Gareth Bale asema ataendelea kuwepo Real Madrid
(GMT+08:00) 2015-01-29 14:01:37
Winga wa Real Madrid Gareth Bale amefutilia mbali uwezekano wa yeye kujiunga na klabu ya Manchester United kwa kusema haoni nafasi yake klabuni hapo na kwamba ana furaha kuendelea kuitumika timu yake ya sasa ya Real Madrid. Kumekuwa na tetesi kuwa nyota huyo atajiunga na Manchester united huku kipa David De Gea akielekea Real Madrid kama sehemu ya mpango huo. Bale alijiunga na Real Madrid kwa ada ya uhamisho ya pauni milioni 85 iliyovunja rekodi ya usajili mwezi septemba 2013. Mchezaji huyo wa zamani wa Tottenham alilaumiwa na baadhi ya mashabiki wa Madrid kwa kumnyima pasi Cristiano Ronaldo kwenye michezo dhidi ya Espanyol. Akizungumzia uhusiano wake na Ronaldo nyota huyo wa kimataifa wa Wales alisema hakuna uadui kati yao. Bale amefunga mabao 36 na kusaidia kutoa pasi za mabao 26 katika michezo 72 aliyoichezea Real Madrid.