• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Sekta ya uchukuzi ya Afrika kupata maendeleo endelevu

    (GMT+08:00) 2014-10-31 12:10:12

    Mchakato mpya wa kihistoria unaozingatia maendeleo endelevu katika sekta ya uchukuzi barani Afrika umezinduliwa katika makao makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia mazingira UNEP Jijini Nairobi.

    Machakato huo umezinduliwa rasimi na rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na katibu mkuu wa Umoja huo wa Mataifa Ban Ki Moon Jijini Nairobi.

    Kulingana na UNEP mchakato huo mpya unalenga kuleta mpango wa uchukuzi ambao, utakuwa unazingatia maendeleo endelevu kote barani Afrika.

    Katika uzinduzi huo mawaziri 42 kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika, wamewakilisha mataifa yao.

    Mchakato huu unalenga kuleta pamoja mipango kabambe ya uchukuzi katika mataifa ya bara la Afrika, kuhakikisha kuwa linapunguza uharibifu wa mazingira ambao unatajwa kuwa na athari kubwa, kwa maisha ya binadamu na viumbe wengine.

    Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta aliyehudhuria uzinduzi wa mchakato huo, anasema ili hayo kufikiwa wadau wote, wanafaa kuhusishwa kikamilifu.

    "Ili kufikia malengo ya maendeleo ya Afrika, tunataka wadau wote wahusishwe, kutoka serikalini, mpaka kwenye mashirika ya serikali, sekta binafsi, wasomi, washirika wa kiutafiti, mashirika ya kifedha na mashirika ya kijamii kwa pamoja na uzuri ni kwamba wengi wa wadau hawa wapo hapa leo katika kikao hiki, hakikisho la lengo letu sote la kuwa na kila mmoja katika safari yetu ya kimaendeleo." Anasema rais Uhuru Kenyatta.

    Aidha rais Kenyatta anasema ikiwa ni mara ya kwanza kwa mawaziri wa uchukuzi na mazingira kutoka mataifa ya bara la Afrika, kukutana inaonyesha nia iliyopo ya kufikia lengo hilo.

    "Ni mara ya kwanza kwa mawaziri wa uchukuzi na wale wa mazingira kukutana, watakuwa wakishauriana katika hadhi ya Kimataifa barani Afrika, kujadili mambo muhimu katika sekta ya uchukuzi kama vile mipango na sera, kuhakikisha uchukuzi unaozingatia maendeleo endelevu barani Afrika, hivyo ni tumaini langu kuwa mpango huu utakapo kamilika na kuanza kufanya kazi utapata mwanya katika mipango ya kila nchi na kufanya kazi." Anaeleza rais Uhuru Kenyatta.

    Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon anasema hata baada ya uchumi wa Afrika ukiwa unaendelea kukua kwa asilimia kubwa, kuna nafasi ya mataifa ya bara hili kukwepa maafa, yanayotokana na maendeleo ya kisasa yanayotokana na njia mbaya za kimaendeleo.

    "Na kama vile uchumi wa Afrika unaendelea kukua, kuna fursa za kukwepa uharibifu wa kijamii, kimazingira na kiuchumi ambao huja na uchukuzi usiozingatia maendeleo endelevu. Kulingana na takwimu kutoka Shirika la Afya Duniani WHO ni kwamba kama vile mkurugenzi wa UNEP Achim Steiner alivyosema watu milioni 7 kila mwaka hufa mapema kutokana na uchafuzi wa mazingira kama vile matumizi ya magari yanayotumia mafuta yanayochafua mazingira katika viwango vikubwa na hayo hayakubaliki kwa kuwa tuna suluhu yake." Anasema Ban Ki Moon.

    Takwimu zinaonyesha kuwa uchafuzi wa mazingira kwa mfano Jijini Nairobi, uko mara saba zaidi ya viwango vinavyokubalika na shirika la WHO, na ndio maana rais wa Kenya anasema wakati huu, ni muhimu kwa kila mmoja barani kuhusiana na agenda 2063.

    "Sisi sote tumekutana hapa wakati ulio muhimu sana kwa bara la Afrika, na pia kwa mpango tulio nao wa agenda 2063 wa maendeleo barani Afrika. Mpango huu unalitaka bara letu la Afrika kufanya mpango ulio mahususi wa kujikuza pamoja na maendeleo endelevu ya kukua kwa Afrika. Pia mpango unataka sisi tufanye mambo tofauti na awali kufikia ruwaza yetu ya Afrika ambayo ina maendeleo na amani. Aidha mpango huu wa agenda 2063 unaoyesha wazi kabisa umuhimu wa mpango wa uchukuzi kama sekta muhimu katika kujikuza kijamii na kiuchumi." Anafafanua Uhuru Kenyatta

    Wakati huo huo katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amezipongeza serikali za Afrika, kwa kuchangamkia mchakato huo wa kutaka kuweka mipango mipya ya uchukuzi, inaozingatia maendeleo endelevu, akisema watazungumzia zaidi uunganishwaji wa uchukuzi katika katika Mkutano wa wiki ijayo Jijini Vienna Austria.

    "Katika kikao cha mataifa ambayo yameendelea yasiyo na bahari wiki ijayo Vienna Austria, tutakuwa na fursa ya kuangazia kwa mapana na marefu kuhusu uunganishwaji wa uchukuzi barani Afrika" Anaeleza Ban Ki Moon.

    Na kama ambavyo amesema rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, ni kwamba iwapo mipango hiyo itawekwa vizuri, bara hili litaweza kufikia malengo yake ya mwaka 2063.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako