• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Beijing kupiga marufuku watu kunywa, kula kwenye subway

    (GMT+08:00) 2014-08-15 17:36:15
    Leo kwenye kipindi hiki tunazungumzia sheria moja ya hapa Beijing iliyopiga marufuku watu kunywa, kula kwenye vitu vya subway, kulikuwa na habari pia sheria hiyo ilipiga marufuku hata kula kwenye lifti, lakini sheria hiyo ilibadilishwa miezi miwili tangu ilipopitishwa. Kuwa nasi tukufahamishe kuhusu sheria hiyo, kwanini iliwekwa na kwanini imeondolewa.

    Pili: Kwanza kulikuwa na mjadala mkubwa kuhusiana na sheria hiyo. Kwanza watu walioiunga mkono walikuwa na sababu za msingi, sababu ya kwanza ni kuwa watu wanakula vyakula ambavyo kwa kawaida havifai kuliwa kwenye sehemu za umma. Hapa nazungumzia vyakula vya michuzi au vyakula vinavyoweza kusababisha hatari kwa watu wengine, kama vile vyakula vya moto, au vyenye harufu, au ambayo vinaweza kuleta vijidudu vinavyoweza kwenda kwa abiria wengine. Na sheria ilikuwa inasema huruhusiwi kula au kunywa ndani ya subway kwenye kituo cha subway au hata karibu na subway. Watu waliounga mkono walikuwa wanaona kuwa hii ni hatua nzuri na inahakikisha usalama wa afya zao.

    Fadhili: sawa lakini kulikuwa na watu wanaopinga, na sababu ni kuwa kwanza inawezekana mtu unakwenda mbali na huwezi kuvumilia kwa muda mrefu kukaa ndani ya subway bila kula, kuna watu wanaamka saa 11 alfajiri wanapanda subway kwa muda wa karibu saa moja na nusu, na wakifika tu wanaanza kazi ofisini, hawana muda wa kutosha kukaa na kupata kifungua kinywa, wao muda mzuri ni kwenye subway, na kuna baadhi ya vyakula ambavyo vinaweza kuliwa bila matatizo kama mikate, au biskuti. Na hii ya kuzuia hata watu kunywa maji kidogo iliwakwaza baadhi ya watu hasa ukizingatia kuwa kuna wakati kunakuwa na joto sana kiasi kuwa huwezi kuvumilia kiu.

    Pili: Lakini tukiangalia kwa upande mwingine sisi watumiaji wa subway hapa Beijing na hata kwenye miji mingine ya China huwa tunakutana na mengi ambayo yanakera, kwa mfano unaweza kuona mtu anaingia na mishikaki au doufu ambayo ina harufu mbaya, hali hii kwa kweli inakuwa kero kwa baadhi ya watu. Unaweza kuona mtu ametoka mahali anakuja na chakula kina harufu, au wakati mwingine anadondosha michuzi, na mwingine anaenda kazini yuko safi anajikuta anachafuka kabla hata ya kufika ofisini. Kwa hiyo kwa upande fulani naweza kusema waliyoleta sheria hiyo walikuwa na maana nzuri, au waliokuwa na nia njema japo kwa upande fulani walivuka mpaka kiasi.

    Fadhili: Labda hilo hatuwezi kusema ni tatizo kubwa, tatizo kubwa ambalo linasumbua kutokana na usafi kwenye subway, na sio subway tu bali usafiri wa umma kwa ujumla hapa Beijing na sehemu nyingine za China ni uchafu. Mara nyingi nilikuwa nashangaa kuona uko kwenye subway au kwenye basi halafu watu wanafanya usafi, nilikuwa najiuliza kwanini wasisubiri hadi jioni? Kwa hapa Beijing kama ukiacha hadi jioni basi kuna wakati inaweza kuwa hatari, maana baadhi ya watu wanadondosha mifuko ya plastiki, wengine wanadondosha chakula, wengine wanadondosha michuzi sasa subway inaweza kuwa chafu. Na tatizo ni kuwa miji mikubwa ya China inakuwa na wahamiaji wengi toka vijijini ambao wengine wanakuwa na matatizo kwenye maswala ya usafi hiyo tukiangalia pande zote mbili zilikuwa sahihi

    Pili: Mara nyingi kunakuwa na mambo madogo madogo ambayo naweza kusema yanakuwa kero kwenye miji ya hapa China. Mambo haya naweza kusema yanaonesha pengo kubwa la ustaarabu au maadili ya watu. Ukiangalia watu wenye elimu na wasio na elimu, au ukiangalia wakazi wenyeji wa mijini na wale wanaotoka vijijini unaweza kuona kuna tofauti kubwa sana. Lakini huwezi kutenganisha watu hao, wanaishi pamoja na kutumia usafiri wa umma kwa pamoja kwa hiyo sheria kama hii inawabana wote, wale wenye maadili mazuri na wale wasio na maadili mazuri.

    Fadhili: Lakini ukiangalia hali halisi ya miji mikubwa ya China, hasa tukiangalia asubuhi wakati kuna abiria wengi sana wanaotumia subway, na tiketi unanunua kwenye mashine, mlango unajifungua wenyewe, kwenye kituo cha subway ndani labda kuna watu wawili au wanne, na abiria baadhi ya nyakati wanakuwa hata zaidi ya 500, kwa kweli kusimamia sheria kama hii ni changamoto kubwa sana. Kwa hiyo inaweza kuwa ni sheria ambayo iko kwenye makaratasi tu, lakini haiwezi kutekelezwa. Na ndani ya subway ndio vigumu zaidi kwa kuwa subway inakuwa na dereva mmoja na msaidizi wake, na abiria wanaweza kuwa hata zaidi ya 5000 na ndani ya mabehewa ya subway hakuna mtu anayeangalia umeshika nini au unakula nini, kwa hiyo inakuwa vigumu kusimamia utekelezaji wa sheria kama hii. Kwa hiyo sana sana inategemea hiari ya watu.

    Pili: Moja ambao tunatakiwa kuwafahamisha wasikilizaji wetu ni kuwa, kazi ya usafi hasa kwa mji mkubwa kama Beijing ni ngumu sana. Serikali za miji zinafanya kazi kubwa sana kujitahidi miji inakuwa safi na hata usafiri wa umma au sehemu za umma kwa ujumla zinakuwa safi. Mara nyingi tunasikia elimu kwa umma kuhusu usafi inatolewa, na hata watoto pia wanafundishwa toka mashuleni kuhusu usafi. Lakini hata kama idadi ya watu wanaopuuza kanuni rahisi za usafi ni ndogo, idadi ndogo kwa mji kama Beijing inaweza kuwa watu milioni moja au zaidi,

    Fadhili: Nakumbuka kuna wakati nilikuwa naangalia takwimu kuhusu takataka kama vile mifuko ya plastiki na chupa za maji, kiasi cha taka ni kikubwa sana. Na wakati sheria ilipopitishwa hapa Beijing kupiga marufuku kutoa mifuko ya plastiki bure, tulianza kuona mabadiliko ya haraka sana na mifuko ilianza kupotea. Mwanzoni watu walilalamika lakini baadaye wengine waliunga mkono hatua hiyo. Kwa hiyo hata hii sheria kuhusu kupiga marufuku watu kula ovyo kwenye usafiri wa umma, pamoja na kuwa imeondolewa inawezekana kuwa ikarudi kwa njia nyingine ambayo itakuwa rahisi kutekelezwa na bila shaka itakuwa na manufaa.

    Pili: Pamoja na kuwa wenzetu wanafikiria sheria kama hizo, hali halisi ni kuwa tatizo sio kubwa, labda ni kuwa na tahadhari tu ili lisiwe kubwa, na kama tulivyosema mwanzo, China ni nchi ambayo watu wake wana viwango tofauti vya elimu na hata ustaarabu, kwa hiyo hatua kama hizi ni za tahadhari. Ukipanda mabasi, subway, au ukiwa kwenye treni na hata ndege hali kwa ujumla ni nzuri. Na hata kwenye vituo vya treni, mabasi na Subway, na hata njiani tu, unaweza kuona watu wanapita na kuokota takataka, kwa hiyo wenzetu wako makini sana na usafi..

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako