• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Ndoa kati ya wachina na waafrika imekuwa ni sehemu ya kubadilishana utamaduni

    (GMT+08:00) 2014-11-13 14:16:12

    Huku ushirikiano wa kibiashara kati ya Afrika na China ukiendelea kuongezeka, maingiliano na mawasiliano ya utamaduni kati ya watu wa pande zote mbili pia unakua siku hadi siku.

    Ndoa ni aina mojawapo ya mifano ya kuonyesha jinsi wachina na waafrika wanatangamana.

    Hivi karibuni mwandishi wetu Ronald Mutie alihudhuria harusi ya Yue Yujiao kutoka China na Olusegun Adekanmi kutoka Nigeria . Hii hapa ripoti yake.

    Ijumaa kwenye ubalozi wa Nigeria mjini Bieing-China.

    Yue Yujiao kutoka China na Olusegun Adekanmi kutoka Nigeria wanafunga pingu za Maisha.

    Wanajiunga rasmi na jumuiya ya familia za China-Afrika zinazoishi hapa Beijing.

    Baada ya kuchumbiana kwa miaka mitatu, mahaba yao leo yamefanywa kuwa rasmi kwa kuvishana pete na kupewa vyeti vya kuwa mume na mke.

    "Nakupenda mpenzi wangu wangu-----nakupenda pia" wanaambiana kwenye harusi yao iliyohudhuriwa na wageni wachina na waafrika.

    Adekanmi ambaye ameishi China kwa miaka sita anasema hajaona lolote la kumzuia kuoa mchina.

    "Tulipoanza kuchumbiana nilimwambia sijali kuhusu utamaduni ..na huo ndio ukweli mimi sijali kabisa na leo nina furaha sana mambo yote yamefanikiwa"

    Mwanzoni, Yue Yujiao alikuwa na uoga kiasi wa kuwa na mchumba wa kiafrika lakini baada ya kukolea kwenye mapenzi ya Odekanmi yuko tayari kuandamana na mume wake hadi nchini Nigeria.

    "Nina jina la Kinigeria …..naitwa Anike tumejuana na bwana yangu kwa muda sasa , tunaaminiana na la muhimu zaidi tunaelewana"

    Siku hadi siku ndoa za aina hii zimeendela kupata umaarufu hapa china na zimekuwa dhihirisho kwamba utamaduni sio kikwazo cha mapenzi duniani.

    Bwana Jiang Wei kutoka Beijing amekuwa akienda Afrika mara kwa mara kwa shughuli za kibiashara.

    Yeye kama wachina wengi hakuwa na ufahamu mkubwa kuhusu mila na tamaduni za Afrika hususan swala la ndoa.

    "mwanzoni lilikuwa ni jambo la kushangaza kuona mwafrika amefunga ndoa na mchina, kusema kweli ilikuwa ni kitu cha kuvutia watu lakini sasa sio hivyo, dunia imefunguka na mambo yamebadilika"

    Kwa kuwa sasa limekuwa ni jambo la kawaida kwa watu wa pande zote mbili kuoana, mamake Yujiao anaamini kwamba familia ya Adekanmi itamtunza vyema bintiye kama tu ilivyo pia na wakwe wengi wa jamii za kiafrika.

    "Sisi wote ni familia moja na nawaomba watu wa nchi hizi mbili kuendelea kuwa marafaiki zaidi "

    Katika miji ya Beijing na Guangzhou nchini China, ni jambo la kawaida kuona ndoa kati ya mchina na Mwafrika.

    Baada ya harusi tunatembelea familia nyingine kati ya mchina na Mnigeria.

    Shui Li Fang na bwana yake Ole Chuku walioona miaka 16 iliyopita na wamejaliwa watoto watatu.

    "Nampenda baba yangu sana, ni mtu mwema" anasema binti yao wa kwanza mwenye umri wa miaka 9.

    Li Fang anasema haoni tofauti kuolewa na mwanaume kutoka sehemu yoyote duniani muhimu kwake ni mapenzi, kuelewana na kulea familia.

    "Tumeoana kwa muda mrefu na hata sijaiona familia yangu kwa kipindi chote hicho"

    Kila siku mume wake anamfunza maneno machache ya kiigbo ili watakapokwenda kwao Nigeria mwaka ujao awe na ufahamu wa kutoa salamu.

    Watoto wao watatu ndio furaha kubwa katika familia hii.。。wanapenda kumtania baba yao wakati wa chakula cha jioni.

    Takwimu zinaonyesha kwamba kuna kati ya wanaume 50 na 60 wa Nigeria ambao wameoa wachina.

    Haijakuwa rahisi kuwianisha tamaduni za pande zote mbili na kulea watoto kwenye mazingira ya tamaduni mseto lakini mambo yanaonekana kuendelea vyema kwa sasa.

    Huku biashara kati ya Afrika na china ikiongezeka kwa zaidi ya dola bilioni 200 za kimarekani, pia uhusiano wa watu kwa watu unapiga hatua kupitia kwa ndoa kama hizi…na inaonekana muziki wa kiafrika utachezwa hata zaidi kwenye harusi za mchina na mwafrika.


    1 2 3
    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako