• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • China yaahidi kuheshimu ahadi yake ya kupunguza utoaji wa hewa chafu

    (GMT+08:00) 2014-11-26 18:14:55

    Serikali ya China imetoa ahadi mpya kuwa itakaheshimu nia yake ya kupunguza utoaji wa hewa chafu ifikapo mwaka 2030. Ahadi hiyo imetolewa wakati ujumbe wa China unajiandaa kuelekea kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya hewa utakaofanyika nchini Peru wiki ijayo. Fadhili Mpunji anaeleza zaidi

    Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Hali ya Hewa utakaofanyika mjini Lima unafuatia China na Marekani kufikia makubaliano makubwa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa wakati wa mkutano wa APEC uliofanyika mwanzoni mwa mwezi huu hapa Beijing. Kama sehemu ya makubaliano hayo, China imekubali utoaji wake wa hewa chafu utashuka kuanzia mwaka 2030, pamoja na asilimia 20 ya umeme wake kuzalishwa kwa kutumia vyanzo endelevu kabla ya muda huo.. Naibu mkurugenzi wa kamati ya maendeleo na mageuzi ya China Xie Zhenhua anasema,

    "Miaka 16 sasa imebaki kabla ya kufika mwaka 2030. Kuna mengi yasiyofahamika mbeleni, ikiwemo maendeleo na rasilimali za kiuchumi na kijamii. Naamini kuwa lengo lililowekwa la mwaka 2030 ni la kisayansi na linatekelezeka. Tuko wazi kuwa tutajaribu kadri ya uwezo wetu kufikia lengo hilo mapema, kama inawezekana. Hii inaonyesha nia thabiti ya China kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa kwa hatua za uhakika"

    Wakati huohuo, ujumbe wa China kwenye mkutano ujao wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Hali ya Hewa utakaofanyika nchini Peru, unasema unataka kuona vitendo halisi kutoka kwa dunia nzima linapokuja suala la mabadiliko ya hali ya hewa. Kiongozi msaidizi wa ujumbe wa China Su Wei anasema,

    "Serikali ya China inatarajia kuwa mkutano wa Lima utatekeleza makubaliano yaliyofikiwa awali kwa pande zote ili kuongeza vitendo kabla ya mwaka 2020. Nchi zilizoendelea zinapaswa kupunguza utoaji wa hewa chafu kihalisi, vilevile kuheshimu ahadi zao za kuziunga mkono nchi zinazoendelea kwa kutoa fedha, kuhamisha teknolojia, na kuzijengea uwezo"

    Wakati huohuo, amesema nchi zilizoendelea bado hazijatekeleza ahadi zilizotoa katika mkutano wa Copenhagen za kukusanya dola bilioni 100 za kimarekani kwa mwaka itakapofika mwaka 2020, ili kuunga mkono mapambano dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa kwa nchi zinazoendelea. Tangu mwaka 2011, serikali ya China imetoa zaidi ya dola za kimarekani milioni 40 kwa mfuko unaolenga kuzisaidia nchi zinazoendelea kukabiliana na masuala yanayohusiana na mabadiliko ya hali ya hewa.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako