• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • China bado ni nchi inayopata oda nyingi za bidhaa za sikukuu ya Krismas mwaka huu

    (GMT+08:00) 2014-10-29 09:34:35

    Kampuni ya Shunmei ya mjini Quanzhou mkoani Fujian ni kampuni maarufu ya kuzalisha mapambo ya fuwele yanayotumiwa katika sikukuu ya Krismas. Baada ya kukabiliwa na shinikizo la kupanda kwa gharama ya nguvu kazi kwa miaka mingi, mwishoni mwa mwaka jana kampuni hii ilianza kuzalisha bidhaa kwa teknolojia ya uchapishaji wa 3D. Teknolojia hii si kama tu imeondoa tatizo la nguvu kazi, bali pia imepunguza muda wa kutengeneza sanamu ambao zamani ulikuwa siku 4 hadi 5 kufikia muda usiozidi siku moja sasa.

    Meneja wa idara ya mauzo ya nje ya kampuni hiyo Bw. He Zhiying anasema, ingawa hali ya soko la kimataifa si nzuri, lakini uagizaji wa bidhaa za sikukuu ya Krismas wa mwaka huu umeongezeka kwa asilimia 30 kuliko mwaka jana. Bw. He amefahamisha kuwa, teknolojia mpya imeiwezesha kampuni hiyo izalishe sanamu nzuri zaidi, na kuinua uwezo wa ushindani katika soko. Wateja wengi wa kampuni hii ni makampuni 500 yenye nguvu kubwa zaidi duniani, na wameridhika na maumbo na rangi za bidhaa za kampuni hii.

    Maonesho ya bidhaa ya Guangzhou ambayo yalishirikisha makampuni elfu 25 ya China yameingia kipindi cha pili, na vifaa vya michezo ya watoto, mapambo, na vitu vya kauri vimekuwa bidhaa muhimu zinazooneshwa kwenye maonesho hayo. Makampuni mengi ya China yameonesha sanamu za Santa Claus, miti ya Krismas, sungura wa Pasaka na modeli za magari. Watu wameshangaa kuona kuwa makampuni yanayozalisha mapambo ya Krismas ambayo yalidhaniwa kupoteza uwezo wa ushindani siku hadi siku bado yana uhai mkubwa. Kutokana na matumizi ya teknolojia mpya na mageuzi ya mikakati ya mauzo, China bado itaongoza katika soko la bidhaa za sikukuu ya Krismas katika siku zijazo.

    Takwimu zilitolewa na forodha ya China zinaonesha kuwa, kuanzia Januari hadi Septemba mwaka huu, mauzo ya mashine na vyombo vya umeme nje ya nchi yameongezeka kwa asilimia 4 tu, lakini thamani ya bidhaa zinazozalishwa kwa nguvu kazi nyingi zikwemo nguo, viatu, samani, plastiki, masanduku, mifuko na vitu vya kuchezea watoto ilikuwa yuan trilioni 2.21, ambayo iliongezeka kwa asilimia 4.9 kuliko mwaka jana. Ongezeko hili pia ni kubwa kuliko ongezeko la jumla la mauzo ya bidhaa nje.

    Naibu mkuu wa shirika la viwanda vyepesi la China Bw. Li Wenfeng amesema, kutokana mabadiliko ya gharama ya uzalishaji nchini China na marekebisho ya muundo wa shughuli duniani, baadhi ya kampuni zimehamishia shughuli zao sehemu nyingine duniani kutoka China, lakini hali hii haimaanishi kwamba China imepoteza uwezo wa kushindana katika shughuli hizi, bali baadhi ya makampuni yamepata fursa mpya kutoka mabadiliko hayo.

    Meneja wa mauzo wa kampuni ya vitu vya kuchezea watoto ya Tongshuo mkoani Zhejiang Bw. Zhou Guanghua anasema, thamani ya mauzo ya kampuni yake ambayo bidhaa nyingi zinauzwa katika masoko ya Ulaya na Marekani inatazamiwa kuzidi dola za kimarekani milioni 100. Baada ya idadi ya wafanyakazi kufikia 1200, kampuni hiyo inatilia mkazo zaidi usanifu wa bidhaa. Sasa imeanzisha ofisi ya usanifu nchini Marekani, na imetenga yuan milioni 10 kwa kazi ya usanifu kila mwaka.

    Bw. Zhou amesema, kushindana kwa ghama ndogo ya uzalishaji ni jambo lisilowezekana sasa kwa makampuni ya vitu vya kuchezea watoto. Kutenga fedha sawa na asilimia 3 hadi asilimia 5 ya thamani ya mauzo katika kazi ya usanifu ni mkakati unaotekelezwa na makampuni yote yanayotengeneza vitu vya kuchezea watoto.

    Ofisa wa shirika la viwanda vyepesi la China amesema, mauzo ya bidhaa za viwanda vyepesi nje yanasaidia kusukuma mbele uchumi wa China, kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje, na kutatua matatizo ya ajira. Shirika hilo linapoviongoza viwanda vyepesi vihamie sehemu za kati na magharibi mwa China, limechukua hatua mbalimbali kutangaza chapa za bidhaa za China.

    Baadhi ya makampuni yanaona kuwa mabadiliko ya orodha za bidhaa za sikukuu ya Krismas yameyafanya makampuni ya China kutambua kwamba yanatakiwa kutafuta maendeleo ya muda mrefu yenye uwiano zaidi katika soko la kimataifa kwa kutumia fursa za kipindi cha mageuzi. Meneja mkuu wa kampuni ya biashara ya kimataifa ya Hongyeyongwei ya mkoa wa Jiangsu Bw. Huang Lintao amesema, kampuni yake imejenga viwanda nchini Cambodia na Bangladesh ili kushughulikia uzalishaji wa bidhaa za kiwango cha chini, na yamefanya usanifu na uzalishaji wa bidhaa za kiwango cha juu nchini China. Bidhaa mpya za kampni yake zimeanza kuuzwa katika soko la Ujerumani, na kampuni hiyo pia imepanua uagizaji bidhaa za kiwango cha juu kutoka nje.

    Bw. Huang amesema, makampuni ya China yana wafanyakazi wenye ustadi mkubwa na mistari kamili ya uzalishaji, hivyo bado yana uwezo wa kushindana sokoni katika siku za baadaye, lakini hii haimaanishi kuwa, China itakuwa nchi inayopokea oda nyingi za bidhaa za sikukuu ya Krismas daima, hivyo kampuni yake inatilia mkazo kuendeleza shughuli zake katika soko la ndani na kuongeza uagizaji wa bidhaa kutoka nje.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako