• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mtaalamu wa mpunga Yuan Longping kufanya majaribio mapya ya mpunga chotara mkoani Xinjiang

    (GMT+08:00) 2014-10-15 15:45:19

    Mpunga chotara uliooteshwa na mtaalamu wa taasisi ya uhandisi ya China Yuan Longping umepata maendeleo mapya, ambao uzalishaji wake umezidi tani 15 kwa hekta. Lakini mtaalamu huyu wa kilimo anayesifiwa kuwa "baba wa mpunga chotara" hajaridhika na mafanikio hayo, na ametunga mpango wa kufanya majaribio mapya mkoani Xinjiang, na kutumia teknolojia ya kumwagilia maji kwa matone.

    Bw. Yuan Longping anasema, ana hamu kubwa ya kutumia teknolojia hii. Anaona kuwa uzalishaji wa mpunga chotara kuzidi tani 15 kwa hekta ni maendeleo makubwa, lakini majaribio mapya mkoani Xinjiang yakipata mafanikio, uzalishaji huo huenda utaongezeka kwa asilimia 15 hadi 20. Bw. Yuan amechagua mashamba ya majaribio yenye ukubwa zaidi ya hekta 10 mkoani Xinjiang.

    Tarehe 27 Agosti, Bw. Yuan Longping alikwenda mjini Shihezi mkoani Xinjiang, na kukagua mashamba ya vielelezo yanayotumia teknolojia za kumwagilia maji kwa matone ambayo yanamilikiwa na taasisi ya kilimo ya Tianye, ili kujua aina za mbegu, kiasi kilichopandwa katika shamba lenye ukubwa fulani, na matumizi ya maji na mbolea. Anaona kuwa teknolojia hii ambayo inaweza kukabiliana na ukame, kubana matumizi ya maji, na kuweka mbolea wakati wa kumwagilia maji, hakika inasaidia kuongeza uzalishaji.

    Mkuu wa taasisi ya kilimo ya Tianye Bw. Chen Lin alifahamisha kuwa, wakulima wanaweka mbolea kwenye maji, na kumwagilia moja kwa moja kwenye mizizi ya mazao, hatua hii inasaidia kupunguza matumizi ya mbolea, kuinua ufanisi wake na kupunguza uchafuzi wa ardhi.

    Bw. Chen pia amesema, teknolojia ya kumwagilia maji kwa matone imebadili hali ya kilimo cha jadi cha mpunga ambacho kinategemea umwagiliaji maji na udongo maalum. Sasa matumizi ya maji yamepungua kwa theluthi moja ya yale ya zamani. Wakulima hawahitaji tena kukausha mashamba kwa siku chache, na kupunguza utoaji wa hewa zinazosababisha kuongezeka kwa joto duniani. Wakulima pia hawana haja ya kuweka matuta kwenye mashamba, na kubana matumizi ya ardhi kwa asilimia 5 hadi 7. Aidha, maji yanayomwagiliwa hayasambai eneo lote shambani, na kuzuia kuenea kwa wadudu.

    Teknolojia hii pia imerahisisha hatua za kupanda mpunga. Wakulima hawana haja ya kuotesha mimea kwenye sehemu maalum halafu kupanda mimea mashambani, sasa wanahitaji kupanda mbegu moja kwa moja mashambani. Wakati matumizi ya maji yanapobanwa, uzalishaji unaweza kuongezeka kwa asilimia 20.

    Taasisi ya kilimo ya Tianye ilianza kushughulikia teknolojia ya kumwagilia maji kwa matone mwaka 2004. Baada ya kufanya majaribio katika mashamba madogomadogo na kutatua matatizo mbalimbali, mwaka 2009 taasisi hiyo ilianza kufanya majaribio katika mashamba makubwa ya vielelezo, na wastani wa uzalishaji ni tani 7.5 kwa hekta.

    Bw. Chen Lin anasema, mwaka huu uzalishaji huo umefikia tani 12.5. Teknolojia hii pia imeanza kufanyiwa majaribio mikoani Ningxia, Jiangsu na Liaoning.

    Bw. Yuan Longping alipozungumzia sababu ya kufanya majaribio mkoani Xinjiang, alisema kuhakikisha uzalishaji mkubwa wa mpungua kunahitaji mambo manne. Kwanza ni aina nzuri ya mbegu, pili ni kufanya kazi kwa makini, zikiwemo kupanda, kuweka mbolea na kuua wadudu, tatu ni ardhi yenye rutuba, nne ni mazingira mazuri ya kimaumbile. Mkoa wa Xinjiang una rasilimali za kutosha za jua, na tofauti kubwa ya joto kati ya mchana na usiku, mazingira hayo mazuri yanasaidia ukuaji wa mpunga.

    China ina historia zaidi ya miaka 6000 ya kilimo cha mpunga. Matumizi ya maji katika kilimo cha jadi cha mpunga yanachukua zaidi ya theluthi mbili ya matumizi yote ya maji katika mambo ya kilimo. Lakini teknolojia ya kumwagilia maji kwa matone imeondoa tatizo la matumizi makubwa ya maji, hivyo hakika italeta faida kubwa ya kiuchumi.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako