• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Amri ya polisi inayowataka wakazi wa Lamu kutotoka nje usiku yaondolewa

    (GMT+08:00) 2014-07-23 08:53:54

    Waislamu katika kaunti ya Lamu nchini Kenya wameondolewa marufuku ya kutotoka nje usiku iliyotolewa na juzi na mkuu wa Polisi kufuatia hali ya ukosefu wa usalama.

    Taarifa iliyotolewa na Inspekta Mkuu wa polisi nchini Kenya Bw David Kimaiyo na kiongozi wa walio wengi bungeni Aden Duale ilisema kuwa mipango kabambe imewekwa ili kuhakikisha kwamba ratiba ya ramadhan na sala za usiku haitoathiriwa na amri hiyo ya kutotoka nje.

    Jumamosi, mkuu wa polisi alitoa amri ya kutotoka nje katika kaunti ya Lamu kuanzia saa 12.30 jioni hadi 12.30 asubuhi kufuatia matukio ya uvamizi ambayo yamepekea vifo vya watu wengi wakiwemo maofisa wa polisi katika maeneo mbalimbali kwenye kaunti hiyo.

    Amri hiyo ya kutotoka nje ilitolewa siku moja baada ya watu saba ,wakiwemo maafisa wanne wa polisi kuuawa na watu waliokuwa na silaha kali. Genge hilo la watu lilimiminia basi la abiria risasi usiku wa kuamkia jumamosi karibu na msitu wa Mambo sasa, katika eneo la Witu. Gari la polisi lililokuwa likikaribia eneo hilo pia lilimiminiwa risasi na kusababisha vifo vya watu sita.

    Baada ya tukio hilo, Mkuu wa polisi David Kimaiyo alitoa amri ya watu kutotoka nje, jambo ambalo lilipokelewa na hisia tofauti.

    Kiongozi wa walio wengi bungeni Aden Duale alipinga amri hiyo na kuwataka waislamu kuipuuza. Aidha wanasiasa wa Lamu pia waliipatia serikali saa 48 kubatilisha amri hiyo la sivyo waende mahakamani..

    Duale anadai kumsihi Kimaiyo kuwapatia waislamu usalama ili kuwawezesha kusali miskitini wakati wa kumi la mwisho la mwezi mtukufu wa Ramadhan.

    Kwenye taarifa yake, Duale alisema kuwa siku kumi za mwisho za Ramadhan ni siku muhimu katika maisha ya kila muislamu. Alisema hizo ndio siku zilizobarikiwa zaidi katika mwezi mtukufu wa Ramadhan kwa sababu ni katika mwezi huo ambapo Qur'an takatifu iliteremshwa.

    Zaidi ya wakazi 500 kutoka kisiwa cha Lamu juzi waliandamana kupinga marufuku hiyo ya kutotoka nje usiku.

    Siku moja baada ya kutolewa amri hiyo, waislamu wengi mjini Lamu walijitokeza kuipinga wakisema itaathiri sala zao za usiku.Baadhi ya watu walimiminika kutoka zaidi ya misikiti 35 walikusanyika katika uwanja wa Mkunguni wakitaka amri hiyo kufutwa.

    Viongozi wa kidini na Gavana wa kaunti ya Lamu Issa Timamy pia walielezea kukerwa kwao na amri hiyo ya kutotoka nje. Walisema jambo muhimu ni serikali kuwahakikishia wananchi usalama na sio kutoa amri ya kutotoka nje hasa wakati wa ibada katika mwezi mtukufu wa Ramadhan.

    "Watu wana haki ya kwenda kuabudu, hivyo tumekubaliana kuwa watu waende kuabudu. Hayo mambo mengine, Mungu akipenda tutakwenda Nairobi tukakae na hawa jamaa watuambie kwa nini wametuwekea amri hiyo,"alisema Bw Timamy.

    Kamishna wa kaunti ya Lamu Miiri Njenga amesema kamati maalum ya usalama wa kaunti itaundwa ili kushughulikia masuala yanayohusiana na dini.

    Wakati huo huo Afisa wa shirika la kutetea haki za binadamu la MUHURI Khelef Khalifa na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Haki Africa Hussein Khalid wamepinga amri hiyo wakisema inakiuka haki na uhuru wa kutembea na kufanya ibada.

    "Ni wazi kabisa kwamba wanafanya kazi kivyao bila kuzijumuisha jamii mashinani,"alisema BW Hussein Khalid.

    Watetezi wa haki za binadamu pia wametaka amri hiyo iondolewa ili waislamu waweze kuendelea na sala zao za maghrib na za usiku kama sehemu ya kalenda ya kiislamu.

    Watetezi hao wanaona amri hiyo itaathiri shughuli za wavuvi ambao huweka mitego yao ya samaki baada ya giza kuingia.

    Baada ya kikao cha wadau mbalimbali jana jioni, inspekta Mkuu wa polisi David Kimaiyo alilazimika kuondoa marufuku hiyo kwa wakaazi wa Lamu haswa waislamu.

    Hata hivyo usafiri wa usiku katika eneo la Lamu bado umepigwa marufuku.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako