• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Kadi maalum ya ukazi "Green card" ya China

    (GMT+08:00) 2014-08-11 15:52:27

    Katika kipindi cha leo tunazungumzia masuala ya ukazi kwa wageni hapa China, na pia tutazungumzia kadi maalum ya ukazi "Green card" ambayo wasikilizaji wetu wengi watakuwa wanaifahamu kwa kuwa ni utaratibu ambao Marekani inautangaza sana kama njia ya raia wengine kwenye kuishi na kufanya kazi Marekani. China pia ina utaratibu huu. Kuwa nasi basi tukufahamishe utaratibu huu kwa China ukoje.

    Pili: sheria na taratibu za ukazi kwa China naweza kusema kwa upande mmoja ni ngumu. Kwa sababu China bado ni nchi ambayo haijafunguliwa sana kwa wageni, yaani inaendelea kufungua mlango. Ni tofauti sana na nchi za Ulaya, Marekani au nchi za Afrika ambako mtu unaweza kuishi na kulowea. Lakini hapa China unaishi kwa kufanya kilichokuleta ukimaliza basi unaondoka. Sababu moja ni kuwa China ni nchi yenye idadi kubwa sana ya watu, haina upungufu wa watu, lakini ina upungufu wa watu kwenye maeneo fulani ndio maana imeweka utaratibu wa kukaribisha wageni

    Fadhili: Miezi miwili iliyopita Rais Xi Jinping alikutana na baadhi ya wafanyakazi wageni mjini Shanghai, kwenye mkutano huo alizihimiza idara mbalimbali za China ziboreshe utaratibu wa kuvutia wageni wenye vipaji kuja kufanya kazi hapa China. Utaratibu wa kadi ya kijani ya China ulianza mwaka 2004. Tangu wakati huo hadi sasa chini ya watu 5000 hivi ndio wamepata kadi ya hiyo, wengi walioomba wamelalamika kuwa utaratibu wa sasa wa kupata kadi hiyo ni mgumu, ndio maana Rais Xi aliagiza utaratibu uboreshwe ili kuruhusu wafanyakazi wageni wenye vipaji waweze kuja China kwa urahisi kufanya kazi.

    Pili: Kwa kweli utaratibu wa kadi ya kijani ya China ni mgumu. Tukijaribu kuangalia masharti ya kupata kadi ya kijani ya China, tukilinganisha na utaratibu wa Marekani au Canada, tunaweza kuona kuwa bado China iko nyuma sana, Marekani kwa mwaka inatenga kadi za kijani kwa wageni zaidi ya elfu 50 na Canada pia inatenga kiasi kama hicho. Na masharti yao ya kupata kadi hiyo si magumu sana kama China. Ndio maana ni chini ya watu 5000 hivi waliopata kadi ya kijani ya China.

    Fadhili: Hebu tuangalie kwanza tunaposema masharti haya ni masharti gani. Kwa utaratibu uliopo sasa, moja ya masharti haya ni kuwa unatakiwa uwe umewekeza hapa China zaidi ya dola laki 5 za Marekani, na kwenye biashara uliyowekeza inatakiwa upate faida kwa miaka mitatu mfululizo na biashara yako iendelee kuwa na faida.

    Sharti lingine ni kuwa uwe umefanya kazi kwa miaka zaidi ya minne kama naibu meneja mkuu, mkuu wa kiwanda, profesa mshiriki na mtafiri msaidizi. Mbali na hayo kama mume wako au mke wako tayari amepata kadi ya kijani, kama mmeoana kwa zaidi ya miaka mitano na kama umeishi China kwa zaidi ya miezi tisa pia unaweza kuomba kadi ya kijani. Lakini mbali na hayo ni lazima uwe na rekodi nzuri ya usalama na afya, kama ukitimiza masharti hayo unaweza kupewa kadi ya kijani.

    Pili: Kimsingi haya masharti ni magumu, kwa hiyo unaweza kuishi China kwa miaka mingi lakini usifikie vigezo vinavyotakiwa, na unaweza kuishi kwa muda mfupi na ukafikia vigezo. Kuna Profesa mmoja alisema ni wageni wachache sana wanaokuja China wakiwa na wakurugenzi au wakurugenzi wasaidizi kwa hiyo kimsingi ni kuwa wanaopata ruhusa hiyo ni wachache sana na wenye umri mkubwa, na walio wengi hawawezi kupata fursa hata ya kuomba kadi ya kijani.

    Fadhili: Vilevile ukiangalia kwa undani unaweza kuona kuwa China ni nchi ambayo kimsingi haina matatizo kama inavyokabiliana nayo Marekani au Canada. Nchi hizo zina ardhi yenye eneo kubwa lakini idadi ya watu wake ikilinganishwa na ukubwa wa ardhi yake ni ndogo. Lakini China ina idadi kubwa sana ya watu. Kanuni zilizowekwa na China ni zile zinazovutia watu wenye ujuzi maalum ambao China haina.

    Pili: Lakini vile vile kuna jambo moja ambalo tunatakiwa tukumbuke kuwa China iko wazi kwa wageni, wageni wengine wanakuja na kuishi China. Mkoa wa Guangdong umekuwa na mawasiliano na nje ya China kwa miaka mingi sana, kwa sasa kwenye mkoa huo kuna watu kutoka nchi mbalimbali wanaishi na kufanya kazi huko kwa muda mrefu, wengine wameona au kuolewa na wenyeji na wanaishi huko. Na kingine ni kuwa utaratibu wa kuja hapa China kwa wageni wanaotaka kufanya biashara ni rahisi, kwa hiyo kuja na kutoka, hasa kwenye masuala ya biashara, naweza kusema ni rahisi kiasi kuliko ilivyo kwenye nchi nyingine.

    Fadhili: NI kweli kuna baadhi ya miji ya China iko wazi sana kwa wageni. Kwa mfano kuna mji wa Yiwu, ambao ukienda huko ni sawa na kama uko kwenye nchi ya kiarabu, wageni kutoka nchi mbalimbali za kiarabu wanaishi huko kama kwao. Lakini kuna tatizo lingine ambalo naweza kusema ni kikwazo kwa watu kuja China ikilinganishwa na nchi za Ulaya na Marekani. Kwa mfano, watu kutoka Afrika ya kati na Magharibi wakienda Ufaransa na Ubelgiji inakuwa ni rahisi kwao kwa kuwa tayari wana msingi wa lugha ya utamaduni wa nchi hizo, au watu kutoka nchi zilizokuwa makoloni ya Uingereza inakuwa rahisi kwa wao kwenda na kuishi Uingereza, Australia au New Zealand. Lakini China haikuwahi kuwa na makoloni kwa hiyo haina mazingira kama hayo

    Pili: Lakini tunatakiwa kukumbuka kuwa nchi nyingi zinapovutia wafanyakazi wageni sababu kubwa inakuwa ni uhaba wa nguvu kazi, hapa China tatizo la uhaba wa nguvu kazi halipo, isipokuwa kuna tatizo la upungufu wa wataalamu kwenye maeneo fulani. Pamoja na kuwa utaratibu wa kadi ya kijani ni mgumu, haina maana kuwa watu wanaokuja kufanya kazi kwenye maeneo yenye upungufu wa wataalamu ni wachache.

    Fadhili: Lakini naweza kusema la muhimu ni kuangalia mahitaji ya nchi. China tatizo lake ni wataalam kwenye maeneo fulani, sio kama tatizo ni kuwa wananchi kubwa na haina watu wa kutosha. Hilo ni tatizo linalozikabili nchi kama Canada, kwa hiyo sera za Canada labda zinalingana na mahitaji yake na za China zinalingana na mahitaji yake.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako