• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Umoja wa Mataifa watoa wito wa juhudi za pamoja katika ulinzi wa haki za binadamu za watu wenye asili ya Kiafrika

    (GMT+08:00) 2014-12-11 19:00:57

    Umoja wa Mataifa umezindua Muongo wa Kimataifa wa Watu wenye Asili ya Afrika kwa lengo la kuongeza uelewa wa watu kuhusu ubaguzi wa rangi ambao watu hao bado wanakabiliana nao hivi sasa. Akizungumza kwenye hafla hiyo, Rais wa Mkutano wa Baraza la Umoja huo Bw Sam Kutesa amesema, katika miaka kumi ijayo, watu wote duniani watatakiwa kushiriki kwenye mazungumzo ya kimataifa kuhusu hali inayowakabili watu wenye asili ya Afrika.

    Bw Kutesa amesema, muongo huo utatoa fursa kwa Umoja wa Mataifa kutafiti changamoto zinazowakabili watu wenye asili ya Kiafrika kutokana na kuenea kwa ubaguzi wa rangi ambao umeenea katika jamii ya sasa. Bw Kutesa ameongeza kuwa, ni lazima hatua thabiti zichukuliwe katika ngazi za kitaifa na kimataifa ili kuchangia mafanikio dhahiri katika maisha ya mamilioni ya watu wenye asili ya Kiafrika duniani.

    Tarehe 23 Desemba ya mwaka jana, mkutano Mkuu wa Baraza la Umoja wa Mataifa ulipitisha azimio la kuanzishwa kwa Muongo wa Kimataifa kwa Watu wenye Asili ya Kiafrika, ambao utaanza rasmi Januari Mosi mwakani na kumalizika Disemba 31, 2024. kauli mbiu ya Muongo huo ni "Watu wenye Asili ya Kiafrika: kutambuliwa, haki, na maendeleo"

    Kipindi hicho cha miaka 10 kitatoa fursa ya kutungwa kwa sheria zinazopinga ubaguzi na kuhakikisha haki kwa kupambana na adhabu zinazotokana na rangi ya mtu. Pia itasaidia kuinua haki ya maendeleo na fursa sawa ya kupata elimu, huduma za afya na ajira.

    Kuhusu suala la haki, Bw Kutesa amesema watu wenye asili ya Kiafrika mara nyingi wanakuwa wahanga wa uhalifu na vurugu, na wanakumbana na ubaguzi katika jitihada zao za kutafuta haki kisheria. Kwa upande wa maendeleo, Bw Kutesa amesema jumuiya ya kimataifa imetambua uhusiano uliopo kati ya umasikini na ubaguzi wa rangi. Licha ya ushahidi wa wazi wa mchango wa watu wenye asili ya Kiafrika katika maendeleo ya jamii, mara nyingi watu hao huwa wanatengwa.

    Bibi Valerie Amos, naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya kibinadamu na uratibu wa mambo ya dharura amesema, watu wenye asili ya Kiafrika wanasumbuliwa na ukosefu wa usawa na kutopewa nafasi kutokana na historia ya utumwa ,na ni moja kati ya watu masikini zaidi duniani wakiwa na ukosefu wa huduma za afya, elimu, na hata ajira.

    Kwa upande wake msaidizi wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia haki za binadamu Bw Ivan Simonovic amesema, haki za binadamu ni za watu wote, na muongo huo unalenga kutoa mwanga kuhusu ukosefu wa usawa, kutoonekana, maendeleo duni, ubaguzi, na vurugu katika kila bara.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako