• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Barua 0114

    (GMT+08:00) 2014-01-14 20:31:23
    Barua ya kwanza inatoka kwa msikilizaji wetu Stephen Magoye Kumalija wa S.L.P 1067 Kahama Shinyanga Tanzania anaanza kwa kusema ni matumaini yangu makubwa kuwa hamjambo sana wafanyakazi wote wa Idhaa ya Kiswahili ya redio China Kimataifa kutoka mjini Beijing, kwa upande wangu mimi ni mzima na naendelea kama kawaida na shughuli za ujenzi wa taifa langu la Tanzania, pamoja na kusikiliza na kufuatilia kila siku matangazo yote ya CRI idhaa ya Kiswahili.

    Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii ili kuwapa pole watanzania wenzangu huku visiwani Zanzibar, kufuatia kuzama kwa meli iliyokuwa ikitokea mjini Dar es Salaam, na kuzama huko Nungwi Zanzibar na kuuwa watu wapatao mia mbili na arobaini na wengine zaidi ya 600 kuokolewa. Hata hivyo ninawaomba viongozi wa serikali yetu ya Tanzania pamoja na ndugu na jamaa za watu waliopoteza maisha na marafiki zao wawe na subira, kwani kazi ya Mungu haina makosa.

    Tunakushukuru kwa dhati msikilizaji wetu Stephen Magoye Kumalija kwa barua yako ingawa ya zamani lakini imefika na tunaisoma. Hata kama muda umepita sana tangu itokee ajali hiyo, nasi kwa upande wetu hatutasita kuendelea kuwatakia faraja na kuwasihi wafiwa wote waendelee kuvumilia, kwani tunafahamu kuwa kidonda cha kufiwa huwa hakiponi, ahsante sana.

    Barua nyingine inatoka kwa msikilizaji wetu Abdi Saidi Iyula Senduka wa S.L.P 6 Kondoa Tanzania anasema kwa kweli ninatoa shukurani kwa ukarimu wenu watu wa China kwa kunisaidia kuwa na hamasa ya kuwa na fikira za kuitembelea China. Kwani mmenifahamisha namna ya kuomba viza ya China pamoja na taratibu nyingine. Pamoja na kuwa nilikuwa na fikira za kutembelea China, kukosekana kwa ufahamu wa taratibu za kuomba viza ilikuwa ni tatizo kubwa kabisa.

    Ndugu wa CRI mimi sikuipenda redio hii kwasababu ni redio yenye majikwazo ya ajabu ajabu, bali nimeipenda kwa sababu CRI ina utaratibu mzuri. Kwa mfano hapa kwetu Tanzania kuna redio nyingi za mataifa haya ya magharibi ambazo sikuzipenda sana kutokana na mfumo wao wa kibepari, japo nilianza kusikiliza siku nyingi. Ahsante sana

    Tunakushukuru sana msikilizaji wetu Abdi Saidi Iyula Senduka kwa barua yako, tunakupongeza kwa kuweka waziwazi hisia zako za kutuunga mkono, kutokana na utaratibu wetu mzuri, tunashukuru kwa hilo. Tunaomba tu usichoke kusikiliza matangazo yetu, kwani mbali na habari pia tunawapatia ujuzi hasa wa kuongea lugha ya kichina ahsante sana.

    Mwisho tunawaletea ujumbe tuliotumiwa na wasikilizaji wetu kwenye tovuti yetu, kwanza ni Samson Kyanzi wa S.L.P 1882 Mbeya Tanzania anasema napenda kushukuru kwa kazi nzuri ya kutuhabarisha kutuelimisha na kutuburudisha Mungu awe nanyi.

    Naye Mutanda Ayub anasema nimefurahi sana kusoma habari za CRI, na nimeshasoma kumbukumbu za barua katika kipindi cha sanduku la barua na nimefurahia jinsi zimepangwa ni nzuri sana.

    Msikilizaji wetu Langi Stany baruapepe yake ni langikitunda@yahoo.fr anasema nataka kuipongeza sana China kwa uhusiano wake huu na Kenya naamini hii si kwa Kenya peke yake bali ni Afrika nzima. Hongera idhaa hii ya Kiswahili ya redio China. Naamini hata hapa Kongo mtahitaji kuwa na mwakilishi siku moja. Kazi njema na salamu kwa wote.

    Joshua anasema napenda kusikia habari zenu. Kwa kweli mpo juu sana. Naomba uhusiano udumu wandugu mjitahidi kuboresha bidhaa zenu ziwe bora na kudumu ili kila mtanzania afaidike ni hayo tu.

    Mwisho ni Stephen Michieka anasema zidisha uchapishaji wa habari za majimbo na mitaa ya mabanda mijini. Habari hizi hutokea kwa wingi bali hukosa ripota wa kiwango cha mitaa hasa.

    Tunawashukuru kwa dhati wasikilizaji wetu wote mliotutumia ujumbe kupitia kwenye tovuti yetu, tunaomba muendelee kusikiliza matangazo yetu zaidi na kutoa maoni na mapendekezo zaidi. Ahsante sana.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako