• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Elimu ya juu inayotafutwa nje ya nchi

    (GMT+08:00) 2014-04-11 14:59:43

    Hujambo msikilizaji na karibu katika kipindi cha China Machoni Mwetu mimi ni Fadhili Mpunji niko na mwenzangu Jacob Mogoa. Leo kwenye kipindi hiki tunazungumzia maswala ya elimu, hasa elimu ya juu inayotafutwa nje ya nchi. Kama ilivyo kwenye nchi zetu za Afrika, hapa China kuna baadhi ya wanafunzi baada ya kuhitimu elimu ya sekondari, au shahada ya kwanza wanapenda kwenye kusoma nje ya nchi. Kuwa nasi tukufahamishe.

    Jacob: Wiki chache zilizopita mke wa rais wa Marekani Bibi Michelle Obama alifanya ziara nchini China. Mbali na kutalii, moja ya mambo muhimu aliyofanya ni kutangaza elimu ya Marekani na kuwahimiza wanafunzi wa China wanaopenda kwenda kusoma Marekani, waende marekani. Na ripoti moja iliyotolewa na shirika moja linalotumiwa kushughulikia mambo ya wanafunzi wanaokwenda kusoma nchi za nje inaonesha kuwa, kwa sasa China ni nchi yenye wanafunzi wengi zaidi wanaosoma nje ya nchi. Mwaka jana idadi hiyo ilifikia zaidi ya laki 4, ikiwa imeongezeka kwa 3.58 kuliko mwaka 2012, na wanafunzi laki 3.8 kati yao walijilipia ada wenyewe.

    Fadhili: Kwa ujumla wimbi la watu kutaka kwenda kusoma nje ya nchi hapa China lilianza mwaka 2007, na kuanzia mwaka huo, idadi ya wanafunzi wa China waliokuwa wanakwenda kusoma nchi za nje iliongezeka kwa zaidi ya asilimia 20. Kama ilivyo kwenye nchi zetu, kusoma katika nchi za nje kuna manufaa yake, kama mtu akiwa anajua lugha nyingine na utamaduni wa nchi nyingine, bila shaka wanaweza kuwa na uwezekano zaidi wa kupata ajira.

    Jacob: Lakini labda tuangalie kwa undani ni kwanini wanafunzi wa hapa China wanakwenda kusoma nje ya nchi? Tujiulize swali hili tukijaribu kulinganisha na mazingira ya Kenya au mazingira ya nchi nyingine za Afrika. Na tukifanya hivyo tunaweza kuona kuwa kwenye nchi zetu vyuo ni vichache, na hata kama tuna vyuo baadhi ya vyuo havina zana za kutosha au hata havina kozi ambazo watu wanahitaji kusoma. Kwa hiyo kwa upande fulani ni kuwa tunalazimika kwenda kusoma nje. Hapa China hali ni tofauti kiasi.

    Fadhili: Hapa China kwa ujumla naweza kusema vyuo ni vizuri, na hapa China huwezi kusikia tatizo la vitabu shuleni, au tatizo la walimu au majengo, kwa hiyo halo haliwezi kuwa sababu ya wanafunzi kwenda kusoma nje. Lakini tatizo ni kuwa vyuo vya hali ya juu hapa China ni vichache sana, na idadi ya wanafunzi ni kubwa, kwa hiyo ushindani ni mkali sana. Kwa hiyo hapa China naweza kusema wanafunzi hodari sana wanasoma hapa hapa China, hii ni tofauti na kule nyumbani ambako wale hodari sana ndio wanapata scholarships.

    Jacob: Pamoja na kuwa tunasema hapa China vyuo ni vizuri, kuna baadhi ya wazazi wana mawazo kama wazazi wetu kwenye nchi zetu za Afrika, wao wanaona kiwango cha elimu ya nchi za nje kama vile Marekani, Canada, Uingereza, Australia ni cha juu zaidi kuliko China. Na mfumo wa elimu ni mzuri zaidi, wanafunzi wanaweza kujifunza mambo mengi na bila shinikizo kubwa wakiwa nchi za nje.

    Fadhili: Hapa China kwa kweli shule ni shinikizo kubwa, kwa hiyo wanaokwenda kusoma nje ya nchi kwa upande fulani naweza kusema wanakwepa shinikizo. Lakini vile vile kuna baadhi ya masomo ambayo ni vizuri zaidi kusomea nje kuliko hapa China. Ukiangalia takwimu unaweza kuona kuwa asilimia 58.99 ya wanafunzi waliokwenda kusoma nje, walichukua kozi ya uchumi na biashara, wengine walichukua kozi za sayansi na uhandisi na wengine mambo ya usanii. Kwa hiyo mengine wanaweza kusoma hapa hapa China kwa urahisi.

    Jacob: Lakini tukiangalia upande mwingine tunaweza kuona kuna hali ya kufanana kati ya China na nchi za Afrika kwenye nchi ambazo watu wanachagua kwenda kusoma nje. Bahati nzuri ni kuwa sisi waafrika tunaweza kuchagua kuja kusoma China, na tunasema nje ya nchi. Lakini nchi ambazo wachina wengine wanakwenda kusoma ni Marekani, ambako mwaka jana walikwenda wanafunzi laki 2, Uingereza wanafunzi elfu 62, Canada elfu 29.

    Fadhili: Lakini kumekuwa na matatizo kwenye kutaka kusoma nje, kwa mfani kwa sasa hapa China watoto wadogo wameanza kwenda nchi za nje kusoma, na idadi ya wanafunzi wa shahada ya pili imeanza kupungua, lakini idadi ya wanafunzi wa sekondari inaongezeka. Kwenye maonyesho ya kimataifa ya elimu ya China ya mwaka 2014, shule moja ya Uingereza iliotangaza kuwa inaweza kupokea watoto wenye umri wa miaka miwili au mitatu, wanakaa shuleni bila wazazi. Baadhi ya wazazi wanaona kuwa watoto wakienda nchi za nje mapema, wanakuwa nguvu zaidi ya ushindani kuingia chuo kikuu, lakini wengine wanaona kuwa hili si jambo zuri.

    Jacob: Unajua malezi sio shule tu, kuna mambo mengi zaidi ya shule. Hata wataalamu wanaona kuwa, mtoto mwenye umri wa miaka 15 hadi 18 akienda nchi za nje kusoma, anaweza kubadilika sana kitabia na kimaadili. Na zaidi ya hapo watoto wanahitaji sana upendo wa wazazi zaidi, sio elimu tu.

    Fadhili: Lakini vilevile kumekuwa na matatizo mbalimbali yanayowakumba wale wanarudi China na kuanza kutafuta kazi. Zamani wachina wengine waliokuwa wanasoma nje ya China walikuwa wanapenda kutafuta kazi nje, walikuwa hawarudi. Lakini takwimu zinaonyesha kuwa, mwaka 2000 wanafunzi chini ya elfu 10 walirudi nchini China, lakini mwaka jana idadi hiyo imefikia laki 3.5.

    Jacob: Kwa upande mmoja, inawezekana kuwa uchumi wa nchi nyingine uko kwenye hatihati, na nchi hizo zinakabiliwa na tatizo la ukosefu wa ajira. Wenyeji wanashindwa kupata ajira, kwa hiyo wageni inakuwa vigumu zaidi kwao kupata ajira. Lakini kwa upande mwingine, serikali ya China nayo inajitahidi kuweka mazingira mazuri sana kwa wahitimu kutoka nchi za nje.

    Fadhili: Tunaweza kuangalia mfano wa Dt. Liu Ying alirudi China mwaka 2013, sasa anafanya kazi katika taasisi ya utafiti wa udaktari katika chuo kikuu cha Beijing. Yeye anasema, uwezo wa China wa utafiti wa sayansi umepata maendeleo makubwa, vilevile serikali na chuo kikuu wanatenga fedha nyini zaidi kwa ajili ya utafiti huo kuliko Marekani, kwa hiyo alivutiwa kurudi nyumbani.

    "Nilisoma nchini Marekani kwa miaka 7 na nusu, sasa nimerudi, naona kiwango cha utafiti wa sayansi cha China, muungaji mkono wa kifedha kutoka nchi na chuo kikuu, ni nzuri kuliko Marekani. Fedha nilizopata kwa ajili ya utafiti wa sayansi ni mara 1.5 hadi 2 kuliko Marekani inayoweza kutoa."

    Jacob: Kwa hiyo tunaweza kusema kwa sasa mazingira hapa China yanaendelea kuboreshwa, kwa hiyo wengi watachagua kusoma au hata kufanya kazi hapa hapa China.

    Fadhili: Kufikia hapa ndio kwa leo tunakamilisha kipindi hiki cha China Machoni mwetu, mimi ni Fadhili Mpunji kwa niaba ya mwenzangu Jabob Mogoa, hadi alhamisi ijayo, kwaheri.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako