• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Changamoto inayowakabili baadhi ya vijana wa China kuhusu ndoa

    (GMT+08:00) 2014-08-27 21:30:52

    Leo katika kipindi hiki tunazungumzia changamoto inayowakabili baadhi ya vijana kuhusu ndoa. Kutokana na sababu mbalimbali kama vile elimu, uwezo mdogo kiuchumi, ajira na kutojua hali ya baadaye kiuchumi itakuwaje, kuna baadhi ya vijana, wavulana kwa wasichana, huwa wanachelewa kuingia kwenye ndoa. Baadhi ya wazazi na hata ndugu, wakiona kijana amefika umri fulani (bila kujali amejiandaa vipi kiuchumi) wanashinikiza vijana kuingia kwenye ndoa. Hali hii sio kama tu iko kwenye nchi za Afrika, hata hapa China tunapoishi hali iko hivyo.

    Pili: Ndoa ni moja ya hatua muhimu kwa binadamu, na mara nyingi inapofikia suala la kuona au kuolewa kunakuwa na changamoto zake. Mara nyingi wazazi hujisikia wamekalimisha malezi ya watoto wao baada ya kuona watoto wao wana ndoa na wamepata watoto. Hapa China, kuna wazazi ambao wanawahimiza watoto wao kuoa au kuolewa ili waone kuwa wamekamilisha jukumu la kuwalea watoto wao, na wenzetu kwa wakati fulani hata huwa wanataka kuona watoto wao wana wajukuu na hata kuwasaidia kulea wajukuu.

    Fadhili: Jambo hili tukiangalia kwa juu naweza kusema lina uzuri wake, kwa kuwa wazazi nao wanakuwa na busara zao, kwenye jamii yetu Tanzania haya mambo pamoja na na kuwa ni ya kizamani bado yapo. Hebu tumsikilize msikilizaji wetu Mchana J Machana akitoa maoni yake.

    Sauti ya Mchana J Mchana

    Fadhili: Mchana J Mchana anasema kama hakuna mapenzi ndoa hazidumu. Hapa China kuna hali kama hiyo mtoto kuhimizwa au kushinikizwa kuingia kwenye ndoa. Bila kujali kama hilo ni jambo zuri au baya, hapa China lina changamoto zake. Kwanza watoto wanapelekwa shule wakiwa wadogo, na wengine wanamaliza wakiwa na karibu miaka 30 hasa wale wanaosoma masomo ya juu, na wakimaliza tu masomo na kuanza kazi, wazazi wanaanza mke, mume, mke mume, wakati kijana hapo anakuwa hata hana muda wa kutafuta mchumba anayefaa. Na siku hizi hapa China kuna baadhi ya watu kwa kweli hawana hata muda wa kutafuta wachumba kutokana na kubanwa sana kazini. Wazazi wao hilo hawaangalii sana, wanachojali ni ndoa na mjukuu.

    Pili: Mfano mzuri ni kwa msichana mmoja mwenye umri wa miaka 25 wa mkoa wa Jiangsu hapa China. Mama yake alimwahidi kuwa atampa dola 50 kila atakapokwenda kwenye "date" na mvulana, akitarajia kuwa binti yake anaweza kukutana na mvulana atakayempenda waanze uchumba, na kufunga ndoa. Mama huyo anaona binti yake ana kila kitu anachostahili kuwa nacho, elimu na kazi nzuri, isipokuwa mume. Kwa hiyo anajiona anatakiwa akamilishe jukumu la malezi ya binti yake kwa kuhakikisha kuwa anaolewa. Lakini msichana anaona mama yake anamshinikiza kiasi kwamba anakosa raha, na wakati fulani anajaribu kumkwepa mama yake.

    Fadhili: Kuna mfano mwingine, Baadhi ya vijana wanaambiwa na wazazi wao, sikukuu hii ya mwaka mpya uje na mchumba, kama hujaja nae basi tutasikitika sana. Wakati mwingine wanaanza kumkumbusha mtoto wao hata miezi sita kabla ya sikukuu yenyewe na wanasema kabisa tumewaandalia chumba na mkiwa huku tumewaandalia gari ya kutembelea na vitu vingi. Ndio maana kuna baadhi ya vijana hapa China huwa wanakodi wachumba, anamtafuta mvulana au msichana, anampa pesa kiasi anaenda nae kwao hata wanakaa kwa siku mbili au tatu nyumbani kwa wazazi wao, halafu wanaondoka wakirudi mijini kila mtu anaendelea na mambo yake.

    Pili: Hali hii ni shinikizo kwa vijana. Kuna msichana mmoja mwenye umri wa miaka 29 alisema siku hizi anakwepa sana kwenda kwao, sababu ni kwamba wazazi wake na ndugu zake huwa wanamshinikiza awe na mchumba, na wakati mwingine akiwa kwao huwa anakutanishwa na wanaume hata watatu kwa siku, ili kuona kama japo anaweza kuchagua mmoja. Lakini mwaka jana wakati wa sikukuu alikwenda hospitali na kumwambia daktari kuwa anaumwa, baada ya daktari kumuuliza akagundua kuwa tatizo ni kuwa msichana ana msongo wa mawazo, kutokana na shinikizo kutoka kwa wazazi wake, na yeye alikuwa anajaribu kuwakwepa wazazi wake.

    Fadhili: Lakini tukiangalia kwa undani tunaweza kuona kuwa shinikizo la wazazi linatokana na upendo kwa watoto wao, lakini mazingira ya siku hizi kwa vijana kidogo ni magumu, na kama kijana akiingia kwenye ndoa ambayo haipendi kunakuwa na matatizo. Nakumbuka kuna rafiki yangu mmoja baba yake alikuwa anawindana na baba yake, anaamka saa 11 asubuhi anaondoka, anarudi usiku sana, siku nyingine halali nyumbani anakuja ru kubadilisha nguo, hadi siku mmoja baba yake alipoagiza watu kuwa akionekana nyumbani asiondoke, ili waongee. Nilimuuliza Bw Francis Mwangobola wa Dar es salaam, Tanzania kama kuna madhara kwa mzazi kuhimiza mtoto kuoa au kuolewa.

    Sauti Francis Mwangobla

    Pili: Naona hapa Bw Francis ameangalia upande wa mahari, lakini si wakati wote wazazi wanahimiza binti aolewe kwa sababu ya mahari. Mfano mzuri ni hapa China, si suala la mahari tu, wazazi wengine wanaona binti akiolewa au mvulana akiona wanakuwa wamekamilisha jukumu la malezi, na wakipata wajukuu basi wanakuwa wanafurahi sana.

    Fadhili: Labda tunaweza kusema maoni yao ni ya mtazamo wa wanaume au wavulana. Wasikilizaji wetu wengine wa klabu ya Kemogemba kule Tarime, nao walitoa maoni yao kuhusu ndoa za kushinikizwa, kwanza ni Grace na mwingine na Nchago

    Sauti Grace, Nchego

    Fadhili: Grace amesema msichana hatakuwa na furaha kwenye ndoa, na anaweza kufanya mambo yasiyofaa, na Nchego amezungumzia sababu za kibiolojia. Bahati nzuri kwa hapa China mambo haya mawili ni nadra kutokea, hasa la watu kuchezea ndoa. Kwa wachina hata kama hupendi ndoa yako, ukiingia kwenye ndoa hiyo ina maana unakubali kuiheshimu, hata kama chungu. Kama kuna wasioheshimu ndoa basi ni wachache sana, na hili la watoto kujifungua wakiwa na umri mdogo hapa China naweza kusema halipo, kama lipo labda hatujawahi kusikia. Kwa hiyo wenzetu haya mawili si matatizo makubwa sana.

    Pili: La muhimu naweza kusema tusiwalaumu sana wazazi wanapotoa shinikizo, si wakati wote wanataka mahari, wengine wanataka kuona watoto wao wana ndoa, na wazazi pia wanatakiwa kujua kuwa siku hizi vijana wana mawazo na mitazamo yao kuhusu ndoa. Cha muhimu ni kutafuta njia inayokubalika kwa wote.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako