• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Katuni ya kwanza iliotiwa sauti ya Kiswahili yaanza kuonyeshwa Afrika mashariki

    (GMT+08:00) 2015-01-23 16:43:02

    Kwa muda mrefu watazamaji wa vibonzo ama katuni Afrika mashariki wamezoea kuona katuni za kiingeeza, lakini siku hizi vibonzo vya Kiswahili vimeanza kupenya kwenye runinga. Hivi karibuni kampuni ya kutoa huduma za televisheni ya Startimes iliweka sauti ya Kiswahili katuni moja kwa ajili ya channeli yake ya Kiswahili na inalenga watazamaji wa Afrika mashariki. Katuni hiyo inayoitwa Poppycat ina zaidi ya wahusika 7 na inahusu hali ya kawaida ya michezo ya watoto kucheza jamii.

    Wahusika wote waliotia sauti wanatoka Afrika Mashariki. Khatib Mjaja anaigiza uhusika wa Egbert ambaye ana shughuli nyingi na hapendi kushirikiana na wengine. Anasema Egbert kama muhusika kwenye katuni hiyo, anaonekana ni mwenye tabia za kipekee na pia anapenda kusababisha matatizo kwenye kundi na kujitenga. Kwenye hali ya kawaida inaonyesha kwamba kuna watoto ambao wanapenda kushirikiana na wenzao na wengine hawapendi. Amesema kuwa, si vizuri kwa watoto kuwa na tabia kama ya Egbert.

    Vipindi vya katuni hutumika kuwafurahisha na kuelimisha watoto. Kwa kawaida huigizwa na wataalam wanaosomea kazi hiyo na kama tamthilia, maisha ya kawaida ya mhusika hayana uhusiano kabisa yale ya kuigiza.

    Wahusika pia wanabadilisha sauti ili kuendana na ile ya vibonzo inayowavutia watoto. Khatib Mjaja anasema jamii isimwangalie kama inavyomuona Egbert kwenye tamthilia hiyo, kwani kwenye maisha ya kawaida, yeye ni Khatib Mjaja na anapenda kushauriana na watu, na kama kiongozi, anapenda zaidi kusikiliza, kutoa ushauri, kuelekeza, na pia kuikosoa jamii.

    Mhusika mwingine kwenye tamthilia hii ni Robert Ochola ambaye anaigiza kama Zuzu. Ingawa yeye hajasomea kazi hiyo, uwezo wake wa kubadili sauti ulimwezesha kuchaguliwa. Anaona pia katuni ya Kiswahili ni muhimu kwa watoto wa Afrika mashariki. Hakuwahi kudhani kwamba atafanya kazi kama hiyo ya kuigiza katuni, na anahisi kama ameuvaa uhusika wa kitoto na kuelewa jinsi watoto wanachukulia mambo na vile hisia zao zinalingana na yale maneno ambayo yamo ndani ya katuni. Katuni ya Kiswahili inakuza lugha na mtoto anapoiangalia mbali na kufurahia anajifunza lugha kwa njia nyingine. Kwa mtazamo wake, Robert anasema hii ni njia ya kuwafurahisha watoto na pia kuwafunza maadili.

    Katuni hii ina sehemu 52 na kila moja ina dakika kumi.

    Kanda ya Afrika mashariki ina zaidi ya watu milioni 130 wanaozungumza Kiswahili. Bi Claire Zhu ambaye ni mhariri wa Kiswahili katika kampuni ya Startimes, anasema wanahitaji vipindi zaidi vya Kiswahili kwa ajili ya channeli yao inayotazamwa kwenye kanda hiyo. Amesema mwanzoni katuni hiyo ilikuwa ya kiingereza kutoka Uingereza, walivutiwa nayo na kuinunua na kuweka sauti ya Kiswahili. Siku za baadaye, anatarajia kampuni hiyo itaweka sauti za Kiswahili kwenye katuni nyingine nyingi kama vile Author King, huku wakiwalenga zaidi watazamaji watoto, wazazi na waalimu wao.

    Ingawa Startimes bado haijatayarisha vipindi vingi vya kiswahili, kuwepo kwa katuni hiyo ni sehemu ya uhusiano wa sanaa na vyombo vya habari unaondelea kuongezeka siku hadi siku kati ya China na Afrika.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako