• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Tatizo la msongamano wa magari na maegesho hapa China

    (GMT+08:00) 2014-06-15 18:43:42

    Leo katika kipindi hiki tunazungumzia tatizo la msongamano wa magari kwenye miji mikubwa hapa China, na hasa tatizo la maegesho, kwa sasa baadhi ya watu hapa China, hasa wa mijini huwa wanajiuliza kuhusu kununua magari kutokana na tatizo la msongamano wa magari na maegesho.

    Pili: Wakazi wa Nairobi na Dar es salaam, watakuwa wanafahamu vizuri sana maana ya msongamano wa magari barabarani, lakini nako pia nadhani tatizo la watu kuhangaika kuhusu sehemu za kuegesha magari hasa katikati ya miji limeanza kuwa kubwa. Hapa China kwa sasa naweza kusema msongamano wa magari barabarani umefikia hatua kubwa sana. Kwa sasa sio katikati ya mji tu, hata kwenye barabara za nje kidogo ya miji kuna tatizo la msongamano.

    Fadhili: Umetaja miji ya Nairobi na Dar es salaam. Tukilinganisha miji hiyo na miji ya hapa China naweza kusema ni miji midogo. Mji wa Dar es salaam kwa mfano una wakazi wapatao milioni karibu tano, kwa hapa China huo ungeitwa mji mdogo, haujafikia hata mji wa kati. Mji wa Beijing kwa mfano una wakazi zaidi ya milioni 20, na ukianglia idadi ya magari ya mji huu ambao hata kwa eneo ni mkubwa karibu hata mara 5 ya dare salaam unaweza kuona ni magari mengi sana, kwa hiyo hapa Beijing tukisema msongamano wa magari basi ni msongamano mkubwa sana. Hasa ukizingatia kuwa barabara ni kubwa Dar es salaam.

    Pili: Lakini kuna baadhi ya mambo ambayo naweza kusema tunaweza kujifunza kwa urahisi kutoka hapa China, ambako wenzetu wamekabiliwa na changamoto hii kwa muda mrefu kiasi. La kwanza ni kuufanya usafiri wa umma uwe mzuri. Hapa Beijing na kwenye miji mingine mikubwa ya hapa China kuna subway, labda hiyo hatuwezi kuizungumzia kwa kuwa kwenye nchi zetu hakuna. Lakini mabasi hapa China yanasimamiwa na kuendeshwa vizuri. Hata kama barabarani kuna msongamano kiasi gani, mabasi yanapita kwa urahisi, kwa kuwa yana njia zake maalumu.

    Fadhili: Kwa sasa mjini Dar es salaam kwa mfano kuna ujenzi wa barabara kwa ajili ya mabasi yanayoenda kwa kasi. Hapa Beijing kuna barabara za namna hiyo, lakini hata hizi barabara za kawaida, kuna mistari imechorwa na kuna maandishi barabarani yanayoonesha kuwa kuanzia saa 10 na nusu hadi saa 3 na nusu usiku, njia hizo zinatumiwa na mabasi tu, kwa hiyo magari mengine hayaruhusiwi kupita. Kwa hiyo hata kama kuna msongamano kiasi gani, ukipanda basi unaweza kusafiri kwa haraka kuliko ukiwa kwenye gari binafsi.

    Pili: Lakini kuna jambo moja ambalo naweza kusema ni tatizo hapa China, pamoja na kuwa usafiri wa umma umepangwa vizuri, kuna wakati kunakuwa na msongamano mkubwa sana kwenye mabasi kiasi kwamba hata kusogeza mguu inakuwa taabu. Pamoja na taabu hiyo, ukiwa kwenye basi huna hofu ya kukaa barabarani kwa muda mrefu kama inavyokuwa ukiwa kwenye daladala au kwenye matatu.

    Fadhili: Tukiangalia swala la maegesho naweza kusema kuna mengi ya kujifunza kutoka kwa wenzetu hapa China. Kwanza mara nyingi nimekuwa Nikiangalia majengo marefu na makubwa hapa China, kuna baadhi yanakuwa na ghorofa tatu au hata nne chini ya ardhi. Na huku kunakuwa na maegesho ya magari au hata baiskeli. Hali hii bao kuonekana kwenye nchi zetu

    Pili: Kwenye nchi zetu kwanza naweza kusema hili ni tatizo jipya, hata majengo ambayo yapo mengi ni ya zamani, hayakujengwa wakati kuna tatizo la maegesho. Wakati majengo mengi yanajengwa idadi ya magari ilikuwa ndogo sana, lakini sasa idadi ya magari imeongezeka na kuwa kubwa. Lakini majengo yanayojengwa siku hizi yameanza kuwa na sehemu hizo ingawa bado ni machache.

    Fadhili: Kwa wenzetu hapa China suala la maegesho ya magari limefanywa kuwa ni fursa ya kibiashara, kwa sasa watu hawalalamiki kukosa sehemu ya kuegesha magari, ila wanalalamika kuhusu gharama za kuegesha magari. Na sehemu za kuegesha magari zinakuwa nzuri zina ulinzi na zimepangika vizuri.

    Pili: Lakini hata ukiangalia barabara za wenzetu, hasa barabara zilizopo kwenye maeneo ya makazi ya watu, zina maeneo maalum ya maegesho. Barabara ni pana kiasi kwamba katika pande mbili za barabara kunakuwa na sehemu zimewekwa alama kuwa ni za maegesho ya magari ya watu wanaishi maeneo hayo. Kule nyumbani mara nyingi tumezoea kuona kuna mtu anakuja kufunga mnyororo kwenye tairi, kama umeegesha kwenye maeneo ambayo wenzetu wanaegesha kwa urahisi tu.

    Fadhili: Lakini hili la kuweka mnyororo naweza kusema ni jambo la ajabu kidogo, hapa China ninachoona ni kuwa wenzetu wanaweka tiketi kwenye kioo cha gari na kukwambia kutokana na kuegesha sehemu ambayo hukutakiwa, unatakiwa uende mahali fulani kulipia. Na kama hukulipia basi utasubiriwa siku ya kwenda kulipia leseni, au gari lako likifika kunakohusika kwa sababu yoyote ile. Naweza kusema wenzetu wana njia ya kistaarabu zaidi kukabiliana na maswala kama hayo.

    Pili: Kuna mengine ambayo tunaweza kujifunza kwa wenzetu. Mara nyingi hapa Beijing unaweza kuona mtu ana gari, pikipiki au baiskeli. Lakini anachofanya ni kuwa anaendesha hadi pale anapofika kwenye usafiri wa umma, anaegesha karibu na kituo halafu anapanda basi au subway kwenda kazini, na baada ya kazi akitoka tu anatumia usafiri wa umma hadi kituoni, halafu baadaye anatumia gari yake, pikipiki au baiskeli. Hali hii naweza kusema bado haijaanza kuonekana kwenye nchi zetu.

    Fadhili: Sasa hivi hapa China pia wenzetu wanaanza kuvuka ile hatua ya magari kuwa kitu cha ufahari, Kuna wengine wanaacha magari yao nyumbani wanatumia usafiri ambao kule nyumbani watu wanaweza kuona ni wa kiwango cha chini. Unaweza kuona matajiri badala ya kutumia magari ya kifahari wanatumia baiskeli au pikipiki. Hii pia inapungumza msongamano wa magari, na hata inapunguza tatizo la msongamano wa maegesho ya magari.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako