• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Dini nchini China

    (GMT+08:00) 2014-07-23 10:22:49

    Mara nyingi watu kutoka nchi za Afrika wakija hapa China moja kati ya mambo wanayoniuliza, ni kuhusu dini hapa China. Baadhi ya watu kutokana na kutokuwa na uelewa mzuri kuhusu dini hapa China, huwa wanakuwa na maswali je, watu hawa wanaishi vipi, tabia zao zikoje kama hawafuati dini?

    Pili: Kwanza tatizo kubwa lililopo kuhusu uelewa wa dini nchini China kwa wenzetu wa Afrika Mashariki ni kuwa, wachina ni wapagani yaani hawaamini Mungu. Huu si ukweli, kuna wachina ambao wanajitaja kabisa kuwa ni wapagani, kuna wachina waumini wa dini ya kibuddha, kuna wachina waumini wa dini ya kidao, kuna waislamu, na kuna wakristo pia. Kwa hiyo wazo kuwa wachina hawana dini, ni wazo la jumla ambalo sio sahihi.

    Fadhili: Kilichopo vile vile ni kuwa idadi ya wakristo na waislamu hapa China ni ndogo sana ikilinganishwa na idadi ya waumini wa dini nyingine. Mara nyingi wageni wakristo na waislamu wakija hapa China jambo ambalo huwa wanashangaa ni kutuona makanisa au misikiti. Hapa Beijing kwa mfano kuna watu zaidi ya milioni 20 lakini kuna makanisa mawili tu, na misikiti hata haifiki mitatu. Lakini kuna baadhi ya nchi idadi ya watu wako ni chini ya milioni 10 lakini unaweza kusikia zina makanisa au misikiti zaidi ya 100, kwa hiyo wakija hapa China huwa wanajiuliza inakuwaje kuna misikiti na makanisa machache, tatizo ni kuwa wanasahau au hawajui kwamba, hapa China kuna waumini wengi wa dini ya kidao na dini ya kibuddha na kuna mahekalu kadhaa ya dini hizo hapa Beijing.

    Pili: Kuna jambo lingine ambalo tunatakiwa kukumbuka, mara nyingi tunapotembelea majumba ya kifalme na baadhi ya maeneo ya kihistoria hapa Beijing na sehemu nyingine za China, tunaweza kuona kuwa karibu kila mahali kuna sehemu fulani ya kufanyia maombi na kutoa sadaka, na kuna picha za Buddha. Hali hii inafanana kiasi na mtu unapokwenda mahali na unakuta ile sanamu ya bikira Maria, lakini hapa sio kwa dini ya kikristo ni dini ya kibuddha. Kwa hiyo kwenye utamaduni wa China unaweza kuona wazi kabisa suala la dini lipo, tofauti na watu kutoka kwenye nchi zetu ambao akilini dini ni ukristo na uislamu.

    Fadhili: Lakini pia kuna tofauti nyingine pili ambayo hata sisi tunaoishi hapa tuliiona mwanzoni wakati tunakuja. Ukiwa unaishi Tanzania, Kenya au nchi nyingine yoyote yenye waumini wengi wa dini za kikristo, inawezekana, kila ikifika ijumaa unaona watu wanamiminika misikitini, na kila ikifika jumamosi au jumapili watu wanamiminika makanisani, na ikifika wakati wa sikukuu za kidini unaona wazi kabisa kuwa ni sikukuu za kidini. Lakini hapa China hali hii haonekani sana, kwa sababu waumini wa dini ya kibuddha huwa hawana siku maalum ya kwenda kwenye hekalu kuabudu na hawana sikukuu kubwa ya Idd el fitri au Krismas.

    Pili: Fadhili wewe umetembelea mara kadhaa kwenye mahekalu ya dini ya kibuddha na ya kidao, labda unaweza kuwafahamisha vizuri wasikilizaji wetu, watu wanaofanya ibada kwenye mahekalu hayo wanafanyaje, na kuna tofauti gani na wakristo au waislamu.

    Fadhili: Kikubwa naweza kusema dini ya kidao ni dini ambayo inakuunganisha wewe binadamu na Mungu wako, sio dini ya mikusanyiko kama dini za kiislamu na kikristo, kwa hiyo watu wakienda hekaluni wanachofanya ni kupiga magoti mbele ya sanamu ya budha na kuomba Mungu lakini sio kwa mikusanyiko, wengine wanachoma udi ikiwa ni kama kutoa sadaka, na udi wananunua pale pale kwenye hekalu ikiwa ni kama njia ya kutoa mchango, au kama wakristo wanavyotoa sadaka kanisani. Na hakuna siku maalum ya kwenda hekaluni kama ilivyo kwa wakristo au waislamu.

    Pili: Lakini tuangalie maana ya dini na lengo lake kwa jamii, halafu tulinganishe hali ya hapa China na kwenye nchi zetu. Kwenye nchi zetu tunaamini kuwa mcha Mungu ni mtu mzuri, yaani kama watu wakifuata amri za Mungu basi jamii inakuwa tulivu na ina usalama na watu watakwenda kwa peponi. Na kama watu wasipomcha Mungu basi kutakuwa na matukio mengi ya uhalifu, taabu na mwishowe wenye dhambi watakwenda kuzimu.

    Fadhili: Hili ni swali muhimu sana, lakini ni juu ya wasikilizaji kuamua kutoa majibu. Tukiangalia hapa China ambako nyumba za ibada sio nyingi, au waumini wa dini sio wengi kama ilivyo kwenye nchi zetu, naweza kusema tunaona watu wana mienendo mizuri zaidi hapa China. Ukiangalia kwa ujumla unaweza kuona wachina hawatendi mambo yale ambayo jamii zetu zinayapinga kwa kutumia dini. Mara nyingi kwenye vipindi vyetu huwa tunasema hali ya usalama hapa Beijing ni nzuri, matatizo ya watoto wa mtaani au wale wanaozaliwa nje ya ndoa nia madogo kama hakuna, na magonjwa kama Ukimwi hapa China sio tatizo kubwa kama ilivyo kwenye nchi zetu. Kule nyumbani ambako tunasema kuna kumcha Mungu haya matatizo ndio makubwa zaidi.

    Pili: Kwa ufupi tunaweza kusema wenzetu mambo ya utamaduni yamekuwa na mchango mkubwa sana kwenye kufanya wawe na maadili mazuri. Ukiangalia dini ya kidao kwa sasa ndio inatajwa kuwa na waumini wengi, lakini sio dini peke yake hata utamaduni unaotokana na mafundisho ya Confucius yamewafanya wenzetu wachina wawe na maadili sana. Kwa ujumla tukiangalia yale ambayo sisi tunasema yanatakiwa kufundishwa na dini, kwenye jamii ya wachina unaweza kuona tayari yamejikita kwenye utamaduni wao.

    Fadhili: Kitu kingine ambacho tunaweza kuwafahamisha wasikilizaji wetu ni kuwa wenzetu wachina wamebahatika kuwa hawabanwi sana na dini kama tunavyobanwa kwenye baadhi ya nchi zetu za Afrika. Kuna baadhi ya watu kwenye nchi za Afrika unasikia kuwa hawawezi kuoa watu wa kabila lingine au dini nyingine, hapa China wenzetu wana makabila 56 lakini kikubwa wanachoangalia sio kabila la mtu, bali ni maadili na utamaduni, au naweza kusema wanaagalia zaidi thamani ya mtu, bila kujali yeye ni muumini wa dini ya kibuddha au wa dini ya kidao.

    Pili: Na uzuri ni kwamba wenzetu hata ukiwaona njiani, hasa kwenye miji mikubwa, huwezi hata kutofautisha huyu ni kabila gani au huyu ni dini gani, wengi wanafanana, isipokuwa makabila machache tu ambayo watu wake wana wajihi tofauti.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako