Katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, makampuni yenye kipato cha zaidi ya yuan milioni 20 kwa mwaka katika eneo la ustawishaji wa sayansi na teknolojia la Zhongguancun hapa Beijing kwa ujumla yalipata mapato ya yuan trilioni 1.4, ambayo yaliongezeka kwa asilimia 15.8 kuliko mwaka jana wakati kama huu, na faida za makampuni hayo zilikuwa asilimia 8.1, ambazo ziliongezeka kwa asilimia 1.5 kuliko mwaka jana. Wakati ongezeko la uchumi wa masoko mapya linapopungua, na uchumi wa China unapokabiliwa na shinikizo kubwa zaidi la kushuka, eneo la Zhongguancun likitegemea uvumbuzi, limepata maendeleo mazuri.
Mtaa wa biashara wa Zhongguancun ulifunguliwa mwezi Juni mwaka huu. Makampuni zaidi ya kumi yanayotoa huduma kwa wawekezaji yakiwemo mkahawa wa Cheku na kampuni ya 36Kr yamefunguliwa kwenye mtaa huu, na kuwavutia wawekezaji wengi. Mtaa huu unatoa huduma za aina mbalimbali kwa wawekezaji hao, teknolojia mpya na taswira nzuri zinaweza kutumiwa, na makampuni madogo na ya wastani yanaweza kupata fursa za kujiendeleza.
Naibu mkurugenzi wa kamati ya usimamizi wa Eneo la ustawishaji wa sayansi na teknolojia la Zhongguancun Bw. Yang Jianhua alisema si makampuni na wawekezaji tu, bali pia wasimamizi wa eneo hili wanapata mawazo mapya. Maana mpya ya makampuni yanayoleta uvumbuzi ni mfano mzuri. Anasema,
"Kuchukua mkahawa wa Cheku kuwa ni kampuni inayoleta uvumbuzi kumeleta maoni mengi tofauti. Tunapojadiliana na idara husika, maofisa wengi wanaona kuwa mkahawa unawezaje kuwa kampuni inayoleta uvumbuzi? Hii inamaanisha kuwa tunatakiwa kuondoa mawazo ya zamani, kampuni yoyote inayoweza kutoa huduma kwa wawekezaji kufanya uvumbuzi, inaweza kuchukuliwa kuwa kampuni inayoleta uvumbuzi."
Habari zinasema katika miaka ya hivi karibuni, uwezo wa makampuni ya sayansi na teknolojia za hali ya juu ya eneo la Zhongguancun umeinuliwa kwa kiasi kikubwa, na mapato ya makampuni mbalimbali maarufu yakiwemo Lenovo, Jingdong, Xiaomi na Baidu yamekaribia yuan bilioni 100.
Katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, thamani ya jumla ya mauzo nje ya China ya bidhaa za makampuni yenye mapato zaidi ya yuan milioni 20 katika eneo la Zhongguancun ilikuwa dola za kimarekani bilioni 15.24, ambayo iliongezeka kwa asilimia 23.7 kuliko mwaka jana. Na eneo hilo limeonesha imani kubwa ya kufanya uvumbuzi katika kuidhinisha makampuni ya sayansi na teknolojia za hali ya juu. Bw. Yang anasema,
"Tumechagua njia isiyoathiriwa sana na maoni ya watu katika kuidhinisha makampuni ya sayansi na teknolojia za hali ya juu. Sehemu zinazoamuliwa na waatalamu zimepungua kuwa asilimia 20 kutoka asilimia 40. Hatua hii haimaanishi kuwa tumeshusha vigezo vya kutoa idhini, bali tunataka kufanya majaribio ya kutoa idhini kwa vigezo vinavyoendana na makampuni ya sayansi na tkenolojia za hali ya juu."
Kazi muhimu ya kutekeleza mikakati ya kujiendeleza kwa uvumbuzi ni kushughulikia vizuri uhusiano kati ya serikali na soko, kulifanya soko liwe nguvu ya kugawanya raslimali za uvumbuzi, na kuyawezesha kihalisi makampuni kufanya uvumbuzi wa teknolojia. Hivi sasa wasimamizi wa eneo la Zhongguancun wanajitahidi kuanzisha mazingira mazuri ya kisera, na kuongeza utoaji huduma kwa makampuni na wawekezaji.
Kampuni ya 36Kr inayoshughulikia akili bandia ilianzishwa katika eneo la Zhongguanzhun kwa mwaka mmoja tu lakini mali zake zimezidi yuan bilioni 1. Afisa mtendaji mkuu wa kampuni hiyo He Bofei anasema,
"Tulipowasiliana na viongozi wa kamati ya usimamizi wa eneo la Zhongguancun, tuligundua jambo la kufurahisha. Kila mara walipokutana na sisi katika kampuni yetu, hawakuchelewa hata mara moja, na kabla ya kuja, walituuliza kama tuna nafasi au la ili wasisumbue kazi zetu."
Faharisi ya Zhongguancun ya mwaka 2014 iliyotolewa hivi karibuni inaonesha kuwa, mwaka jana faharisi ya jumla ya eneo la Zhongguancun ilifikia 242.1, ambayo ni kubwa kuliko ile ya mwaka juzi kwa 47.5. Wataalamu wamesema data hizi zinaonesha kuwa mazingira ya uwekezaji katika eneo la Zhongguancun yameboreshwa siku hadi siku, na uwezo wa makampuni wa kufanya uvumbuzi pia umeinuliwa hatua kwa hatua. Eneo la Zhongguancun linapiga hatua madhubuti katika kutimiza lengo la kuwa kituo cha uvumbuzi wa sayansi na teknolojia chenye ushawishi mkubwa duniani.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |