• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Tabia ya watalii wa China

    (GMT+08:00) 2014-03-28 15:32:50

    Kwa muda wa siku kadhaa sasa wimbi kubwa la watu hapa China, lilikuwa kwenye mapumziko ya sikukuu ya mwaka mpya wa jadi, wengine walikuwa makwao, na wengine walikwenda kutalii sehemu mbalimbali za China, na wengine nje ya China. Leo katika kipindi hiki tunawafahamisha kuhusu mwenendo wa kutalii wa wachina.

    Pili: Tukianza kuangalia takwimu za mwaka jana, inaonesha kuwa watalii karibu milioni 100 kutoka China walikwenda nchi za nje. Idadi hii ni ongezeko la watalii milioni 14, kuliko mwaka 2012. Inawezekana mwaka huu wa 2014 huenda idadi hiyo pia itaongezeka na kuwa kubwa zaidi. Idadi ya wachina wanaosafiri kwenda katika nchi nyingine ni kubwa zaidi kuliko watu wa nchi nyingine duniani wanaokwenda kutalii nje ya nchi zao.

    Fadhili: Bila shaka ukubwa wa nchi na idadi kubwa ya watu, vinaifanya China iwe ni nchi yenye kupokea watalii wengi sana. Lakini tunalotakiwa kukumbuka ni kuwa, mbali na idadi, hata kiasi cha pesa walizotumia wachina katika mambo ya utalii ni nyingi zaidi kuliko walizotumia wajerumani au wamarekani. Mwaka jana wachina walitumia jumla ya dola za kimarekani bilioni 102 kwa ajili ya utalii. Hizi kwa kweli ni pesa nyingi sana.

    Pili: takwimu hizo basi zinaweza kutusaidia kueleza vizuri tabia au mwenendo wa wachina kuhusu utalii. Kwanza ikilinganishwa na watalii wengine duniani, wachina wanaonekana kuwa ni watu wanaotumia pesa nyingi sana kwenye mambo ya utalii. Hata tukisikiliza maoni ya watu wanaopokea watalii unaweza kuthibitisha kuwa, ikilinganishwa na watalii wengine, watalii wachina wanatumia sana pesa nyingi kwenye utalii.

    Pili: Kwanza Bwana Muema anayeuza vinyago mjini Nairobi anasema watalii wachina wanatumia pesa nyingi kununua vitu. Na haya si maoni ya Bw Mutuma peke yake, mtafiti mmoja kuhusu mambo ya utalii hapa China anasema mjini London maduka makubwa yanaongeza idadi ya wafanyakazi wanaoweza kuongea kichina, na kuna vitu vingi vya kuwasaidia wachina kulipia vitu wanavyonunua Uingereza. Na kuna baadhi ya watu hata huwa wanasema wachina ni kama "wallet inayotembea" kwani wanapokwenda kutalii ni kama wanakwenda kutafuta njia ya kutumia pesa zao, wao wanapotalii wanajitahidi kununua karibu kila kitu wanachopenda.

    Fadhili: Lakini tunatakiwa tukumbuke kuwa wachina wana changamoto sana wanapokwenda kutalii nje ya China. Changamoto kubwa kabisa ya kwanza ni lugha, na ya pili ni utamaduni. Ni bahati mbaya sana kuwa watu wengi wamezoea watalii wanaoongea Kiingereza au kifaransa, na wanajua utamaduni wa watu wa nchi hizo. Lakini wachina wana utamaduni tofauti sana kiasi kwamba baadhi ya watu wanaona watalii wachina ni wa ajabu kidogo. Matokeo yake ni kuwa kunakuwa na tatizo la mawasiliano na kutoelewa kwa mara kwa mara, kama anavyoeleza Bw Otieno Ahmed

    Pili: Baadhi ya watu wanalalamika kuwa ukija China, wachina wanakupa chakula chao, lakini wao wakija Afrika hawataki chakula cha waafrika, ila wanataka kula chakula cha kichina. Hii kweli ni desturi tofauti ya kutalii, Na nyingine kutokana na wachina kushindwa kujichanganya na watu wengine, hasa kutokana na lugha na kutojua utamaduni wa wenyeji, wenyeji wanakuwa na hisia kuwa wachina ni wabaguzi. Lakini ukweli ni kwamba si kama wachina ni wabaguzi. Ni kutokana na kutojua utamaduni wa wenyeji na hata lugha za wenyeji. Matokeo yake ni kuwa wanakuwa katika vikundi vikundi, na wengi hawawezi kutalii mmoja mmoja kama watalii wengine wa Ulaya au hata wajapan.

    Fadhili: Lakini kuna lingine ambalo naweza kusema kwa kiasi fulani linashangaza kuhusu watalii wachina kama alivyosema Bw Otieno, wachina wanapokwenda kununua vitu mara nyingi huwa wanakuwa makini na vitu wanavyonunua. Sio kama tu bora wanunue, wananunua vitu ambavyo wanapenda kuona vina ubora, sio vitu feki. Hebu tumsikilize Bw Erastus Munyao

    Pili: Naona si jambo baya kununua kitu halafu kuhakikisha kuwa kila kina ubora unaotakiwa. Ukweli ni kwamba hata sisi tunapokwenda madukani huwa tunafanya hiyo, sio bora kununua, tunakuwa makini sana.

    Fadhili: Kuna baadhi ya mambo ambayo mara nyingi huwa yanatajwa kuhusu watalii wa China. Kuna wale ambao baadhi ya wakati hawaheshimu taratibu za usafi au kufuata utaratibu kwenye maeneo ya utalii. Baadhi ya watu wanasema kuwa wachina wakinywa maji wanatupa taka ovyo, wengine wanasema wachina hata hawafuati mistari huwa wanapenda kusukumana. Pili sisi tunaishi na wachina hapa kila siku labda wewe unaweza kuwaeleza wasikilizaji.

    Pili: Kwanza ni vizuri tukifahamu kuwa kwenye baadhi ya miji serikali zinatumia pesa nyingi kuhakikisha miji inakuwa safi. Kwa mfano, hapa Beijing kuna watu wanapita kwenye kila barabara na vipikipiki au baiskeli kuokota karatasi, chupa, au hata takataka ndogo ndogo. Kwa hiyo hata kama wakitupa taka mjini haiwi michafu, tofauti na kwenye miji au nchi nyingine. Lakini kuna lingine ambalo ni gumu zaidi, kutokana na kuishi mazingira yenye idadi kubwa ya watu, kuchelewa chelewa hapa China kunaweza kukufanya uchelewe kweli. Kwa hiyo hali hiyo naweza kusema inatokana na uwingi wa watu. Hata wageni wanaokuja hapa China kwa wakati fulani nao wanatakiwa kuchangamka.

    Fadhili: Hata hivyo serikali ya China imepitisha sheria ili kuwahimiza wachina kufuata baadhi ya mambo ambayo yanalinda sura ya China na wachina nje ya nchi. Kuna mfano wa tukio moja lililowakasirisha wachina wengi, pale kijana mmoja alichonga maneno kwenye mapiramidi kule Misri aliiandika "Ding Jinhao alikuwa hapa", wengi walijadili suala hilo vikali kwenye internet, na kumlaani kijana huyo. Kwa hiyo wachina kila wanapokwenda kutalii wanaelekezwa kufuata maadili, sheria na taratibu za sehemu wanazokwenda kutembelea.

    Pili: Lakini mengine pia yanaleta wasiwasi. Kwa mfano hapa China kuna hali nzuri ya usalama, kwa hiyo watu wanaweza kutembea wakiwa na simu, vidani na vitu vingine vya thamani bila wasiwasi. Lakini nje ya China hali haiko hivyo. Katika baadhi ya nchi ambazo watalii wa China wanakwenda, kuna wakati wanajisahau na kudhani kuwa wako China matokeo yake ni kuwa wengine wanavamiwa na kuporwa, au wengine wanatibiwa na vibaka.

    Fadhili: Kufikia hapa ndio kwa leo nakamilisha kipindi hiki cha China Machoni Mwetu, mimi ni Fadhili Mpunji kwa niaba ya mwenzangu Pili Mwinyi, hadi alhamisi ijayo…zai jian

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako