• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Kenya na China zaendelea kushirikiana katika sekta ya elimu

    (GMT+08:00) 2014-08-29 10:52:34

    Wanafunzi 69 kutoka nchini Kenya wanatarajiwa kujiunga na vyuo mbali mbali hapa nchini China kuanzia tarehe tatu Septemba ili kupata elimu ya juu chini ya mpango wa ufadhili wa masomo baina ya serikali za Kenya na China.

    Wanafunzi hao ambao watakuwa wakisomea kozi tofauti za digrii ya kwanza, shahada ya uzamili na uzamivu, wameandaliwa sherehe ya kuagwa na ubalozi wa China nchini Kenya pamoja na kukabidhiwa stakabadhi za kuingia nchini China Kusoma.

    Baada ya kupata alama A katika mtihani wa kidato cha nne, Tom Mwai alikosa matumaini hasa baada ya kukosa fedha za kuendelea na masomo yake, katika chuo kikuu nchini Kenya kutokana na umaskini. "Sikuwa na matumaini maishani, kila kitu kilikuwa kimevunjika." Alisema Tom Mwai

    Lakini sasa Tom ana haja ya kutabasamu kwani ni mmoja kati ya wakenya 69 ambao watawasili hapa China tarehe tatu Septemba, kusoma chuo kikuu baada ya kupata ufadhili wa masomo ya uhandisi wa kuunda ndege, nchini China.

    Wanafunzi hawa wamepata ufadhili kutoka serikali ya China katika mpango wake wa kila mwaka wa kuwapa wanafunzi werevu fursa ya kusoma nchini, katika taaluma mbali mbali fursa inayolenga maendeleo ya kielimu na teknolojia, kwa wakenya.

    Akiongea katika sherehe hiyo ya kuwaaga wanafunzi hao Balozi wa China nchini Kenya Liu Xianfa amesema elimu ni nguzo muhimu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, na kuwataka wanafunzi hao kutumia fursa hiyo kupata elimu ya kujiendeleza wao wenyewe pamoja na nchi yao ya Kenya.

    "Miaka 35 ya mabadiliko ya haraka ya kimaendeleo nchini China, yanaonyesha kwamba elimu inaweza kuleta mabadiliko chanya ya kitaifa. Na kwangu mimi binafsi ni kwamba elimu inaweza kuwawezesha watu kufikia malengo yao maishani. Na hiyo ndio sababu kuu ya kuwa China imekuwa ikiunga mkono maendeleo ya kielimu nchini Kenya." Anaeleza Balozi Liu Xianfa

    Idadi ya wanafunzi wa Kenya ambao hupewa ufadhili huo iongezeka kila mwaka na kulingana na katibu wa kudumu katika wizara ya elimu ya Kenya Bi. Collette Suda, ni kwamba Kenya inatarajia kuendelea kushirikiana na China katika sekta ya elimu, na maendeleo ya teknolojia na katika sekta nyinginezo.

    "Ushirikiano huu wa China na Kenya haupo tu katika sekta ya elimu pekee, bali pia katika sekta nyingine nyingi za kiuchumi na maendelo. Lakini elimu ni muhimu pia kwa hivyo tunahitaji hiyo elimu mnayoenda kusoma nyinyi na walioenda kabla yenu ili tuitumie kuendeleza nchi." Anasema Profesa Collette Suda

    Naye mkurugenzi wa elimu nchini Kenya katika kanda ya Asia Duncan Anindo amewataka wanafunzi hao kuelewa kwamba, China ni taifa lililo na fursa nyngi na wanafaa kuzitumia vilivyo.

    Aidha amewataka kuheshimu sheria na tamaduni za China, na kuwa mabalozi wa Kenya nchini humo.

    "Ama kweli ufadhili huu wa masomo mnaopata kwenda China ni ishara ya uhusiano wa kuridhisha kati ya nchi zetu mbili. Na kwenu nyinyi wanafunzi mnaokwenda nje, nataka mfahamu kwamba mnaenda kwenye ulimwengu wenye fursa na nafasi nyingi, na kuna afasi nyingi za ajira kwenu wote iwapo mtajitolea kusoma kwa bidii. Mtakuwa mabalozi wa Kenya na Kenya inawatarajia mheshimu sheria na utamaduni wa China wakati wa masomo yenu huko." Anafafanua Mkurugenzi Anindo Duncan

    Bi Lucy Kiuti ni mwenyeji wa Pwani ya Kenya na atakuwa akifanya shahada ya uzamivu katika somo la uhandisi, na anasema lengo lake kuu baada ya masomo ni kwenda na kuwekeza nchini kwake Kenya, pamoja na kuisaidia nchi yake kuendelea kama China.

    "Baada ya masomo nigependa kurudi Kenya, nifanye kazi kwa kuwa tunajua kwamba China imekua kwa haraka sana, kwa hivyo kuna mengi ya kusoma nchini China. Na nigependa niende huko nisome halafu nije hapa nchini ili niendelee kuijenga Kenya." Anasema Lucy Kiuti

    Evans maina ni mmoja wa wanafunzi ambao wamefaidika na mpango kama huu, na amesomea shahada ya uhandisi wa nyumba. Alijiunga na Chuo kikuu cha Dalian na anasema kusomea China amefunguka macho. "Kwa kusomea nchini China nimefunguka akili sana, na nimejifunza mengi sana hususan katika taaluma hii ya uhandisi." Anaeleza Evans Maina.

    Waswahili wanasema elimu ni ngao na kwa wanafunzi ambao wamepata fursa hii tayari ngao wameipata.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako