• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Moyo wa kuchapa kazi walio nao wachina

    (GMT+08:00) 2014-07-23 10:24:32
    Leo kwenye kipindi hiki tutazungumzia moyo wa kuchapa kazi walio nao wenzetu wachina. Mara nyingi kwenye kipindi hiki mimi na mwenzangu Pili Mwinyi tunawapa nafasi watanzania wenzetu watoe maoni yao kuhusu yale wanayoyaona hapa China

    Pili: Kama ulivyosema Fadhili sisi tunaishi hapa Beijing, na mara nyingi mambo tunayozungumzia kwenye kipindi hiki, mengi ni yale tunayoyaona hapa Beijing. Leo tuko na vijana wawili kutoka Tanzania, wao ni wanafunzi wanaosoma na kuishi mjini Guangzhou, huko kusini mwa China. Wao wameishi huko kwa miaka mitatu, na sasa wamezoea maisha ya hapa, lakini zuri zaidi ni kuwa mbali na masomo pia wanajifunza mambo mbalimbali huko wanakoishi.

    Fadhili: Nyumbani tuna msemo mmoja "tembea uone", na kuona sio kuona tu, unaona na kijifunza ili wenzako wananufaika na kile ulichokiona wewe. Unajua tukiangalia idadi ya watu karibu milioni 45 wa Tanzania wanaotembea na kuona labda ni asilimia 2 au tatu, wengine hawana fursa ya kutembelea sehemu za mbali kama China.

    Pili: Ni kweli hebu sasa tuwasikilize vijana hawa, mmoja ni Ramadhani Kairo na mwingine Juma Mussa. Kwanza kabisa Ramadhani anaeleza maoni yake kuhusu wachina, kama akiuluzwa kutoa picha ya jumla kuhusu wachina maoni ya ni nini?.

    Fadhili: Pili sisi tumekuwa tunawaambia wasikilizaji wetu mara nyingi kuhusu jinsi wachina wanavyofanya kazi, na tumemsikia Bw Ramadhani anaunga mkono hilo. Lakini mara nyingi huwa najiuliza hivi sisi watanzania tunaokuja hapa China na kuona wachina wanavyofanya kazi, au kwenda katika nchi nyingine na kuona wenzetu wanafanya kazi, huwa tunajifunza nini? Hivi tukirudi nyumbani na sisi huwa tunabadilika, au ndio ukiona kitu fulani nje basi kinaishia huko huko nje.

    Pili: Swali hili ni gumu, lakini ninachoweza kusema ni kuwa watanzania wengine wakija hapa China, wanachosema ni kuwa wenzetu wanafanya kazi sana, lakini tatizo ni kuwa ukirudi nyumbani utamaduni kidogo ni tofauti. Wewe unaweza kuwa una moyo wa kuchapa kazi, lakini wale unaoshirikiana nao wanakuwa na matatizo. Kwa hiyo sio jambo la mtu mmoja. Bw Juma Musa ambaye pia ni mwanafunzi huko Guangzhou, yeye pia ana maoni kama ya bwa Ramadhani..

    Pili: Tumemsikia Juma amesema kwanza wanapenda kazi, pia wanaheshimu muda, na tatu ni wa kweli, akisema nitamaliza kazi muda fulani au nitakuletea kitu fulani muda fulani basi ni kweli. Kama hakufanya hivyo basi atakueleza mapema na atakupa sababu inayoeleweka, na sio kuleta porojo kama ilivyozoeleka kwa baadhi ya watu kule nyumbani.

    Fadhili: Hili kweli ni tatizo ambalo mpaka sasa mimi huwa najiuliza ni kwanini tuna tatizo kama hili, jibu siwezi kupata. Labda wasikilizaji wetu wanaweza kutoa maoni yao. Kwa mfano, kuna baadhi ya mambo tunashindwa kufanya kwa kuwa hatuna teknolojia, kuna mengine tunashindwa kufanya kwa kuwa hatuna pesa, lakini suala la kumaliza kufanya kazi kwa makini, kuheshimu wakati na kutimiza ahadi, haya hayana uhusiano na pesa, hayana uhusiano na teknolojia na hayana uhusiano na sayansi ya aina yoyote. Tumsikilize tena Bw Ramadhani akitoa maoni yake kuhusiana na hili

    Pili: Ramadhani anasema ni utamaduni, kwa hiyo hata kama mtanzania au Mkenya akija kwenye mazingira kama haya akaona jinsi wenzetu wanavyoheshimu muda, wanavyofanya kazi na kutimiza ahadi, si rahisi kama akaiga kwa siku mbili tu. Inatakiwa kukua katika mazingira kama hayo tangu akiwa mtoto,.

    Fadhili: Tukiachana na suala la kuheshimu kazi, kuheshimu muda na kuheshimu ahadi, kuna suala la chakula. Watu wengi wanaokuja hapa China huwa wanakuwa na wasiwasi kuhusu vyakula watakavyokula. Na bahati mbaya ni kuwa watu wanasema wachina wanakula vitu vingi sana, hasa huko kusini kwenye mkoa wa Guangdong. Ramadhani Kairo anatueleza uzoefu wake kuhusu chakula.

    Pili: Nadhani Ramadhani ameeleza vizuri, kwamba hapa China kama sehemu nyingine duniani, ukitaka kula chochote kile unaweza kukipata. Kuna vyakula vingi tu kama tunavyokula nyumbani, na vingine vizuri tu ambavyo kule nyumbani hatuvijui. Lakini ni kweli kuna watu wanakula vyakula vya ajabu, hasa kwenye sehemu ya kusini mwa China. Hata wachina wengine nao wanawashangaa watu hao. Kwa hiyo kama msikilizaji ukibahatika kuja hapa China, hili si suala la kuwa na hofu.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako