• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Uzoefu kiasi kuhusu kuishi na wachina

    (GMT+08:00) 2014-06-19 16:45:40

    Kwa mara kadhaa sasa watu kutoka Tanzania au katika sehemu nyingine za Afrika wakija hapa Beijing kama ni mara yao ya kwanza kufika hapa China, swali wanaloniuliza ni kama hapa China kuna ubaguzi wa rangi. Huwa wanataka kujua kama wachina wabagua waafrika au wageni kwa jumla. Mimi Fadhili Mpunji na mwenzangu Pili Mwinyi tumeishi hapa China kwa muda sasa, kwa hiyo tuna uzoefu kiasi kuhusu kuishi na wachina.

    Pili: Kweli hili swali huwa linaulizwa mara nyingine na wageni ambo wanatembelea China kwa muda. Lakini ukweli kuhusu jambo hili nadhani liko kwenye maadili ya wachina. Kwa ufupi naweza kusema wachina hawawabagui watu kutokana na mwonekano wao. Kuna baadhi ya wakati watu wanaweza kuwa wanakushangaa kutokana na jinsi unavyoonekana hasa kama ukienda vijijini. Kwa mijini ambako kuna watu wa rangi mbalimbali, hali ni kawaida huwezi kusema kuna ubaguzi.

    Fadhili: Lakini vile vile kuna mengine ya kuangalia kuhusu fikra potofu hasa tunayokuwa nayo sisi waafrika tunapokuja hapa China. Kwanza wachina ni watu ambao wanapenda faragha sana, Hii ni kutokana utamaduni wao, mara nyingi wachina wanajizuia kusema na wanalinda sana sura yao, wanapenda kulinda heshima yao. Kwa hiyo hata wakati wa kuongea unaweza kuona kuwa wanachagua maneno ya kuongea, hawaongei ovyo, na kama hawana la kuongea basi wanachagua kukaa kimya, au wanaepuka kuongea. Kwa mtu ambaye ndio anafika mara ya kwanza hapa China anaweza kutafsiri hali hii vibaya.

    Pili: Hali hii si kama wanaifanya kwa wageni tu, hata kwa wao kwa wao wachina. Wakati mwingine hata ndani ya familia, kwanza kutokana na maadili ya jadi ya wachina mbele ya mgeni unatakiwa uoneshe sura nzuri na kumwachia mgeni picha nzuri kuhusu maadili yako. Hata mbele ya mtu mzima unatakiwa kuonesha unyeyekevu sio ukaidi au tabia za ajabu. Lakini ukiangalia kwa sisi wageni kuna wakati unaweza kuona kuwa hali ni tofauti, wakati mwingine unaweza kuona mtu anaongea tu bora kuongea na bila hata kujua maana au matokeo ya kile anachoongea.

    Fadhili: Lakini vile vile kuna baadhi ya mambo ambayo huwa tunayaona kwa wageni hapa China. Unajua wenzetu wachina wana mila na desturi zinazoongoza mahusiano ya watu. Kwa mfano ni nadra sana kuona wachina hata wanasalimiana kwa mikono, wakiona wanasema tu ni hao, labda iwe ni katika hali rasmi ndio wanasalimiana. Bahati mbaya wageni wengine wanakuja kutoka kwao huko wamezoea kukumbatiana wanaaza kusumbua wenyeji hapa China, kwa hiyo wengine wanajaribu kujiweka pembeni.

    Pili: Hili ni kweli unajua kwa sisi tuliozoea kuishi na wachina naweza kusema wachina ni watu rahisi sana kuishi nao, na wala hawana ubaguzi. Lakini kwanza unatakiwa ujue utamaduni wao, na uwe ni mtu unayejiheshimu na kufanya mambo yasiyoendana na maadili yao. Kama ukifanya hivyo inakuwa rahisi sana kuishi na wachina, sio hapa China tu, hata sehemu nyingine nje ya China

    Fadhili: Kuna jambo moja ambalo mara nyingi mimi huwa naliona hasa kutoka kwa vijana wa Afrika wanaokuja hapa China. Kwanza kutokana na kutojifunza jambo moja au mawili kuhusu utamaduni wa China, wao wanakuwa na tabia kama vile wako nyumbani, lakini hawajui kuwa baadhi ya mambo ambayo ni kawaida kufanya kule nyumbani kwa wachina si kawaida. Kuna siku tulimwalika kwenye kipindi hiki mwanafunzi mmoja mtanzania kutoka mikoa ya kusini mwa China. Yeye mpaka alikasirika alisema kila mara watazania wenzake wanapomuuliza kuhusu China wanasema wanataka kupata wachumba wachina, mpaka akauliza hhivi hakuna kitu kingine cha kuuliza kuhusu China? Hata kama wasichana wa China ni warembo sio kila mara kufikiria wasichana tu. Sasa ukionekana una akili kama hizo watu wanaona huna maana.

    Pili: Vilevile kuna jambo moja ambalo baadhi ya rafiki zetu wachina huwa wanazungumza. Unajua wachina mara nyingi ni watu wanaopenda faragha, hata kama wanaongea huwa hawaongei kwa kupayuka, wanaongea taratibu. Ukiingia kwa mfano madukani unaweza kusikia kelel kiasi, lakini si kelele kubwa za kukufanya mtu ughadhabike, au ukiwa ofisi wakati mwingine hata mawasiliano kati ya wafanyakazi kwenye ofisi moja yanakuwa kama ni kunong'onezana na sio mpaka mtu mwingine asikie.

    Fadhili: baadhi ya watu wakiona wewe unaongea kwa sauti na kupayuka wanaweza kukukwepa, kwa hiyo kama hujui vizuri utadumi wa wachina, unaweza kusema ni kutokana na rangi ya ngozi yako. Lakini ukweli ni tabia tu ya mtu na sio rangi yake. Mimi nawafahamu watanzania na waafrika kadhaa ambao wameoa wachina na wanaishi nao kwa furaha, na siku hizo pia kuna hata wachina wanaoa watanzania na waafrika kwa hiyo unaweza kuona kuwa suala hapa sio rangi ya ngozi ya mtu bali ni tabia ya mtu.

    Pili: tunatakiwa kujua vile vile kuwa China ni nchi ambayo inaendelea na mageuzi na kufungua mlango, kwa hiyo wageni katika baadhi ya maeneo hawajulikani. Kwa maeneo ambayo wageni kama sisi hatujafika, kuna wakati watu wanaweza kuwa wanashangaa, na wakati mwingine wanweza hata kuwa na woga fulani. Labda mfano ni kuwa hata msikilizaji ukisikia mtu wa kijani amekuja au ukikutana na mtu wa bluu, kwanza utakuwa na wasiwasi na utakuwa unajiuliza maswali mengi huyu mtu yukoje.

    Fadhili: Lakini vile vile kuna hali fulani ambayo naweza kusema kidogo inatokana na athari ya vyombo vya habari vya magharibi, ukiangalia jinsi filamu za Marekani za zamani zinavyomuonesha mtu mweusi, unaweza pia kuona kuwa baadhi ya watu wamekuwa na picha kama ya vyombo vya habari vya nchi za magharibi. Ni sawa na baadhi ya waafrika wanavyowaona wachina nyumbani, kwa hiyo ni picha ambayo sio halisi isipokuwa ni ili ilijengwa na vyombo vya habari vya habari.

    Pili: La muhimu la kukumbuka ni kuwa watu wanapokuja hapa China, wanatakiwa kujitahidi kujua kuwa wachina ni watu wenye utamaduni wa muda mrefu, kwa hiyo wanatakiwa kuwa makini na sio kukimbilia kulalamika kubaguliwa wakati wao wenyewe hawaangalii mambo wanayofanya.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako