• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Sera ya China kuhusu watoto wawili yafuatiliwa na watu

    (GMT+08:00) 2014-01-19 20:46:50
     Sera ya uzazi wa mpango ni sera muhimu hapa China. Kadiri hali ya uchumi na jamii inavyozidi kupata maendeleo, ndivyo sera hiyo inavyozidi kurekebishwa na kukamilika. Hivi karibuni serikali ya China imetangaza kutekeleza sera ya watoto wawili kwa familia ambayo mmoja kati ya wanandoa ni mtoto wa pekee katika familia yake. Sera hiyo imethibitishwa katika Mkutano wa tatu wa Kamati kuu ya 18 ya chama cha Kikomunisti cha China uliofanyika mwezi uliopita na katika Mkutano wa 6 wa baraza la 12 la kudumu la bunge la umma la China uliofanyika tarehe 23 Desemba mjini Beijing.

    Ili kuzuia idadi ya watu isiongezeke kwa kasi kupita kiasi, na kuinua sifa ya watu, tangu miaka ya 70 ya karne ya 20, China imekuwa ikitekeleza sera ya uzazi wa mpango, na kuifanya kuwa sera ya kimsingi ya taifa, pia imekamilishwa kwa kufuata mabadiliko ya hali ya idadi ya watu, na maendeleo ya uchumi na jamii. Wachambuzi wanaona kuwa, utekelezaji wa sera hiyo umesaidia katika kupunguza shinikizo la mazingira ya asili, na kuhimiza maendeleo endelevu ya uchumi na jamii. tangu ianze kutekelezwa sera hiyo, hali ya idadi ya watu nchini China imekuwa ikibadilika. Kiwango cha chini cha uzazi kilichodumu kwa zaidi ya miaka 20 kimeshuka kupita kiasi, hali ambayo imeleta tatizo la kimuundo la idadi ya watu.

    Mkurugenzi wa Chuo cha Jamii na idadi ya watu katika Chuo Kikuu cha Renmin cha China Bw. Zhai Zhenwu anaona kuwa, marekebisho ya sera ya uzazi wa mpango yamefanyika kwa wakati na yana umuhimu mkubwa kwa China.

    "Kutokana na hali ya hivi sasa ya China, kukamilisha na kurekebisha sera za uzazi wa mpango kunasaidia kupunguza tatizo la kuwa na idadi kubwa ya wazee katika jamii, kusaidia kuboresha muundo wa familia, na kuhimiza uwiano wa kijinsia."

    Sera ya watoto wawili kwa familia ambayo mmoja kati ya wanandoa ni mtoto wa pekee katika familia yake itawahusisha watu milioni 15 hadi 20.

    Sera hiyo ina umuhimu kwangu, kwani mimi ni mtoto wa pekee katika familia yangu. Kama nitakuwa na watoto wawili, wataweza kucheza pamoja, na nikiwa mzee, wataweza kugawana majukumu ya kunitunza."

     "Naunga mkono sera hii. Kwani sera hiyo inawasaidia na kuwanufaisha watu wanaopenda watoto."

    Sera hiyo inatunufaisha, kwani wazazi wangu pia wanataka nipate watoto wawili.

     "Naona sera hiyo ni nzuri. Kwani hivi sasa kuna wazazi wengi wenye mtoto mmoja tu, endapo mtoto huyo wa pekee atakufa kwa ajali, basi wazazi watakabiliwa na changamoto kubwa."

    Suala la utekelezaji wa sera hiyo utaleta mabadiliko gani kwa hali ya idadi ya watu nchini China pia linafuatiliwa na watu. Je, watu wangapi wana nia ya kupata mtoto wa pili?

     "Nina mpango huo. Watoto wawili watakuwa wenzi wazuri."

     "Kwangu mimi binafsi, nitafikiria kwa makini kama nitapenda kupata mtoto wa pili au la."

     "Mtoto mmoja anatosha. Naona haina haja ya kupata mtoto mwingine, kutokana na shinikizo kubwa la maisha kama vile mshahara na bei kubwa ya nyumba, nadhani watoto wawili watakuwa shinikizo kubwa kwangu."

     "Vijana kwa hivi sasa wanakabiliwa na shinikizo kubwa la nguvu ama fedha, isitoshe wako kazini kila siku, na hawana muda wa kuwatunza watoto, na hawawezi kuwalea watoto bila ya msaada wa wazee."

    Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanyika, kati ya watu milioni 15 hadi milioni 20, asilimia 50 hadi 60 wanapenda kupata mtoto wa pili, na idadi ya watu wanaopenda kupata mtoto wa pili katika miji mikubwa ni ndogo kuliko ya watu wa miji midogo na ya kati. Mtafiti wa Taasisi ya uchunguzi kuhusu mageuzi ya utaratibu wa uchumi ya China Bw. Li Xiaoning anasema:

    "Miji midogo na ya kati inatofautiana na miji mikubwa. Gharama za kuishi katika miji mikubwa kama vile Beijing, Shanghai na Guangzhou ni kubwa sana, na shinikizo la kupata mtoto wa pili pia ni kubwa. Lakini hivi sasa watu wengi wanapenda kutafuta ajira katika miji mikubwa, hivyo naona hakuna uwezekano kuwa idadi ya watoto itaongezeka kwa kiasi kikubwa."

    Wataalamu wanaona kuwa, hatua mbalimbali za kusaidia kupunguza shinikizo la uzazi wa mpango zinatakiwa kuchukuliwa ili kuhakikisha sera ya watoto wawili inatekelezwa kwa utaratibu.

    Wasikilizaji wapendwa, mliyosikia ni sera ya watoto wawili ya China kwa familia ambayo mmoja kati ya wanandoa ni mtoto wa pekee katika familia yake. Sasa tutupie macho Kenya barani Afrika, kwani nchi hiyo pia inazingatia suala la idadi ya watu, na kutekeleza sera ya "uzazi wa mpango".

    Pendekezo la serikali ya Kenya kwa kila familia nchini humo kupata watoto wasiozidi wawili limeendelea kuzua hisia tofauti kwa wananchi wake.

    Baadhi ya wakenya wanadai kuwa serikali haifai kuingilia swala la kupata watoto huku wengine wakiunga mkono pendekezo hilo.

    Mwandishi wetu kutoka studio zetu za Nairobi Mark Muli aliongea na baadhi ya wakenya na kutuandalia taarifa ifuatayo.

    Kulingana na serikali ni kwamba idadi ya wananchi humu nchini inaendelea kukua kwa haraka na huenda idadi hii ikapita ile serikali inaweza kukidhi katika mahitaji ya kimsingi ikiwa haito chukua hatua.

    Sababu za idadi ya wakenya kuongezeka kwa wingi serikali imesema zimetokana na kuimarika kwa hali ya maisha humu nchini na sasa ongezeko hili linafaa kushugulikiwa.

    "Serikali ya Kenya kwa sasa inalenga kudhibiti ongezeko la wananchi wake kwa kupunguza watoto ambao kila familia inafaa kuapata, kutoka watoto 4.6 kwa kila mwanamke hadi watoto 2.6 ifikapo mwaka wa 2030, na kisha watoto 2.1 ifikapo mwaka wa 2050."

    Kwa sasa idadi ya wananchi humu nchini inakua kwa asilima 3 kila mwaka ambayo ni idadi ya watu milioni moja kila mwaka.

    Ikiwa idadi ya wakenya itaendelea kukua kwa asilimia hio ifikapo mwaka wa 2030 nchi hii itakuwa na wananchi takribani milioni 55 na kufikia viwango ambavyo serikali inasema.

    Baada ya serikali kutoa pendekezo la kila familia humu nchini kupata watoto wasiozidi wawili, pendekezo hili limeanza kuzoa hisi tofauti tofauti miongoni mwa wakenya.

    Baadhi ya wakenya wanaounga mkono pendekezo hili ni wale wanaoishi katika miji na walio elimika.

    Vincent Ouma ni mkaazi wa jiji kuu la Nairobi na kwake pendekezo hili limekuja katika wakati unaofaa.

    Ouma anasema kuwa katika hali ya sasa ya ukosefu wa fursa za kazi, ukosefu wa chakula na pia maisha bora hatua hiyo inafaa kabisa.

    "Katika hali ya sasa watu wanaendelea na kuongezeka, ukosefu wa kazi pia upo kwa wingi, chakula ndio hicho kimepotea, unaona sasa ukipata watoto wengi sasa bila shaka utashindwa kuwalea"

    "Katika maeneo ya mashambani hali ni tofauti sana.

    Mzee Matumoni Lelkuoni ni mwenyeji wa Samburu na kulingana na yeye ni kwamba watoto wengi ni baraka na udhibitisha uwezo wa mwanaume katika jamii.

    Anaeleza kuwa serikali inafaa kuachia mzigo wa uzazi, akisema yeye ana wawtoto zaidi ya 16 na wake zaidi ya 3.

    Mzee Matumoni anazidi kueleza kuwa katika mila za jamii yake lazima mwanaume apate wake wengin na watoto ili aweze kutambulika na kupewa hadhi katika jamii yao.

    Aidha anasema azma ya jamii yake ni wao kuwa wengi.

    "Sisi tunataka kuwa wengi, mimi niko na watoto kumi na sita, mimi ninawalisha hao wototo wote mzuri sana.Hakuna mtu anayenisaidia hata kidogo.

    Sisi katika kimila yetu kama wasamburu ikiwa una mke mmoja wewe hauna manyatta na hautambuliki"

    Kando na mzee Matumoni Daniel Juma ambaye ni kijana wa umri wa miaka 24 anasema yeye haoni shida ya serikali kutoa pendekezo hilo.

    Anasema kwake hata motto mmoja anatosha ukilinganisha na hali ya maisha ilivyo kwa sasa.

    "Mimi naona kwamba hata moto mmoja ni tosha, kwa sababu bora uitwe mzazi.Naamini kuwa ukipata mtoto mmoja utakuwa na uwezo wa kumshughulikia katika maisha yake vilivyo hata katika masomo.

    Mambo sasa imekuwa ni ngumu sana.Kwa hivyo mtoto mmoja kwangu ninaona anatosha."

    Mzee Odongo Randa ni mzee aliye na umri wa miaka 72 kutoka eneo la Nyanza humu nchini.

    Kulingana na yeye ni kwamba wananchi wanafaa kuachiliwa wajichagulie idadi ya watoto kila familia inataka kupata katika ndoa.

    Mzee Odongo anashangaa ni kwa nini hilo lifanyike ilhali watu wanafariki kutokana na majanga tofauti humu nchini, akihoji kuwa pengo hilo linafaa kuzibwa.

    "Wachaneni na watu waendelee kuzaana, kwa sababu siku hizi watu wanakufa kama inzi, watu wanakufa na Ukimwi katika nchi yetu hii, na sasa kama mtasema kila mwanamke apate watoto wawili nani anajua kwamba hao watoto wataweza kuishi?"

    Vivian Wanjiku kijana wa miaka 26 na mkaazi wa Nairobi anasema kuwa wanotaka kuendelea kupata watoto wengi ni wale bado hawajaweka mpango mahususi wa kuhakikisha kuwa watoto wao wanapata maisha mazuri ya baadaye.

    Wanjiku anasema wazo hilo la serikali kwa familia kupata watoto wasiozidi 2 linafaa kutekelezwa pasipo pingamizi.

    "Mimi nafikiria ni wazo nzuri, kwa sababu ni vyema mtu kupata watoto ambao anaweza kulea vizuri pasipo na taabu."

    Hatua hii ya serikali ya kutoa pendekezo hilo imekuja hata baada ya kuweko kwa mpango wa kupanga uzazi uliokuwa ukitiliwa mkazo na serikali kwa muda wa miaka kadha sasa.

    Serikali inasema mpango huo wa kupanga uzazi uliwapa wanandoa fursa ya kuamua idadi ya watoto watakao pata lakini sasa itabidi serikali kuweka idadi hii ya watoto 2.

    Sera ya kuzaa watoto wawili kwa familia ambayo mmoja kati ya wanandoa ni mtoto wa pekee katika familia yake hapa nchini China, pamoja na pendekezo la kuzaa watoto wawili lililotelewa na serikali ya Kenya, zote zinalenga kusawazisha mapungufu yaliyojitokeza kufuatia idadi kubwa ya watu kati ya nchi hizi mbili, kwa hapa China habari hizo zimepokelewa kwa furaha, lakini je kwa upande wa Kenya pendekezo hili litazingatiwa na hatimaye kupitishwa na kuwa sera kamili.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako