• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mchango wa harusi

    (GMT+08:00) 2014-07-23 10:33:35

    Hujambo msikilizaji na karibu katika kipindi cha China Machoni Mwetu. Kwenye moja kati ya vipindi vyetu vya huko nyuma tuliwahi kuzungumzia suala la harusi, na mila zinazohusu harusi. Leo tutazungumzia tena suala hilo, lakini kwa mtazamo tofauti kidogo.

    Pili: Nyumbani Tanzania au na sehemu nyingine za Afrika tumezoea kuwa wenzetu wanapojiandaa kufunga ndoa, huwa tunasaidiana kwa kuchangia pesa kiasi, tunaita mchango wa harusi. Kwa sasa imefikia kiasi kwamba, utaratibu huu umekuwa kawaida na kwa kiasi fulani naweza kusema suala la vikao vya harusi na michango ya harusi imekuwa ya kawaida.

    Fadhili: Lakini siku hizi pia kumeanza kuwa na maswali kuhusu michango hii ya harusi. Imeanza kuonekana kuwa baadhi ya watu wanalazimisha watu kutoa michango, japokuwa hawasemi moja kwa moja, ila unaweza kusikia kuwa ukitoa shilingi elfu 5 hualikwi kwenye Reception, ukitoa elfu 50 utaalikwa. Na wengine wanaonekana wanajali sana kutoa michango ya harusi, lakini kama mtu anaumwa au kama mtoto anahitaji karo ya shule, ukiomba msaada au hata ukijaribu kukusanya michango ya kumsomesha mtoto ambaye unaona ana mwelekeo mzuri wa shule hakuna mtu anayejali.

    Pili: Hapa China suala la harusi kwa upande fulani inaweza kusema lina linalingana sana na kwetu Afrika. Kuna mambo mengi yanayohusiana na harusi yanayoendeshwa kwa mtindo wa jadi. Kwa mfano maandalizi ya harusi na changamoto zake zinazohusiana na michango kwa kiasi fulani zinafanana na sisi waafrika. Lakini wenzetu hapa China, walio wengi hawana ule utamaduni unaohusu dini kuhusu harusi, kama vile kumhusisha shehe au mchungaji. Ni wachache sana wanaofuata utamaduni huo. Lakini kuna utamaduni wa kuchangia harusi unaofanana sana na wetu.

    Fadhili: Hapa China wenzetu huwa wanachangiana pesa kwa ajili ya harusi, lakini uchangiaji wake uko tofauti kidogo na ule wa kwetu. Kwanza sikumbuki kama wenzetu wana vikao vya harusi, kama vipo basi ni vidogo vodogo tu, na sikumbuki kama kuna mweka hazina na mambo mengi yanayohusu vikao. Michango ya harusi inasimamiwa zaidi na wenye harusi wenyewe, nakumbuka kuna rafiki yangu mmoja wakati anaona mchumba wake ndiye aliyekuwa anakusanya michango na hata kuangalia gharama na hata orodha ya waalikwa.

    Pili: Wenzetu wachina wanapotoa mchango huwa wanatoa bahasha nyekundu, ambayo ndani yake wanaweka pesa. Lakini hivi karibuni kuna mtu mmoja alitoa bahasha nyekundu ambayo haina pesa, lakini ndani yake aliandika ujumbe kumwambia rafiki yake anayeolewa "utanidai Yuan 800". Maana yake ni kuwa harusi ya rafiki yake ilifika wakati yeye hana pesa, lakini kwa njia moja aliona kuwa anahitaji kumchangia, kwa hiyo aliona ni bora ampe pesa baada ya harusi, kwa kuwa wakati huo hakuwa na pesa.

    Pili: Kama ilivyo kwa sisi waafrika, hapa China watu wameanza kujiuliza, hivi kumchangia mtu pesa ni lazima? Au ili kuonesha kuwa unamtakia mtu kila la heri kwenye harusi yake, ni lazima utoe pesa? Maswali haya yanafanya baadhi ya watu waanze kuona kuwa michango inakuwa kama ni malipo ya lazima, na sio kitu cha kumtakia heri mtu. Na ni kama sasa kinafikia kiwango cha kuwa kero kwa mchangiaji, na wala si mchango wa hiari nia mchango wa lazima na usiwe mdogo.

    Fadhili: Lakini kwa sisi waafrika naweza kusema tunasema mara nyingi tunapenda kuonesha kuwajali wenzetu pale wanapopata mtoto, na katika kipindi hicho watu wanatoa zawadi na pongezi nyingi, na baada ya hapo ni wakati wa ndoa, na baadaye ni wakati wa msiba. Lakini kutokana na mabadiliko kwenye jamii, inaonekana msiba bado una maana ile ile ya tangu zamani, kujitolea chochote unachoweza ili kumsindikiza marehemu, na watu wanajitoa wenyewe bila kujali wana nini mfukoni. Lakini harusi imekuwa ni jambo la kibiashara au kama shughuli ya kiuchumi.

    Pili: Hali hiyo naweza kusema kwenye suala la kuchangia harusi hapa China linaanza kuonekana pia kuwa jambo lenye utatanishi. Maana ukiangalia kiundani mtu unapoona au kuolewa ni jambo lako binafsi, wengine ni kuunga mkono kuonesha urafiki tu. Nadhani wanaosema unapoolewa mume ni wako, au unapoona mke ni wako, kwa hiyo wewe ndio unatakiwa kuingia gharama na sio wengine kuingia gharama. Kama mtu anachangia hata akichangia senti moja inatakiwa kuthaminiwa, sio michango ikiwa mikubwa ndio ithaminiwe.

    Fadhili: Labda naweza kusema hapa ndio tunaweza kuona hali fulani ya kufanana kwa tamaduni kati ya wachina na waafrika. Naona suala la harusi tunalichukulia kwa umuhimu unaofanana. Ukiangalia wenzetu wa magharibi unaweza kuona kuwa kwanza harusi ni jambo ambao linahusisha watu wachache sana, tena mtu anapooa au anapoolewa marafiki wanatuma kadi ya kumtakia kila la heri, na uzito wa kadi au maana yake inakuwa kubwa kuliko pesa. Labda wenzetu suala la maandalizi ya harusi si gumu kutokana na kuwa harusi ni jambo la watu wachache sana, sisi ni jambo la ukoo.

    Pili: Lakini tunatakiwa pia tukumbuke kuwa mambo yataendelea kubadilika, hasa kutokana na jinsi jamii inavyobadilika masuala haya yataendelea kuwa na mabadiliko. Kule nyumbani watu bado wana muda sana wa kwenda kwenye harusi na kufurahia sherehe ya harusi, hapa China kidogo hali hiyo inakuwa na mabadiliko. Mara nyingi ukiangalia watu wanaokwenda kwenye harusi unaweza kuona kuwa walio wengi ni watu wazima kwa kuwa wao wana muda mwingi wa ziada, tofauti na nyumbani ambako watu wengi wazima wanakuwa nyumbani na kuona mambo ya sherehe, ni ya vijana wenye nguvu.

    Fadhili: inawezekana ikafika wakati watu waanze kutambua kuwa hatutaweza kuingia kwenye ndoa kwa kutegemea msaada wa wengine. Ndoa sio suala la dharula kama msiba, kwa hiyo michango ni hiari na ni vizuri tukiendelea na utamaduni wa kufanya hiari si utumwa.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako