzuri ulioimbwa na mwenyeji wa Guangdong.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako