• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Lugha ya Sheng yalaumiwa kwa kuangusha lugha za Kiingereza na Kiswahili

    (GMT+08:00) 2014-03-14 11:04:04

    Lugha ya Sheng ni moja wapo ya lugha zinazotumiwa na wananchi nchini Kenya mbali na lugha za Kiingereza na Kiswahili. Lugha hii ni mchanganyiko wa Kiswahili, Kiingereza na lugha nyingine za Kibantu japo sio lugha rasmi.

    Kwa sasa lugha hii imeweza kuenea katika maeneo mengi ya Kenya licha ya kuonekana kama Lugha ya vijana pekee. Katika matokeo ya kitaifa ya shule za msingi na upili nchini Kenya kwa muda wa miaka mitatu ambayo imepita, masomo ya lugha ya Kiswahili na Kiingereza yamekuwa yakiendelea kudorora na lawama kutupiwa lugha hii ya Sheng.

    Mara ya kwanza lugha hii kutajwa kama sababu kuu kwa lugha hizi kuanza kodorora ilikuwa ni mwaka  2011, baada ya aliyekuwa waziri wa elimu wa wakati huo Profesa Sam Ongeri kutaja lugha hiyo kama hatari kwa lugha hizo katika shule, suala hilo likaendelea kujitokeza katika mitihani ya mwaka 2012 na 2013.

    Lakini swali ni je, lugha hii ya Sheng ina hatari yoyote kwa lugha hizi mbili za Kiingereza na Kiswahili na inafaa kulaumiwa katika shule za Kenya? Mwandishi wetu Mark Muli kutoka studio zetu za Nairobi ameliangazia swala hilo na kuandaa ripoti ifuatayo.

    Simon Oloisoya Shitipha amekuwa akifunza katika shule ya msingi ya Moi Avenue hapa jijini Nairobi kwa miaka sita sasa. Katika muda huo wote amekuwa akifunza lugha ya Kiswahili, na ameshuhudia matokeo ya wanafunzi wake katika lugha ya Kiswahili yakiendelea kudorora.

    "Lugha ya Kiswahili na Kiingereza kwa jumla zimekuwa zikishuka na ninaona ya kwamba tukiendelea na maisha haya hali ya lugha ya Kiswahili na Kiingereza itaendelea kuwa mbaya zaidi."

    Shida kubwa ya kuanza kudorora kwa matokeo katika masomo ya lugha katika shule yake na katika shule nyingine nchini ni nini?

    "Mimi ninaona tu Sheng ndiyo lugha ambayo inaathiri Kiswahili kiasi ya kwamba lugha hiyo ndiyo wazazi hata waalimu wanaitumia mpaka hata wakati wanafunza."

    Bi Vivian Rotich pia ni mwalimu wa lugha katika shule hii ya Moi hapa jijini Nairobi.

    Anaeleza lugha hii imekuwa mzigo mkubwa kwa wanafunzi wake katika darasa la tano analofundisha Kiswahili.

    "Sheng imeathiri wanafunzi wa darasa la tano kiasi kwamba hata ukiwafunza sasa hivi, ukienda darasani wanajibu maswali wakitumia lugha ya Sheng."

    Lawrence Munuve ni mzazi na swala la mtoto wake kutumia lugha ya Sheng katika mtihani sio geni kwake.

    "Wakati tunadurusu mitihani yake haswa katika somo la Kiswahili unapata anachanganya lugha kwa sababu hiyo ndio lugha wanayotumia wakicheza na wenzake.Kwa hivyo hilo linawatia katika mashaka wanapojibu mitihani kwa kuwa hawajui lipi ndilo nzuri na lipi lililosahihi."

    Eunice Wanjiku Ng'ethe alimaliza kidato cha nne mwaka jana katika shule ya upili ya Mumbi katika mkoa wa kati, na anasema lugha ya Sheng ilimpa changamoto si haba, katika masomo yake, hususan baada ya kuzoea kuitumia sana.

    "Lugha ya Sheng imeniathiri sana  mimi piakatika njia zote katika masomo yangu. Lugha hii ilifanya masomo yawe magumu kwangu kwa kiasi fulani haswa katika somo la Kiswahili."

    Mwalimu Simon Oloisoya anasema maisha ya sasa ndiyo yanafaa kulaumiwa kutokana na kuongeza na kusambaza matumizi ya lugha hii hususan vyombo vya habari.

    "Kile kinachangia sana ni maisha haya ya kisasa, vyombo vya habari, kando na vyombo habari pia walimu, wazazi na watu wengine kwa jumla."

    Lakini tofauti na wanaolaumu lugha hii ya Sheng na kusema ni hatari kwa lugha hizi mbili, Omar Babu Marjan ambaye ni mhadhiri wa Kiswahili katika chuo kikuu cha Cologne nchini Ujerumani, anasema shida sio Sheng, bali ni watumiaji wa lugha.

    Omar Babu Marajan:

    "Mpaka tuzingatie tujue kwamba lugha za vijana zipo, katika maeneo yote kote Duniani. Kwa mfano kuna Kiswanglish jijini Dar es Salaam Tanzania, kuna Kiengsh yaani kuna lugha nyingi hata pia ukienda Uganda zipo.Lakini tatizo kuu ni kwamba sisi hatujui pahala pa kutumia lugha hii."

    Omar Marjan anazidi kueleza kwamba adui mkubwa wa lugha ya Kiswahili ni lugha zote mbili za Kiswahili na Kiingereza.

    "Kwa mimi ninavyoona sasa hivi ile mantiki ya kiingereza ndiyo adui mkubwa wa Kiswahili, kwa mfano, kwa nini mtu aseme, kujihami kwa jino na ukucha, eti kwa sababu anamaanisha armed to the tooth and nail.

    Kwa nini mtu aseme napelekea, mwingine akasema kwa mtandao mimi, na fulani na fulani ndio tuliofanya kazi fulani akakosolewa akaambia sema fulani na fulani na mimi, sababu ni ipi? Kwa sababu ya mantiki ya Kiingereza.Mwingine anasema kula uji kwa sababu Kiingereza kinasema eat porridge!

    Kwa hivyo hata tukilaumu Sheng pia tujue mantiki ya Kiingereza inaumiza Kiswahili kuliko hata Sheng yenyewe."

    Baada ya wengi kuuliza ni vipi lugha ya Kiswahili itaweza kunusuriwa kutoka kwa mtego wa Sheng na matatizo mengine yanayokikumba Kiswahili Omar Marjan amejibu hivi.

    "Tukijaaliwa pawe na taasisi inayohusisha wadau wengi wanaojua Kiswahili kama wanavyoitwa siku hizi, isije ikawa wasomi tu ndio wamekaa pahala wakajifanya kujua zaidi, na kutenga waswahili asilia sababu waswahili asilia wanamchango. Sababu lugha ni yao, huwezi kwa mfano ukajitungia maneno ya Kiingereza bila kufikiria asili ya kiingereza."

    Kama Omar Marjan Hassan Morowa ambaye ni mshairi anayesifika nchini Kenya, anasema wanaoandika vitabu vya lugha hususan Kiswahili, wanasahahu kwamba ngeli ilikuja baada ya lugha yenyewe, kwa hivyo kuainisha ngeli hakupaswi kuboronga Kiswahili kile asilia.

    "Hivi karibuni kumekuwa na mjadala mkuu kuhusu neno kiu. Ngeli, wanasema iwe kiu cha. Ambao sio kweli. Kiu ni kiu ya na katika lahaja zote kama ni kumi na tano ama ni ishirini, mpaka chimwiini ukitafuta hakuna mswahili yeyote anayesema kiu cha ni kiu ya, yaani kiu ya maji."

    Fred Muoka ni mwalimu mkuu wa shule hapa nchini Kenya na anasema anaamini, suluhu ya tatizo linalozikumba la lugha za Kiswahili na Kiingereza lipo.

    "Suluhisho ipo, ya kwamba tunaweza tunaweza kujaribu kama waalimu katika shule za msingi, kuanzia hapo wanafunzi wanatiliwa mkazo watumie lugha zinazofaa na hii lugha ya sheng iweze kutolewa kabisa katika shule. Kama wanafunzi wanafaa kuongea Kiswahili waongee Kiswahili pekee.Kama ni Kiingereza waongee Kiingereza pekee.

    Kwa hivyo walimu wanafaa kuchukua jukumu la kuhakikisha kuwa wanafunzi wanazungumza lugha sahihi."

    Lakini Eunice Wanjiku Ng'ethe ana maoni tofauti kuhusu suluhu ya tatizo hilo akisema adhabu pekee haitoshi.

    "Kuna viranja wa lugha ambao huripoti visa vya matumizi ya lugha kama sheng shuleni lakini hilo haliwezi kuwa suluhu ya kudumu."

    Vyombo kadha vya habari  nchini Kenya upeperusha matangazo kwa lugha hii ya Sheng na kwa wengi lugha hii huenda ikajikita na kuwa moja wapo ya lugha za humu nchini.

     

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako