• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Wachina huwa wanafanya nini baada ya kazi?

    (GMT+08:00) 2014-08-11 15:50:47
    Wachina wanajulikana sana kwa kuwa wachapa kazi, na sisi waswahili tunasema "kazi na dawa", yaani baada ya kazi tunapumzika, na tunapopumzika huwa kunakuwa na mambo tunayofanya, wengine hucheza bao, wengine huimba nk..lakini wachina huwa wanafanya nini baada ya kazi? Kuwa nasi tukufahamishe.

    Jacob: Ni kweli kabisa kazi na dawa. Na kama ulivyosema wenzetu wachina wanatumia muda mwingi sana kufanya kazi, lakini kuna kitu kimoja ambacho bado hatukijui, baada ya kazi wachina wana njia nyingi ambazo ni tofauti sana na za sisi waafrika kupumzika na kuburudika, na hata mazingira yao yako tofauti sana.

    Fadhili: Ni kweli Jacob, unajua kule nyumbani Tanzania na hata Kenya mara nyingi baada ya kazi, shule au mkutano, kama watu wanapumzika mara nyingine tunakutana kwenye bia na nyama choma, na kuna wakati tunakwenda kucheza soka. Lakini hapa China kwanza michezo kama hiyo si maarufu sana, wao mara nyingi wanaalikana na kukutana kwenye mikahawa na kwenye baa, huko wanakula kunywa chai na hata kucheza michezo mingine kama karata.

    Jacob: Hili ni jambo ambalo wageni wengi wanaweza kushangaa wakija hapa China. Kule nyumbani kwenye nchi zetu ukiwa Nairobi au Dar es salaam, ukitembea karibu mita 500 unakuta baa na unakuta watu wanakunywa, lakini hapa China hali ni tofauti sana. Hapa kilichopo ni kuwa ukitembea kidogo unakuta mikahawa.

    Fadhili: Sisi huwa tunakwenda baa kunywa bia wakati mwingine hata kuangalia mechi za soka, lakini wenzetu wachina bia mara nyingi inanywewa wakati wa kula, hii ni tofauti kiasi na sisi watu wa Afrika au na hata watu wa sehemu nyingine duniani.

    Jacob: Lakini jambo lingine ni kuwa wenzetu wachina ni hodari sana kwenye kusoma, huwa wanasoma asubuhi wanapokuwa kwenye mabasi au subway, na vile vile hata wanapokuwa nyumbani wanapumzika wengine wanajitahidi kuendelea kusoma. Wao kusoma sio jambo la kwa ajili ya mitihani, vile vile ni jambo la kujiburudisha na kupitisha wakati. Lakini sisi kule nyumbani mara nyingi huwa tunasoma pale tunapojiandaa kwa mitihani.

    Fadhili: Kama ulivyosema kuna baadhi ya mambo ni tofauti. Kwa mfano wachina wengi kwanza huwa hawajumuiki majumbani, kujumuika majumbani kwao ni jambo la nadra. Mara nyingi hata wakiwa na marafiki huwa hawakutani nyumbani, wanakutana nje. Zamani tukisikia wachina wanasema nitakubaribisha chakula cha jioni tulidhani ni kama tunavyofanya sisi kule nyumbani, lakini wao maana yao ni kuwa tutaenda kula mahali halafu analipia chakula. Kidogo hii ni tofauti ya utamaduni.

    Jacob: Mara nyingi huwa baadhi ya watu wanajiuliza inakuwaje wenzetu wachina wanakusanyika sana kwenye bustani? Inakuwaje wachina wengi wanakusanyika kwenye maeneo fulani, sababu ni kuwa wenzetu pia huwa wanatumia muda wa mapumziko kutembelea sehemu mbalimbali kuangalia mandhari, kupiga picha na hata kufanya vitu kama pikniki. Sisi huwa kidogo hatufanyi hivyo.

    Fadhili: Kuna mengine naweza kusema ni utamaduni, Kwa mfano yanapofika majira ya joto, kwa kawaida watu wazima hapa China huwa wanakusanyika kwenye bustani au kwenye sehemu za wazi wanaweka muziki na kuanza kucheza kwa kufuatana. Hii huwa inaonekana asubuhi na jioni, lakini mara nyingi wanaofanya hivi ni watu wazima sio vijana. Kama kuna vijana, basi wanakuwa wachache sana.

    Jacob: Kule nyumbani watu wengi huwa wanafikiri kuwa ukija China, kila mtu anacheza kung fu, lakini ukweli ni kuwa si wachina wote wanaocheza kungfu ni wachina wachache sana. Lakini kitu ambacho ni wazi ni kuwa wachina wengine wanacheza mpira wa meza wakati wa mapumziko. Na ninaposema mapumziko sina maana tu mapumziko ya wikiendi, wakati mwingine hata wakati wa mapumziko ya mchana, kuna watu huwa wanakwenda kwenye sehemu zenye meza ya mchezo wa mpira wa meza halafu wanaanza kucheza.

    Fadhili: Hili naweza kusema ni jambo geni kwa waafrika wengi, lakini yapo baadhi ya mambo ambayo wachina wanapenda kufanya baada ya kazi au wakiwa na muda, ambayo kwa kiasi fulani yanafanana sana ya yale tunayofanya kule nyumbani kwenye nchi za Afrika. Kwa mfano kuna mchezo unaoitwa Mahjong, mchezo huu kimsingi ni kama bao au daft. Lakini watu wanakusanyika nje pamoja na kucheza. Mazingira kimsingi yanakuwa sawa na yale ambayo tumeyazoea wenye nchi zetu, lakini wanaofanya hivyo ni watu wazima vijana mara nyingi hawafanyi hivyo.

    Jacob: Nakumbuka hata mimi nilipoona hilo nilishangaa sana kuona kumbe hata wenzetu wachina nao wanakuwa nia vitu kama vijiwe vya wazee kule nyumbani, kuna wakati hata nilijisikia kama niko nyumbani, hasa nilipoona baadhi wanacheza huku wanakunywa chai.

    Fadhili: Lakini vile vile kuna mengine ambayo naweza kusema ni mageni kiasi, au kama yapo kwenye nchi zetu ndio kwanza yatakuwa yanaingia kwa sasa. Hapa China kuna kitu kinaitwa Karaoke, wengine wanapokuwa na nafasi wanakwenda wanajikusanya na kwenye karaoke. Huku kwenye karaoke ni kuwa wanasikiliza muziki wa ala halafu wao wanaimba kwa kufuatisha, hili ni jambo ambalo kule nyumbani ni geni kidogo. Nafahamu kuwa Nairobi kuna baadhi ya watu wanafanya biashara hii, lakini kwa Tanzania ni kama bado kidogo.

    Jacob: Sio hilo tu, labda hilo kweli bado ni geni kwa sisi waafrika. Lakini yapo mengine ambayo naweza kusema hata wasikilizaji wakisikia wanaweza kushangaa kiasi. Kuna siku katika pitapita zangu niliwaona wazee wachezea PIA, kama vile tulivyokuwa tuinafanya tulipokuwa watoto. Kwa hiyo ni kweli kuna michezo mingine kwa kweli inafanana sana na michezo ambayo wasikilizaji wetu watakuwa wameizoea.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako