• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Kazi ya kuunda baraza jipya la mawaziri nchini Afghanistan yakabiliwa na vikwazo

    (GMT+08:00) 2015-01-23 18:53:43

    Inaelekea kuwa serikali ya Afghanistan itaendelea kuendeshwa na kaimu mawaziri baada ya bunge la chini la nchi hiyo kukataa baadhi ya mawaziri waliopendekezwa na rais Ashraf Ghani wa nchi hiyo. Baada ya rais huyo mpya wa Afghanistan kuapishwa aliahidi kuwa angeunda baraza jipya la mawaziri ndani ya siku 45, lakini imechukua siku takriban 110 tangu kuapishwa kwake Septemba 29 mwaka jana, kuunda baraza la mawaziri lenye mawaziri 25 na kuteua mkurugenzi wa usalama wa nchi hiyo pamoja na mkurugenzi wa Benki Kuu ya Afghanistan. Baraza hilo lilitangazwa rasmi jumanne wiki hii. Pili Mwinyi anaeleza zaidi

    Vyombo vya habari vya Afghanstan vinasema, wakati wa mchakato wa kuwapitisha wateule hao, jumatano wiki hii baraza la chini la bunge la Afghanistan liliwakataa mawaziri 7 waliopendekezwa kwa kuwa wana uraia wa nchi mbili. Bunge hilo limemtaka rais Ghani kuteua mawaziri wengine kuziba nafasi zao. Mawaziri waliokataliwa ni pamoja na wale waliopendekezwa kusimamia wizara muhimu kama vile ulinzi, mambo ya ndani, na mambo ya nje.

    Mbunge Abdul Qayum Sajadi anasema, ingawa kati ya mawaziri walioteuliwa kuna wengine wenye taaluma na uwezo mkubwa, wananchi wanaonekana kutoridhishwa na orodha ya mawaziri. Bw Sajadi anasema, si vigumu kupata watu 25 wenye taaluma na uwezo wasio na uraia wa nchi mbili kati ya watu milioni 30 wa Afghanistan. Naye mchambuzi wa masuala ya kisiasa Najib Paikan nchini humo anasema, hatua ya baraza la chini la bunge la Afghanistan kukataa uraia wa nchi mbili inapaswa kupongezwa. Profesa Tahir Hashimi wa Chuo Kikuu cha Kabul anasema, ugumu wa kuundwa kwa baraza la mawaziri kunaonyesha kuwa bado kuna tofauti ndani ya serikali ya umoja. Amesema, kwa mtazamo wake baraza hilo ni la umoja na kwa kawaida baraza kama hilo linaweza kuvunjika wakati wowote. Ameongeza kuwa inaweza kuchukua wiki hata miezi kadhaa kumaliza mchakato wa kuwachunguza mawaziri wateule ila tu kama serikali itateua kati ya watu wasio na tatizo la uraia wa nchi mbili.

    Uchaguzi wa rais wa Afghanistan ulifanyika April 5 mwaka jana, na kwa kuwa hakuna mgombea yeyote kati ya wanane waliokuwa wanawania nafasi hiyo aliyepata asilimia zaidi ya 50 za kura, duru ya pili ya uchaguzi ilifanyika Juni 14 kati ya Ashraf Ghani na Abdullah Abdullah ambao walikuwa na kura nyingi zaidi.

    Kwa kuwa wagombea hao walisema uchaguzi huo haukuwa wa wazi, waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry alifanya ziara nchini humo mara mbili kutafuta mwafaka wa suala hilo. Kutokana na upatanishi wake, mwafaka ulifikiwa kuwa Ghani atakuwa rais wa Afghanistan na Abdullah Abdullah kuwa mtendaji mkuu wa serikali, nafasi ambayo ni sawa na waziri mkuu.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako