• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • barua 0121

    (GMT+08:00) 2014-01-25 20:48:04
    Barua ya kwanza inatoka kwa msikilizaji wetu Philip Ng'ang'a Kiarie wa S.L.P 601 Maragua Kenya, anaanza kwa kusema kwanza nawapa mkono wa salamu wana idhaa ya Kiswahili ya redio China Kimataifa. Pili sina budi kuwapongeza wachina wote mahali popote walipo. Bila shaka uvumbuzi na vitu vilivyobuniwa na watu wenye ujuzi na teknolojia za kisasa wa China umewanufaisha watu wengi sana na pia kuboresha pamoja na afya. Ninapofikiria kiwango ambacho China imewanufaisha watu duniani kote, wengi watakubali kwamba China ndiyo itaubadili ulimwengu kikweli.

    Hata hivyo jambo linalothibitisha kwamba wananchi wenye hekima wa China ni wa pekee na bado watu wa mataifa karibu yote duniani wanaamini na kupenda vyombo na vitu vilivyotengenezwa China bila ya kusahau misaada yake isiyokuwa na masharti yoyote. Kwa kweli kuna nchi ambazo huishushia heshima China kwa vile nchi hizo zina kijicho huku wakisahau kuwa China hujiunga na wengine wakati wa matukio ya dharura, huwapongeza wenye kufanya vizuri, hufurahia kuwa pamoja na mataifa mengine na wachina ni watu wenye hekima ya kipekee. Hata hivyo China imewapita wote umaarufu wake na uvumbuzi wa kisayansi unazidi kuwapa matumaini watu kote duniani, ahsante sana.

    Tunakushukuru kwa dhati msikilizaji wetu Philip Ng'ang'a Kiarie kwa barua yako, pia tunakushukuru kwa sifa ulizotumwagia wachina, kwani kawaida mtu akitenda mema ni lazima asifiwe, na sisi kwa upande wetu wachina tunajitahidi kuwafanyia wema hasa marafiki zetu wa enzi na dahari kama vile nchi za Afrika.

    Barua nyingine inatoka kwa msikilizaji wetu Gulam Haji Karim wa S.L.P 504 Lindi Tanzania naye anasema salamu sana natumaini hamjambo na mnaendelea vizuri na pirika za kazi, kwa upande wangu ni mzima, ni muda mrefu nimekaa kimya lakini sio lengo langu ila ni kutokana na hali ya maisha kuwa ngumu, inaturudisha nyuma.

    Leo ningependa nikuzungumzia kuhusu kipindi cha sauti ya wanawake kilichorushwa tarehe 5 mwezi wa 4 mwaka 2011 kuhusu ndoa. Ndoa yaani kuoa au kuolewa ni kuzuri na pia kuna ugumu wake, ndoa nyingi za siku hizi ni za ubabaishaji, utaona mwanamke au mwanamume wanadai wanapendana na kuanza kufanya tendo la ndoa kabla hata ya hiyo harusi yenyewe kufungwa, mara tu mwanamke akihisi kuwa ni mjamzito hapo ndio balaa linapoanza, mwanamume anaanza mkwara na kutoa sababu kama vile, si nilikukuta na yule rafiki yako, mimba hii sio yangu, mtafute mwenyewe umpe.

    Katika maisha ndoa ni kitu azizi, inahitaji ichukuliwe kwa uangalifu na tahadhari kubwa kabla ya wawili hao kujuana na kuelewana. Mfano mimi nilihimizwa kuoa nikiwa nina miaka 25 lakini sikutaka kuoa, niliendelea na ubaleghe mpaka nilipofikisha miaka 35 ndio nikaoa. Sasa nina miaka 40 tunaelekea uzeeni na bado ndoa yetu ipo shuwari, kwa hiyo tatizo ni ndoa za utotoni, ahsante sana.

    Tunakushukuru sana msikilizaji wetu Gulam Haji Karim kwa barua ambayo umezungumzia mada adhimu kabisa ya "Ndoa". Ni kweli ndoa ni kitu azizi, lakini vijana wa siku hizi wanachukulia kama ni mahali pa kufanya majaribio. Wawili wanapopendana wakafikia hadi kuoana, basi wameaminiana, hivyo wanatakiwa kustahamiliana kwa kila kitu. Uvumilivu na mapenzi ni nguzo kubwa ya ndoa, ahsante sana.

    Mwisho tunawaletea maoni tuliyotumiwa na wasikilizaji wetu kupitia kwenye tovuti yetu kwanza ni Paskali Malkiadi anasema hongereni sana kwa kazi yenu.

    Eliezer Alfred anasema nawapongeza wote kwa kutoa huduma nzuri

    Na mwisho ni ujumbe kutoka msikilizaji wetu Mogire Machuki wa Kisii Kenya anasema asante sana CRI kwa taarifa hii ya kina kuhusu mkoa wa Anhui. Tamaduni kama hizi daima huwa ni za kuvutia mno. Salamu za mchana Beijing. Hapa shwari kama kawaida hapa nipo na marafiki zangu na mapema ili kufahamu yaliojiri Beijing na pia kusoma baadhi ya yale mapya ambayo mmechapisha kwenye tovuti yenu, ahsante sana.

    Tunapenda kuwashukuru wasikilizaji wetu wote mnaotembelea tovuti yetu ili kupata habari na matukio mbalimbali, mbali na tovuti pia tunawasihi musikilize matangazo yetu kwenye redio ili muweze kutoa maoni na mapendekezo yenu kwa lengo la kuboresha zaidi matangazo yetu, ahsanteni sana.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako