• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Rais Kenyatta akutana na Bw. Ban Ki-Moon

    (GMT+08:00) 2014-10-30 21:08:36

    Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya jana jioni alifanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Umoja Mataifa Ban Ki-moon na Rais wa Benki ya Dunia Jim Yong Kim katika ikulu ya Nairobi. Mazungumzo yao yalilenga maendeleo na jukumu la Kenya katika kukuza utulivu wa kikanda.

    Fursa ya kukutana na Katibu Mkuu wa Umoja Mataifa imechukuliwa na wengi kama faida na ishara nzuri kwa Kenya, hasa ikitiliwa maanani hapo awali Marekani na nchi za magharibi zilitoa vitisho vya kutoshirikiana na Kenya iwapo Kenyatta angechaguliwa kuwa rais kutokana na kesi aliyo nayo katika Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai ya The Hague.

    Baada ya mkutano wao, Rais Kenyatta, Ban Ki-moon, na Rais wa Benki ya Dunia Jim Yong Kim walifanya mkutano wa pamoja na waandishi wa habari. Rais Kenyatta alishukuru msaada wa dola 8.3 bilioni za kimarekani kutoka kwa taasisi za kimataifa za kusaidia kukuza amani na miradi ya maendeleo katika nchi za Pembe ya Afrika. Aidha rais Kenyatta alisema Kenya itaendelea kusaidia kuleta amani na kusuluhisha nchi zilizo na mizozo. Amesema Kenya inaendelea kutoa msaada wa rasilimali ya utaalamu katika kazi ya kujenga ukanda thabiti ambao unashirikiana kiuchumi kwa ajili ya kufikia mafanikio ya watu wa kanda hiyo.

    Naye katibu Mkuu wa Umoja Mataifa Ban Ki-Moon aneipongeza Kenya kwa kuonyesha ujasiri na ari ya kupambana na ugaidi, na kusema kuwa alipendezwa na alichokiona wakati alipotembelea kambi ya wakimbizi ya Dadaab, kambi kubwa ya wakimbizi iliyo nchini Kenya. Amesema Kenya imeonyesha ujasiri na kujitolea dhidi ya kupambana na ugaidi baada ya shambulizi la Westgate na matukio mengineyo. Aliongeza kuwa haiwezekani kuwa na maendeleo katika kanda iwapo hakuna amani na usalama. Akizungumzia suala la mlipuko wa Ebola Afrika magharibi, Ban Ki-Moon alisema Ebola ni tatizo la dunia nzima, na ushirikiano wa kikanda unahitajika ili kupambana na ugonjwa huo. Ameeleza kufurahishwa na ahadi zilizotolewa na nchi nyingi za Afrika za kupeleka wahudumu wa afya kwenye nchi zilizoathiriwa na ugonjwa huo, lakini pia amezitaka nchi hizo kutowawekea karantini wahudumu hao pindi wanaporejea nchini kwao.

    Kwa upande wake Rais wa Benki ya Dunia Jim Yong Kim alimhakikishia Rais Kenyatta kuwa Benki ya Dunia itasaidia na kuunga mkono mipango ya maendeleo na amani. Pia amempongeza rais Kenyatta kwa juhudi zake za kutafuta amani na usalama wa kikanda ili kutoa fursa kwa jamii za Pembe ya Afrika kushiriki katika shughuli za kiuchumi zenye faida ili kuboresha maisha yao.

    Miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Rais wa Benki ya Maendeleo ya kiislamu Ahmed Mohammed Ali na mshauri wa rais wa Benki ya maendeleo ya Afrika (AfDB) Youssouf Ouedraogo. Umoja wa Ulaya uliwakilishwa na Naibu Mkurugenzi wa kamisheni ya Ulaya anayehusika na maendeleo na ushirikiano, Marcus Cornaro.

    Jumatatu wiki hii mjini Addis Ababa, Ethiopia, viongozi hao walitoa ahadi ya msaada wa kisiasa na kifedha kwa ajili ya nchi za Pembe ya Afrika, ikiwa ni pamoja na ufadhili wa dola za kimarekani biliobi 8 ili kusaidia ukuaji wa uchumi na fursa, kupunguza umaskini na kuongeza shughuli za biashara katika nchi nane za Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Somalia, Sudan, Kenya, Uganda na Sudan Kusini, ambazo ziko kwenye Pembe ya Afrika.

    Hii leo katika makao makuu ya UNEP jijini Nairobi, Ban Ki-Moon atazindua mradi wa kupinga ukeketaji kwa wanawake.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako