• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Rais Kenyatta yuko The Hague kuhudhuria kikao maalum leo

    (GMT+08:00) 2014-10-08 15:58:29

    Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya leo saa tano asubuhi atasimama mbele ya majaji wa mahakama ya kimataifa ya jinai ya ICC katika tukio muhimu maishani mwake ambalo huenda likasababisha kuanza au kufutwa kwa kesi dhidi yake.

    Nje ya mahakama hiyo, Kenyatta atalakiwa na mamia ya wakenya, wengi wao wakiwa wamekwenda The Hague kama ishara ya umoja na kumtia nguvu, wengine wanaoishi The Hague na sehemu nyingine.

    Miongoni mwa wanaotarajiwa kumpokea mahakamani ni pamoja na wabunge na mawaziri ambao wamesafiri nae Uholanzi jana. Hata hivyo ataingia katika milango ya mahakama peke yake. Baadhi ya wabunge na maafisa wa serikali ambao wamejiandikisha kwa mahakama hiyo watapewa nafasi katika eneo la umma ndani ya mahakama, na wengine watabaki nje. Mawakili wataingia mahakamani kupitia mlango mwengine, na pengine kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miezi 18, Kenyatta hatakuwa na wasaidizi wala maafisa wa usalama. Atakuwa pekee na mawakili wake wakati akihojiwa na mwendesha mashtaka mkuu Bi Fatou Bensouda na maafisa wengine wa mashtaka na majaji watatu. Kikao hicho maalum ambacho kimeanza leo, kitajadili mambo mazito ya binafsi yanayomhusu Bw Kenyatta na kesi dhidi yake, jambo ambalo majaji walihitaji uwepo wake. Kwa mujibu wa afisa wa masuala ya kisheria wa ICC Daphne Vlachojannis, kikao hicho maalum kina mambo mawili muhimu katika ajenda. Moja ni ombi la Bw Kenyatta kuwa kesi dhidi yake itupiliwe mbali kwa ukosefu wa ushahidi. Hata hivyo mwendesha mashtaka mkuu Bi Fatou Bensouda amepinga na kusema kuwa, kesi hiyo isifutwe kwa sababu Kenya imeshindwa kutoa taarifa muhimu, na kumlaumu rais Kenyatta kwa hilo. Jambo la pili ni ombi la Bensouda kwa mahakama hiyo kuahirisha kesi hadi pale Kenya itakapotoa taarifa muhimu kuhusiana na masuala binafsi ya rais Uhuru Kenyatta.

    Afisa wa masuala ya sheria wa ICC Daphne Vlachijannis amesema kuwa, kikao hicho maalum kitajadili maombi hayo mawili kutoka kwa mawakili wa Kenyatta na kutoka kwa mwendesha mashtaka. Amesema majaji watatoa uamuzi kuhusiana na mambo hayo kila mmoja kivyake na kwa uwazi.

    Bensouda amesema kuwa, rais Kenyatta anapaswa kubeba jukumu kwa serikali yake kushindwa kutekeleza maombi ya ICC. Lakini mawakili Steven Kay na Gillian Higgins wamemlaumu mwendesha mashtaka huyo kwa kutaka kuahirisha kesi hiyo ambayo alisema wazi kuwa hana ushahidi wa kutosha kumshtaki mteja wao. Uamuzi utakaotolewa leo huenda ukaahirisha kesi hiyo au kufuta mashtaka dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta.

    Akihutubia bunge mnamo siku ya jumatatu, rais Kenyatta alizuia kutolewa kwa taarifa zenye ushahidi ambazo mwendesha mashtaka anazitaka kutoka serikali ya Kenya. Alisema yeye na mawakili wake hawakuhusishwa katika majadiliano kati ya mwendesha mashtaka na serikali.

    Bw Kenyatta alimkabidhi madaraka naibu rais William Ruto mnamo siku ya jumatatu ili ahudhurie kikao maalum cha leo kama raia wa kawaida. Aidha aliwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta kama abiria wengine, na alikwenda The Hague kwa kutumia ndege ya kawaida ya abiria.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako